Home Makala Tatizo si Mkapa wala Kikwete…Ni ahadi zao

Tatizo si Mkapa wala Kikwete…Ni ahadi zao

882
0
SHARE
  • Na Magufuli je?Mkapa na Kikwete

RAIS Mstaafu, Benjamin Mkapa, alimaliza muda wake wa kuliongoza Taifa hili na kuondoka. Kwa hakika alifanya mazuri mengi kwa Watanzania. Hakuna anayeweza kutilia shaka uzalendo wake na mapenzi yake kwa Taifa hili.

Kama alivyowahi kuandika mwandishi mashuhuri wa masuala ya jamii, Padri Privatus Karugendo, katika Rai namba 633 mwaka 2006, Rais Mkapa atakumbukwa kwa mengi, mazuri na mabaya.

Waliokubaliana na kila alichokifanya watamkumbuka kwa mema daima. Wale watakaokuwa wakweli na kuona kwamba kuna aliyoyafanya mazuri, na kuna mabaya pia watapima.

Vivyo hivyo ndivyo tunavyompima Rais Mstaafu mwingine aliyemfuata, Jakaya Kikwete. Wote hawa kama mazuri yatazidi mabaya, basi mabaya yatafunikwa. Vilevile kama mabaya yatazidi mazuri, hayo mazuri yatafunikwa. Ingawa binadamu tulivyo, baya moja linaweza kufunika mema hata kama ni 1,000.

Kama alivyosema Padri Karugendo, ukweli ni kwamba wanafiki tu ndio watakaosema kuwa kila walichokifanya marais wastaafu hawa ni kizuri. Kwa bahati mbaya namba ya wanafiki ni kubwa.

Watajitahidi kuyafunika mabaya na kuyataja mazuri. Kwa kweli watu kama hawa hawalisaidii Taifa katika kuweka kani (force) ili  maendeleo yake yaje kwa kasi, hasa kwa Taifa kama letu ambalo bado ni changa na linahitaji kukua kwa kila hali.

Na wale watakaosema kuwa kila walichokifanya ni ovyo, nao hawatawatendea haki pia. Na si kwamba hawatawatendea haki marais wastaafu wetu hawa, bali pia hawatalitendea haki Taifa letu waliloliongoza kwa kipindi cha miaka 10 kila mmoja na kuiacha Tanzania ikivuma kwa mataifa ya nje au vinginevyo, na hasa washirika wetu katika maendeleo ambao kwa lugha nyingine huitwa wafadhili.

Ni kweli kabisa kwamba yapo mazuri mengi yaliyotendeka wakati wa awamu zao, ni mengi mno pengine kuwa vigumu kuyaoredhesha yote. Lakini pia yapo mambo mengi yaliyoikera mno jamii ambayo hawakuyatimiza au kuyaondoa.

Kila rais kabla au mara tu baada ya kuingia Ikulu, huwapa matumaini makubwa wananchi katika masuala fulani yanayowakera, na pengine ambayo wanakuwa wamekata tamaa nayo katika maisha yao ya kila siku.

Kwa Tanzania, masuala ambayo yanawakera wananchi ni kadhaa, lakini suala ambalo kwa sasa wamekata tamaa nalo ni tatizo la rushwa na ufisadi. Wagombea urais wote hawa walilisemea tatizo hili wakati wa uongozi wao.

Mara tu baada ya kuchaguliwa kuiongoza Tanzania mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa alihojiwa na mwandishi mmoja maarufu wa Kiingereza, David Martin, ambaye wakati huo alikuwa akiishi Zimbabwe. Kwa sasa ni marehemu.

Miongoni mwa maswali ambayo mwandishi huyu alimwuliza Rais Mkapa lilihusu rushwa, na alijibu: “…Lazima ufike mahali ambako ili kuuthibitishia umma kwamba unapigana vita dhidi ya rushwa, ni kuwang’oa madarakani watuhumiwa, hata bila ushahidi wowote.

“Kama watu hawaachi kukwambia ‘fulani anafanya hivi, fulani anafanya vile’, hata kama hakuna ushahidi, lazima uwe tayari kumwita mtuhumiwa na kumwambia: ‘Eeh bwana, kwa jinsi ilivyo ni kwamba wewe sasa ni mzigo. Hufai kwa kufuata vigezo vya utawala bora, kwa hiyo tafadhali jiuzulu,’ hili ni suala la ujasiri…”

Maneno hayo hapo juu yalikuwa maneno mazito yaliyoashiria kuwa mapambano dhidi ya rushwa yalikuwa yanaelekea kukolea hasa.

Kama wasemavyo wahenga, madaraka makubwa si tu kwamba hulevya, bali pia hupofusha mhusika asiweze kuona mambo, na wakati mwingine kujiingiza katika vitendo vya rushwa na vingine vilivyo kinyume cha maadili ya Taifa.

Rais Mkapa aliahidi kutokomeza rushwa kubwa wakati Rais Jakaya Kikwete naye aliahidi kufanya vivyo hivyo, ukiwamo ufisadi uliopindukia. Wote  hawakufanikiwa.

Haya ni masuala ambayo yamekuwa yakiwakera sana Watanzania tangu enzi za Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, ya Pili ya Ali Hassan Mwinyi, ya Tatu ya Mkapa, ya Nne ya Jakaya kikwete na ya Tano ya hivi sasa ya Rais Dk. John Magufuli.

Lakini suala ambalo kwa sasa wamekata tamaa nalo kabisa ni rushwa na ufisadi uliotamalaki nchini. Rais ambaye anataka kukoga nyoyo za Watanzania, ni yule mwenye uwezo wa kulikabili tatizo hili kwa dhati na utashi wa kisiasa, si kwa maneno.

Rais Dk. Magufuli ameanza kazi hiyo, amekwisha kutumbua watu wengi; na haijulikani atafika wapi na kufanikiwa kiasi gani.

Oktoba mwaka jana Rais Kikwete akiwa anasubiri kumkabidhi madaraka Dk. John Magufuli, kila siku kulikuwa na vilio vikubwa na vingi kuhusu rushwa na ufisadi.

Ni vita gani hii ambayo kwa miaka 10 ya Mkapa, yaani tangu mwaka 1995 hadi 2005, na vita ya Kikwete ya tangu 2005 hadi 2015 haikuonyeshi matunda yanayokuna nyoyo za Watanzania, wengi wakiwa walalahoi?

Ni vita gani hiyo ambayo haikuwa na kishindo cha kusababisha kuanguka kwa maadui wa haja, majeruhi au kupatikana kwa mateka mapapa kama ilivyoonekana nchini Kenya, Kenya ya Mwai Kibaki katika miezi 10 Awamu yake ya Kwanza kabla naye kuishiwa pumzi baadaye ghafla?

Ndiyo, Rais Dk. Magufuli yupo madarakani sasa. Ithibati ya utumishi wake itambeba ama kwa njia chanya au hasi machoni mwa Watanzania na jumuia ya kimataifa.

Ndiyo, wameanza kumpima hata kwa ahadi zake alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni. Eti Kagera wanasubiri meli mpya aliyawaahidi baada ya Mv Victoria na Mv Serengeti kuzeeka na kushindwa kufanya kazi.

Pia anasubiriwa kutekeleza ahadi nyingine  kwingineko. Ahadi ni deni, eti?