Home Makala TEKNOLOJIA IMELETA MAGEUZI SEKTA YA AFYA

TEKNOLOJIA IMELETA MAGEUZI SEKTA YA AFYA

662
0
SHARE

NA VERONICA ROMWALD


KWA lugha rahisi, teknolojia ni utumiaji, utengenezaji na vifaa vya maarifa, mashine, mbinu, mifumo au njia zitumikazo kutatua tatizo kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa jambo fulani.

Kadiri miaka inavyosonga mbele tunashuhudia kukua kwa kasi kwa maendeleo ya teknolojia katika nyanja mbalimbali.

Sekta ya afya ni miongoni mwa nyanja nyingi ambazo leo hii tunashuhudia mabadiliko makubwa, kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia.

Mabadiliko hayo yamesababisha kufanyika kwa maboresho ya aina yake katika sekta hii hasa hapa nchini na kuifanya Tanzania sasa kuwa kama nchi nyingine zilizoendelea.

Wengi sasa wananufaika na kukua kwa teknolojia na tunaona hata huduma ambazo awali tulikuwa tukizifuata katika nchi nyingine leo hii zinafanyika hapa hapa nchini kwa ufanisi mkubwa.

Huduma kama za upasuaji wa moyo, matatizo ya mifupa, ubongo na mengine yanafanywa nchini na wataalamu wetu wazalendo kwa kushirikiana na wenzao wa mataifa mbalimbali na hivyo kusaidia kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumika kutibu watu waliokuwa wakizifuata nje ya nchi huduma kama hizo.

Awali, kabla ya kukua kwa kasi, maendeleo ya kiteknolojia, njia pekee waliyokuwa wakitumia madaktari kufanya upasuaji ni ile ya kufungua kifua au tumbo.

Upasuaji huo kitaalamu unaitwa open surgery, umefanyika kwa muda mrefu nchini na kuokoa maisha ya wengi. Ili kumtibu mtu tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu kwa mfano madaktari walilazimika kufungua kifua cha mgonjwa na kisha kuuzibua mshipa ulioziba.

Aidha, ili kumtibu mgonjwa tatizo lililopo ndani ya tumbo walilazimika kufungua tumbo na kisha kumtibu mgonjwa husika.

Pamoja na kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi, upasuaji wa njia hii unaonekana kuwa na changamoto nyingi.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaituni Bokhary, anasema ili kumfanyia mgonjwa upasuaji kwa njia hiyo huhitajika kuwapo kwa damu ya kutosha ya akiba.

“Kwa sababu tunafungua sehemu fulani ya mwili, tunahitaji damu ya ziada maana wakati mwingine mgonjwa hupoteza damu nyingi hivyo lazima tumwongezee ili kuokoa maisha yake,” anasema.

Anasema changamoto nyingine ni kwamba, mgonjwa anayefanyiwa upasuaji kwa kutumia njia hiyo hulazimika kukaa wodini muda mrefu madaktari wakichunguza maendeleo ya afya yake kabla ya kumruhusu kurejea nyumbani.

“Changamoto zipo nyingi ikiwamo kusababisha mzigo kwa ndugu na hospitali kwa sababu mgonjwa anapokaa wodini muda mrefu maana yake ni kwamba ndugu wanalazimika kuja kila mara kumwangalia na madaktari lazima tumfuatilie kwa karibu kila wakati hadi tuhakikishe afya yake inatengemaa,” anasema.

Anasema kukuwa kwa teknolojia kumesaidia kubuniwa njia nzuri zaidi ya kumsaidia mgonjwa anayehitaji kufanyiwa upasuaji kumtibu viungo vyake vya ndani.

“Awali ilikuwa lazima tutumie ‘open surgery’ lakini sasa kuna njia hii nyingine ya ‘laparoscopic’ ambayo kwa kweli tunaona ni nzuri zaidi kuliko ile ya awali,” anasema.

Anafafanua “Laparoscopic ni upasuaji unaofanywa kwa kutumia njia ya matundu madogo ambapo madaktari hutumia vifaa maalumu kutibu tatizo linalomsumbua mgonjwa husika.

“Kuna tofauti kubwa mno katika kufanya upasuaji kwa njia ya ‘open surgery’ na ‘laparoscopic’, katika ‘open surgery’ tunafungua sehemu ya mwili mfano tumboni ili kutibu tatizo, lakini kwa kutumia njia ya ‘laparoscopic’ tunatumia vifaa mbalimbali ambavyo tunavituma katika sehemu ya tatizo na kutibu,” anasema.

Anasema ili kufanikisha upasuaji kwa kutumia njia ya matundu madogo ni lazima pawepo na gesi ya kutosha ya oxygen kabla ya kuanza kumtoboa mgonjwa ili kumtibu.

“Huwezi kufanya upasuaji kwa njia hii kama huna gesi ya kutosha ya oxygen, huwa tunaitumia kunyanyua tumbo la mgonjwa, huwezi kutoboa matundu ikiwa tumbo la mgonjwa halijanyanyuka kidogo,” anasema.

Dk. Bokhary anasema baada ya kumwekea mgonjwa gesi hiyo, hutumia vifaa maalumu kutoboa matundu katika mwili wa mgonjwa na kutazama kupitia kifaa maalumu ‘monitor’ jinsi ambavyo vifaa walivyoviingiza ndani vinavyopenya hadi kufika katika eneo lenye tatizo.

“Tunaona kila tunachokifanya kupitia monitor inayokuwa mbele yetu,” anasema.

Anasema njia ya upasuaji wa laparoscopic ni nzuri zaidi ikilinganishwa na ile ya open surgery kwani kuna faida lukuki ambazo wamekuwa wakiziona.

“Kwanza tunapofanya upasuaji kwa njia ya matundu, tumekuwa tukitumia kiasi kidogo mno cha damu kumwongezea mgonjwa, kwa sababu hatufungui sehemu kubwa ya mwili bali tunatoboa matundu kidogo hivyo mgonjwa huwa hapotezi damu nyingi kama inavyokuwa tukitumia njia ya open surgery,” anasema na kuongeza:

“Mgonjwa anayefanyiwa upasuaji kwa njia ya matundu hukaa muda mfupi hospitalini na kuruhusiwa hata ndani ya saa 24 tukijiridhisha kwamba anaendelea vizuri lakini anayefanyiwa upasuaji mkubwa wa kufungua sehemu ya mwili hukaa muda mrefu.

Anasema mgonjwa anayetibiwa kwa njia ya laparoscopic hupata maumivu kidogo kulinganisha na yule aliyefanyiwa upasuaji kwa njia ya open surgery.

“Maumivu yanakuwa madogo kwa sababu kidonda chake huwa hata hakihitaji kushonwa wakati yule aliyefanyiwa upasuaji kwa njia ya open surgery ni lazima kidonda chake tukishone na hivyo hupata maumivu makali baada ya upasuaji,” anasema.

Anasema Februari 20 hadi 23, Muhimbili waliwafanyia upasuaji kwa njia ya laparoscopic watoto sita waliokuwa wakisumbuliwa na matatizo mbalimbali.

Anasema walifanya upasuaji huo kwa kushirikiana na madaktari wenzao wa Hospitali ya King Faisal ya nchini Saudi Arabia.

“Tulifanya upasuaji huo kwa mafanikio makubwa, kuna wawili ambao tuliwafanyia upasuaji huu na kushusha kokwa zao za uzazi ambazo zilibaki ndani tumboni, hadi kwenye vifuko vyao vya korodani,” anasema na kuongeza:

“Mtoto mmoja mwishoni mwa mwaka jana tulilazimika kumfanyia upasuaji kuzisogeza karibu na korodani kwa sababu zilikuwa mbali sana, ni hatari kokwa za korodani kubaki ndani kwa baadaye mtoto husika hushindwa kutungisha mimba.

Daktari huyo anasema walifanikiwa pia kuwafanyia upasuaji watoto wengine waliokuwa na matatizo mbalimbali, mmoja alikuwa hana njia ya haja kubwa, awali tulimfanyia upasuaji na kumtengeneza njia ya muda katika ubavu wake mmoja.

“Kwa hiyo huyu tumemfanyia na sasa ataweza kutoa haja kubwa kwa njia ya kawaida kama wanadamu wengine walivyo, mtoto mwingine tumepanua njia yake ya chakula, awali ilikuwa imebana hali ambayo ilikuwa inamfanya ashindwe kula vizuri chakula.

“Mtoto mwingine tumemfanyia upasuaji wa kurudisha utumbo wake ndani ambao ulikuwa unatoka nje kila alipokuwa akijisaidia,” anasema.

Daktari huyo anasema upasuaji huo ni mkubwa kufanyika katika hospitali hiyo na kwamba wanatarajia utaanza kuleta mageuzi makubwa kwani unaonekana kuwa na manufaa makubwa kwa wagonjwa hasa kupona haraka na kuruhusiwa kurejea nyumbani mapema.