Home kitaifa TFF ije na ‘gia’ mpya SWPL

TFF ije na ‘gia’ mpya SWPL

21188
0
SHARE

NA ZAINAB IDDY 

YAPO mengi ya kukera katika uendeshaji wa soka la Tanzania, kubwa ikiwa ni waamuzi wabovu, ukiacha ubora mdogo wa viwanja na mkanganyiko wa ratiba kwa Ligi Kuu (TPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Kwa bahati mbaya, hayo yamekuwa yakisemwa kabla na baada ya kila msimu lakini hakuna mabadiliko ya kutia moyo. Inachosha.

Unaweza kusema viongozi wenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya wa mchezo wa mpira wa miguu wameshindwa kujifunza kutokana na ripoti ya tathmini ya mwishoni mwa kila msimu.

Hata hivyo, nijitose moja kwa moja katika kile kilichonisukuma kuandika makala haya, nikimaanisha Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (SWPL).

Nikumbushe tu kuwa uwepo wa ligi hiyo ni matokeo ya kelele za muda mrefu za wadau wa kandanda, waliotaka kuliona soka la wanawake linapewa nafasi kama ilivyo katika mataifa mengine, nikitolea mfano Nigeria na Afrika Kusini.

Ikiwa inatarajia kufikia tamati Mei 19, mwaka huu, tayari JKT Queens imefanikiwa kulitetea taji lake baada ya kuvuna pointi 57, ambazo haziwezi na timu zilizopo.

Hii ni mara ya pili kwa JKT kutwaa ubingwa tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo msimu wa 2016/17, ambao ni Mlandizi ndiyo iliyoibuka kidedea.

Lakini wakati ni msimu wa tatu unaelekea ukingoni, bado kuna mambo mengi yanayorudisha nyuma maendeleo ya soka la wanawake kama si kupoteza mvuto kabisa.

Nalisema hilo nikiamini kuwa endapo ligi ya wanawake itakuwa bora, basi hata matatizo ya Twiga Stars kushindwa kufurukuta kimataifa kitabaki kuwa historia.

Kwanza, ni suala la ukata, ambapo kwa msimu huu licha ya kuwa chini ya udhamini wa bia ya Serengeti Lite, bado hali ya kiuchumi imekuwa tatizo, kiasi cha baadhi yake timu kushindwa kufika katika vituo husika kwa wakati.

Cha kushangaza, hata kile kidogo kinachotolewa na Serengeti Lite kinacheleweshwa kuwafikia walengwa, jambo linalosababisha timu shiriki kuwa na maandalizi ya bora liende.

Katika hili ni vizuri TFF kwa kushirikiana na Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA) kuibuka na mikakati ya kuihakikishia udhamini ligi hiyo kwa msimu ujao.

Pili, bado miundombinu ni tatizo kubwa, ingawa hilo lilipigiwa kelele hata kabla ya ligi kuanza.

Mfano ulio hai ni Uwanja wa Karume uliopo mbele ya Ofisi za Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambao hauna hadhi ya kutumiwa hivi sasa kwa kuwa ubora wake umepungua kama si kuondoka kabisa.

Kwa Dar es Salaam, uwanja mkubwa ambao umekuwa ukitumika kwa michezo mingi ya ligi ya wanawake ni Karume, hivyo kitendo cha kuruhusu kufikia hatua ya kapeti lake kuchoka ni aibu kwa TFF.

Hakika ni jambo la aibu ikiwa hata viongozi wa taasisi hiyo wameshindwa kulipatia ufumbuzi suala la uwanja huo unaotazama na ofisi zao.

Mwisho, tofauti na ilivyokuwa kwa TPL, ratiba haikuwa ‘pasua kichwa’ kwa msimu huu wa ligi ya wanawake. TFF ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoipa nafasi kero hiyo.

Walau inatia moyo kuona hadi kufikia hatua hii, hakuna timu iliyolalamika kuhusu suala la ratiba, ni jambo la kupongeza na pasi na shaka litakuwa endelevu.