Home Latest News TAZARA SASA ILETE UHURU WA KIUCHUMI

TAZARA SASA ILETE UHURU WA KIUCHUMI

547
0
SHARE
Rais Dk. John Magufuli akifurahia jambo na mgeni wake Rais wa Zambia Edgar Lungu.

NA BALINAGWE MWAMBUNGU,

SIKU za usoni, Tazara itakuwa na umuhimu wa kipekee kwa Tanzania. Tazara kitakuwa kiungo muhimu kwa uchumi wa Tanzania endapo Serikali itaamua kuinganisha Reli ya Tazara na mipango yake ya Tanzania ya Viwanda kwa kuwa imo katika ukanda wa kilimo unaojulikana kama Tanzania-Zambia Corridor.

Tayari Tazara imefungua fursa kwa wakazi wa Dar es Salaam ambao wameanza kufaidika na treni ya abiria kutoka Stesheni Kuu kwenda Mwakanga. Treni hiyo inasimama katika vituo vya Kwa Fundi Umeme Kwa Limboa, Kigilagila B, Sigara, Kitunda,Kipunguni.

Ukanda wa Tanzania-Zambia una umuhimu wa kipekee kwa sababu sehemu kubwa ambako reli imepita, lilikuwa ni vigumu kufika kutokana na ukosefu wa barabara za uhakika. Sehemu hizo ziliweza kufika tu wakati wa kiangazi. Ukanda huu una umuhimu mkubwa kutokana na ukweli kwamba reli ya Tazara imesaidia kupanua wigo wa kilimo na biashara kwa wananchi—kuanzia Kilombero mkoani Morogoro, Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya na Rukwa. Haya ni maeneo tajiri kwa kilimo cha mazao mbali mbali ya chakula na biashara.

Wakulima wa mpunga wilayani Kilombero, Usangu, Wilaya ya Mbarari mkoani Mbeya na maeno mengine, wamepanua kilimo hicho na mazao mengine. Mazao ya biashara yanayolimwa eneo hili ni pamoja na kahawa, pamba, tumbaku, pareto na  mazao ya chakula kama mahindi, miwa pamoja na mbegu za mafuta na matunda ya kila aina ya matunda.

Kilimo ndio kiwanda mama na Tanzania ya viwanda ambayo viongozi wanaiota—haiwezi kujengwa bila kukipa kilimo umuhimu stahiki. Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.

Ukanda huu una barabara zilizounganishwa zenye urefu wa kilometa zaidi ya 10,300 ambazo zinatumika kwa ajili ya kusafirisha mazao, abiria na bidhaa mbali mbali. Ukanda huu sasa umekuwa maarufu kutokana na biashara ya miti na mbao.

Kuna mapendekezo pia kwamba kwa kuwa usafirishaji kwa njia ya reli ni gharama ndogo ukilinganisha na usafirishaji kwa njia ya barabara, ipo haja ya kuinganisha reli ya Tazara na Reli ya Kati kutoka Tunduma-Sumbawanga na Kigoma. Hii itafungua fursa nyingine ya biashara na nchi jirani za Zambia, Congo (DR), Malawi na hata Zimbabwe kwa kuwa njia ya reli itakuwa ya aina moja.

Tanzania ni mwanachama wa Jumuia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), itawezekana pia Tazara kusafirisha mizigo na abiria kutoka miji ya wanachama. Hii itaipa wigo mpana zaidi reli ya TAZARA kufanya biashara na kupata faida kubwa badala ya kuishia Kapiri Mposhi, Zambia.

Mbali ya kusafirisha aina mbali mbali ya mizigo ikiwemo shaba kutoka Zambia, shaba ndio bidhaa kubwa. Shaba inachangia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni. Mwaka 2014, asilimi 70 ya fedha za kigeni zilitokana na mauzo ya shaba.

Mwaka huu, Zambia imekadiria kusafirisha kiasi cha tani 750,000 za shaba kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Kutokana na matarajio kwamba baada ya Rais wa Zambia, Edgar Lungu, alipoitembelea Tanzania kwa mwaliko wa Rais John Magufuli, aliahidi kwamba nchi yake itaongeza usafirishaji wa mizigo itokayo na ingiayo nchini mwake kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa sababu TAZARA sasa imeunganishwa na reli ya Shirika la Reli la Zambia, upo uwezekano wa kupanua wigo wa biashara kwa kufungua mlango mwingine wa kuleta watalii kutoka kutoka nchi za Kusini mwa Afrika. Kwakuwa Tanzania na Zambia zina hisa sawa kwenye Tazara, Shirika la Reli la Zambia pia linaweza kusafirisha abiria moja kwa moja hadi Dar es Salaam—na kama mashirika haya yakafanya kazi kwa ushindani na ufanisi zaidi, yatachangia kukua kwa uchumi wa nchi mbili hizi na kuwaongezea fursa ya biashara wananchi wa Zambia na Tanzania.

Maadui wa Tazara—wafanyabiashara ya malori, wangependa Tazara ife, ili wachukue nafasi yake ya usafirishaji, lakini kwa msimamo uliopo baina ya nchi hizi mbili—watasubiri sana. Tazara ipo, itakuwapo na itaendelea kuwapo.

Tazara ilibatizwa kuwa ni Reli ya Uhuru, kwa kuwa ilikuwa na mchango mkubwa katika kuinusuru Zambia na harakati za wapigania uhuru Kusini mwa Afrika, ni wakati mwafaka sasa, ichangie ukombozi wa kiuchumi kwa Tanzania na Zambia.

Ujenzi wa Tazara umeleta faida kubwa kwa Tanzania—kiuchumi na kijamii.Watanzania wengin waliajiriwa kama wafanyakazi na vibarua, kabla na baada ya ujenzi kuisha, hivyo kipato chao kilibadilika na wakaishi maisha bora zaidi.

Watanazania ambao ni wafanyakazi wa Tazara wanalipa kodi. Serkali inatoza inapata kodi kutokana na shughuli mbali mbali za kibiashara.

Vituo vingi (stesheni) vilivyojengwa na Tazara sasa hivi ni miji midogo midogo kama vile, Mlimba na Makambako na imefungua biashara za kila aina na fursa nyingine za kiuchumi kama vile kilimo, viwanda vidogo vidogo. Huduma za kijamii pia zinapatikana kama vile shule, zahanati, maji na ujenzi wa barabara.