Home Latest News TETEMEKO LA ARDHI LIMEWAACHA GIZANI KAGERA

TETEMEKO LA ARDHI LIMEWAACHA GIZANI KAGERA

873
0
SHARE

Na Renatha Kipaka, Bukoba 

WAKATI wakazi wa mkoa wa Kagera wakiendelea na maisha yao ya kila siki ikiwa ni pamoja na kulisahau janga la tetemeko la ardhi bado kuna watu wapo gizani kwa maana ya kuikosa nishati ya umeme.

Hali hiyo ilisababishwa na tetemeko lililotokea Septemba 10 mwaka jana majira ya saa tisa alasiri na kuwaacha wakazi wa mkoa huo hasa katika manispaa ya Bukoba, Missenyi, Bukoba vijijini katika hali ya taharuki na majonzi.

Licha ya wakazi wa mkoa huo kupoteza watu 17 kwa mujibu wa Serikali pamoja na makazi yao lakini pia wapo waliopoteaza miundombinu ya umeme baada ya nyumba kudondoka na zingingine kupata nyufa ambazo zilikosa hadhi ya kuwa na umeme kuanzia wakati huo.

Baadhi ya wananchi wameeleza jinsi walivyopoteza umeme na kubakia wakilala gizani. Judi Jeremia ni na Vectra Mwemezi mkazi wa Hamugembe Omukishenye, Rehema Athumani mkazi wa Omkigusha.

Judi Jeremiah ambaye ni mkazi wa Kibeta anasema; “Kwa upande wangu nimepata wakati mgumu katika kipindi ambacho sikuwa na umeme nyumbani kwangu kwani nililazimika kutumia vitu mbadala kama vile kibatari, tochi na wakati mwingine chemli ili kusaidia familia yangu kuendelea kupata mwanga japo ulionekana kuwa hafifu ila wapo wengi ambao mpaka sasa hawajarejeshewa umeme” anasema Jeremiah

Vectra Mwemezi mkazi wa Hamugembe anaeleza kuwa wakati wa tetemeko nyumba yake ilianguka upande mmoja ambao ndio mita ya umeme ilikuwa imewekwa na kusababisha mita hiyo kuharibika moja kwa moja.

Rehema Athumani mkazi wa Omkigusha nae anasema; “baada ya tetemeko la ardhi kupita kwa upande wake ilikuwa ni shida kwani sikuwa na sehemu ya kuishi tena hivyo hata umeme kwa wakati huo ilikuwa ni hadithi kwangu mimi na familia yangu.

“Lakini katika tetemeko hilo hakuna nilichokibakisha siku hiyo Zaidi ya kubakia mimi na watoto wangu wawili pamoja na mume wangu na hiyo mita, kiasi kwamba sasa ndio nimeaza upya kurejesha makazi yangu japo mpaka naishi kwa wazazi wangu kwa muda wote huo”anasema Athumani

Kaimu Meneja wa Tanesco mkoani Kagera, David Mhando, anasema wakati tetemeko la ardhi lilipotokea hatua ya kwanza walioichukua ni kuzima umeme kutokana na taharuki iliyokuwepo kwa wakati huo.

Anasema baada ya kukaa kwa muda umeme ulianza kurudishwa kidogo kidogo kwa baadhi ya maeneo ambayo hayakuathirika zaidi kwa tahadhari.

Katika kufuatilia uharibifu uliosababishwa tetemeko hilo Mafundi mitambo walianza kuondoa nyaya ambazo zilizokuwa katika mfumo mkubwa wa umeme kuelekea katika mfumo mdogo unaopeleka umeme kwenye makazi ya watu.

“Niseme tu kwa upande wetu Tanesco miundombinu yetu mikubwa ya mfumo wa umeme haikuathirika, labda eneo lililoathirika zaidi ni kwenye laini ndogo za kusambaza umeme kwa watumiaji tu ambazo mpaka sasa miundombini hiyo imesharekebishwa na kurudi katika hali yake” anasema Mhando

Meneja huyo anasema Mkoa wa Kagera una watumiaji wa nishati ya umeme 65,000 .

Mhando anasema changamoto zinazowakabili  ni uelewa mdogo wawa wananchi juu ya matumizi ya sahihi ya umeme pamoja na kulinda miundombinu yake.

Aidha, anasema wateja waliokatiwa umeme kutokana na athari ya tetemeko ni wateja 852 na mita zilizotolewa kwenye majumba 428 mpaka sasa na kwa upande wa wateja ambao wamerudishiwa mita zao ni 213.

Anamalizia kwa kusema mpaka sasa wananchi walioupoteza umeme wakati wa tetemeko wanaendelea kurejeshewa umeme siku hadi siku.