Home Makala TCRA-CC NA MASAIBU YA WATUMIAJI SIMU

TCRA-CC NA MASAIBU YA WATUMIAJI SIMU

1122
0
SHARE

NA ESTHER MNYIKA


BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CC), ni taasisi ya umma iliyoundwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Namba 12 ya mwaka 2003 kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano.

Kutetea na kulinda maslahi ya watumiaji kwa kuwasilisha maoni na taarifa pamoja na kushauriana na Mamlaka, na Waziri mwenye dhamana ya mawasiliano, kupokea na kusambaza taarifa kuhusu maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano.

Kuanzisha kamati za watumiaji wa huduma za mawasiliano za mikoa, pamoja na kushauriana nazo na watoa huduma, Serikali na vikundi vingine vya watumiaji juu ya masuala yanayohusu watumiaji.

Mtumiaji ana haki ya kupata huduma za mawasiliano, haki ya kuchagua huduma, haki ya kupata huduma na bidhaa zenye ubora, haki ya kupata elimu, haki ya kusikilizwa, haki ya kulalamika, haki ya kupata taarifa na haki ya kupata usiri/faragha.

Akizungumza na Rai Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Mary Msuya anasema  lengo la kuanzisha   ni kuwa na chombo imara  na cha kutegemewa katika kutetea haki na maslahi ya watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano pamoja na kuleta maelewanomiongoni mwa wadau wa sekta ya mawasiliano.

Anasema dhamira ni Kujenga mtandao imara wa kuhamasisha na kuelimisha watumiaji juu ya haki na wajibu wao, ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya mashauriano na wadau mbali mbali wa sekta ya mawasiliano.

Anasema  mtumiaji  anaweza kulalamika kuhusu kutopatikana kwa huduma, huduma  zisizokidhi viwango, kukatiwa huduma bila sababu za msingi, matangazo ya biashara yenye udanganyifu, bidhaa isiyokidhi kiwango na ukiukwaji wa usiri au faragha.

Anasema  mtumiaji wa huduma za  mawasiliano anaweza kuwasilisha malalamiko kwa muuzaji wa bidhaa, mtoa huduma zinazohusiana na bei, ubora na upatikanaji.

“Mtumiaji ana wajibu wa kulipia gharama za huduma anazotumia, kutafuta taarifa, kutunza mazingira, kulalamika, kulinda miundo mbinu ya mawasiliano pamoja na kuhakikisha kuwa anatumia huduma na bidhaa za mawasiliano kwa usahihi kulindana na kanuni na sheria zilizopo,”anasema Msuya.

Msuya anasema  zipo kazi nyingi ikiwa ni  pamoja na kupokea  na kusambaza taarifa na maoni  kuhusu masuala ya msingi ya watumiaji wa huduma hizo na kuanzisha kamati za watumiaji katika ngazi ya mkoa, wilaya na sekta na kushauriana nazo. Anasema mtumiaji asipopata haki zake ana haki ya kulalamika kwa kufuata utaratibu uliowekwa kisheria.

Anasema utaratibu huo unamtaka mtumiaji kuwasilisha malalamiko yake kwa mtoa huduma, endapo tatizo halijapata utatuzi mtumiaji atawasilisha malalamiko yake kwa maandishi kwa Mamlaka ya Mawasiliano yaani TCRA.

Msuya anasema mtumiaji wa huduma za mawasiliano ana haki ya kuhudumiwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, mtumiaji ana haki ya kupata huduma hizi kwa bei halali.

Anasema mtumiaji ana haki ya kupata huduma salama kutoka kwa watoa huduma, haki ya kulindwa dhidi ya bidhaa au huduma ambazo ni hatari kwa afya au maisha.

Anasema  mtoa huduma anapaswa kujiridhisha kila wakati kuwa huduma anayopeleka kwa mtumiaji ni salama na haihatarishi usalama wa mtumiaji.

“Haki ya kupata taarifa sahihi na zinazotosheleza kuhusu huduma ili kumwezesha kufanya maamuzi sahihi na endelevu, mtumiaji pia ana haki ya kupata taarifa juu ya sekta zinazosimamia mawasiliano nchini, juu ya sera, sheria na miongozo mbali mbali zinazoathiri huduma zinazotolewa kwa mtumiaji,”anasema.

Anasema haki ya kuchagua huduma kwa kuzingatia bei, ubora, mahitaji na uwezo wa kifedha wa mtumiaji, haki hiyo pia inategemea upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu huduma inayotolewa na watoa huduma.

Anasena mtumiaji ana haki ya kuwasilishwa kwenye vyombo vya kutunga sheria, kusimamia sera ama kwa mdhibiti wa huduma za mawasiliano,kuwasilishwa huku kunaenda sambamba na kupatiwa taarifa za masuala yaliyojiri yenye manufaa kwa mtumiaji.

Msuya anasema haki ya utatuzi mzuri wa madai, kufidiwa kutokana na kupatiwa bidhaa zenye dosari au huduma mbovu.

Anasema hivyo  mteja anapaswa kukataa huduma zisizoridhisha na kurudishiwa fedha zake taslimu au kupatiwa bidhaa nyingine na mtoa huduma.

Msuya anasema wao kama baraza wanapomtetea  mtu akijua haki zake  anajitambua, hivyo watu wengi ambao wanaleta malalamiko na kwamba wengi wanaowafikia ni wale wasiotambua haki zao.

Anasema Sekta ya mawasiliano  ina badilika kila siku  na huduma  za simu  nyingi zinaongezeka. Kutokana na hali hiyo anatoa rai kwa watoa huduma  ili wawaelimishe vizuri watumiaji  wajue haki zao.

“Mtumiaji ana haki ya kupata elimu na ujuzi unaohitajika kwa  kukufanya maamuzi ya msingi kwa kujiamini wakati wa kununua au kuchagua bidhaa au huduma, haki ya kufahamishwa viwango, kanuni na taratibu za kitaifa na kimataifa zinazohusu mahitaji yake,”anaseama.

Anasema watoa huduma wana wajibu wa kuhakikisha na kudumisha usiri wa maudhui ya mawasiliano au data ambayo mtoa huduma anaweza kupata kutokana na kumhudumia mtumiaji.

Pia, taarifa za maudhui au data hazitatolewa kwa mtu yeyoye bila ridhaa ya mtumiaji au agizo la mamlaka, vyombo vya dola kulingana na sheria na mtumiaji anashauriwa pia kutumia  nakala kwa baraza  hilo.

Anasema katika kuelimisha  watumiaji, huwa wanatumia njia ya semina, redio, luninga, Shule za msingi na sekondari, instragram, njia ya ujumbe mfupi ‘message’ na kushirikiana na taasisi kama EWURA-CCC, SUMATRA –CCC  kwa sababu mtumiaji ni mmoja.

Msuya anasema nchi ni kubwa  huwa wanafanya hivyo kwa njia hizo kuelimisha watumiaji ili kuwafikia walengwa pamoja kuwepo na kamati  hizo.

Anaeleza kuwa watanzania bado hawajawa na mwamko wa kujitetea  wala kuanzisha  vikundi vya watumiaji wa mawasiliano kama vya wajasiliamali. Tena viwangio vya sheria mpya ya mtandao havijafikiwa ncini hali inayoongeza changamoto.

Anasema watumie mitandao hiyo kwa kutafuta fursa mbalimbali,  kwa wanafunzi kutafuta  maarifa ya elimu na kuelimsha jamii sio kwa vitu ambavyo ni kinyume cha sheria.

Msuya anasema wanakabiliwa na changamoto nyingi  pamoja na teknolojia  inakwenda haraka  na bado watumiaji wa Tanzania  hawana uelewa wa kutosha.

Anasema teknolojia  inabadilka   kila siku katika huduma za simu. Wametoka analogia na sasa wapo digitali kutokana na hali hiyo bado hawajafikia malengo.

Anasema nchi ni kubwa na wana ofisi Dar es Salaam tu lakini wanawafikia walengwa kwa muda mwafaka kupitia kamati zilizoundwa.

Msuya anasema  kwa wastani  kwa mwezi, wanapokea   malalamiko  20 hadi 25 na malalamiko  mengi watumiaji hawana taarifa. Aidha, anawashauri watumiaji wanapopeleka  malalamiko kwenye baraza  kutafuta  na taarifa za kutosha na watumie fursa hiyo kuleta kero zao.