Home Habari TGNP: Vyama vijiulize kwanini wanawake hawajiungi navyo

TGNP: Vyama vijiulize kwanini wanawake hawajiungi navyo

1324
0
SHARE

LEONARD MANG’OHA

MKURUGENZI Mtendaji wa Matandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Liliani Liundi, ni miongoni mwa wanaharakati maarufu katika utetezi wa masuala ya jinsia amekuwa katika nafasi hiyo tangu mwaka 2014 baada ya kuitumikia idara mbalimbali katika taasisi hiyo.

Lilian alianza kuitumikia TGNP kama Ofisa Programu katika masuala ya teknolojia ya habari akiratibu chumba cha mawasiliano, mtandao ulikuwa ukisaidia wanawake na watu wengine wa pembezoni kuhakikisha wanapata huduma za mtandao kwa urahisi katika kipindi hicho ambacho matumizi ya intaneti yalikuwa bado madogo.

Baadaye alishika wadhifa wa Mkuu wa Idara ya Uibuaji na Usambazaji Taarifa TGNP pamoja na Masuala ya Uchambuzi. Mwaka 2006 alisoma masuala ya uratibu wa habari za kimataifa nchini Uholanzi kisha akarejea na kuendelea na nafasi yake ya ukuu wa idara hadi mwaka 2014.

Kabla ya kujiunga na TGNP alifanya kazi katika Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kama Database Administrater and Information Management. Pia amewahi kufanya kazi katika kampuni ya IPP Media (ITV na Redio One) katika masuala ya masoko, maktaba na mawasiliano.

RAI: Kuna ugumu gani wa kufanya kazi hizi za utetezi wa haki za watu hasa katika eneo hili la jinsia?

Lilian: Ukiwa ni mtu ambaye unapenda kuona dunia ambayo watu wote wanaifurahia hutaiona kazi hii ni ngumu. Kwa hiyo mimi hii kazi sioni kama ni ngumu hasa ninapowaona wanawake, wanaume na vijana ambao wako pembezoni tunaweza tukafanya kitu ambacho kinabadilisha maisha yao, mimi ndiyo furaha yangu na ndiyo ninaona nimefanya kitu.

Tumeweza kufikia wanawake wengi ambao wasingeweza kufikiwa kwa urahisi. Kwa kutumia njia mbalimbali wamefahamu haki zao, wameweza kutetea haki zao au kutetewa lakini pia tumeweza kuwafanya wananchi wengi waweze kujitambua wajibu wao kama wananchi na kusimama katika nafasi zao katika kuchangia maendeleo ya nchi hii.

Lakini vilevile kuwajibishana wao wenyewe pale walipo kwa kufahamu na kutekeleza majukumu yao, lakini pia wawajibishe wale ambao wamewapa mamlaka pale ambapo wanaona hawatekelezi majukumu yao kwa kufuata taratibu ambazo zimewekwa katika nchi hii.

Tulianzisha mkakati kwa ajili ya kuwafikia wananchi kwa wingi na kuwafanya wao wenyewe waweze kushika hatamu katika maendeleo yao, tukawa tumeanzisha uragbishi ngazi ya jamii ambapo tunafanya utafiti shirikishi ambao unafanya watu waweze kujitambua na waweze kuibua masuala katika maeneo yao, waweze kufanya uchambuzi kwa jicho la kijinsia lakini pia waweze kutoka na mikakati kwamba wao kama wananchi wanawezaje kutatua changamoto zao.

Lakini pia wadau mbalimbali ikiwamo Serikali wana nafasi gani katika kutatua changamoto zao na hapo hapo suala la uwajibikaji likiwa ni msingi kwamba wao wanawajibika vipi, lakini ambao hawawajibiki wananchi wasikae kimya waweze kupaza sauti kwa kutumia sheria zilizopo kuhakikisha kwamba viongozi wanawajibika.

Tunaamini kwamba wananchi wakifanya kazi sambamba na viongozi na kila mmoja akisimama kwenye nafasi yake maendeleo yetu yatakwenda kwa kasi zaidi.

RAI: Mnafanya utetezi wa masuala ya jinsia ni kwa kiasi gani mmesaidia jamii iliyo pembezoni kutambua haki zake za kisiasa na hata kuzitafuta.

Lilian: Ukizungumzia masuala ya siasa na uongozi ni mambo ambayo ni mtambuka kwa TGNP, sisi katika mikakati yetu yote suala la wanawake kushiriki katika uamuzi ni mojawapo ya kipaumbele. Kwamba tunaamini nchi yetu hii ya Tanzania au hata nchi nyingine wananchi wake wote wakishiriki katika kutoa maamuzi inaleta tija zaidi.

Nchi zetu za Afrika, wanawake ni zaidi ya asilimia 50 kwa hiyo hawawezi kuwekwa pembeni kwenye kufanya maamuzi katika nyanja mbalimbali ziwe za kiuchumi, kisiasa hata ziwe za kijamii. Ndiyo maana unapokuja wanawake kushiriki kwenye masuala ya nafasi za uongozi na maamuzi katika siasa kwetu ni kipaumbele.

TGNP tangu ilivyoanzishwa miaka ya 1993 imekuwa ikishiriki sana katika kujengea uwezo wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na makundi mengine. Mwaka 1995 wakati huo taasisi ilikuwa bado ni changa kabisa lakini bado ilishiriki katika mambo mengi ya kujenga uwezo wanawake ambao walikuwa wametia nia na wale ambao walikuwa wamegombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Sisi tunaamini kwenye kuongozwa na ajenda na kuwa na sauti ya pamoja kwamba wanawake wa Tanzania katika masuala ya siasa ni nini vipaumbele vyetu, tunataka nini hao viongozi wakiingia madarakani wafanye.

Tunataka nini Serikali ikiingia madarakani ifanye. Sasa kupitia hapo sisi huwa tunatengeneza ajenda ya wanawake ambayo tunaiita ilani ya uchaguzi ya wanawake ambayo inakuwa ni shirikishi kwamba makundi mbalimbali ya wanawake na wanaume walioko pembezoni, lakini pia vijana tunakuja pamoja na kufanya kuangalia muktadha na kuchambua ni masuala gani ambayo tunaona ni changamoto tunataka yafanyiwe kazi ili kutengeneza Tanzania ambayo tunaitaka.

Kwa hiyo katika huo mchakato tunapata hivyo vipaumbele ambavyo tunaviita madai katika ilani ya wanawake ya uchaguzi ambapo mwaka 2000 tulitengeneza ilani ya kwanza, mwaka 2005 tukatengeneza ilani ya pili, mwaka  2010, 2015 mpaka sasa hivi 2020 tunetengeneza ilani nyingine ambayo ina hivyo vipaumbele vyote vya wanawake kuonesha tunataka vyama vya siasa vifanye nini, Serikali ambayo itaingia madarakani ifanye nini, tunataka wagombea wafanye nini watakapopata mamlaka.

Lakini mamlaka za Serikali kama Takukuru, Tume ya Taifa ya Uchaguzi tunataka ifanye nini, lakini hata sisi wanaharakati tunatakiwa tufanye nini, vyombo vya habari vifanye nini ili kuhakikisha kwamba vipaumbele vya wanawake vinafanyiwa kazi.

Na tunapozungumza masuala ya vipaumbele vya wanawake ni masuala ya kijamii kwa sababu unapozungumzia suala la afya ni la kijamii, unapozungumzia suala la elimu ni la kila mtu kwa hiyo tunajua unapozungumzia vipaumbele vya wanawake ni kwamba tunaikomboa jamii yote na wala si wanawake tu.

Kwa hiyo safari hii pia tumetengeneza hiyo ajenda yetu ambayo inaweka sauti yetu pamoja na makundi mbalimbali ya wakulima, wafugaji, vyama vya wafanyakazi, asasi za kiraia, vyuo vikuu wote tulikuja pamoja tukafanya huo mchakato na tukatoka na hivyo vipaumbele vya ilani yetu ambayo tumeshaisambaza kwenye vyama vya siasa.

Wanajamii na taasisi mbalimbali ili waone hayo madai ya wanawake na waweze kuyaingiza kwenye ilani zao kwa sababu sisi tunasema wanawake tuko wengi na tuna nguvu ya idadi kwa hiyo angalia madai yetu, yafanyie kazi madai yetu tutakupa kura yetu.

RAI: Kutokana na jitihada zote hizo mnazozifanya mwitikio wa wanawake kujitokeza kuwania nafsi za uongozi ukoje?

Lilian: Tumepiga hatua si kwamba tumesimama, ukilinganisha na huko nyuma sasa hivi wanawake wana mwitikio lakini kikubwa zaidi ambacho tunatia msisitizo ni kwamba huwezi ukawapeleka watu kwenye uwanja wa mbio ukawaambia kimbieni huyu mwingine kabeba mizigo mgongoni, mwingine wala hana vifaa vya kukimbilia.

Uwanja hauko sawa kwa hiyo wale ambao wana vitu vingi wamebeba nyuma yao watashindwa hizo mbio na ndiyo maana kila wakati tunasema sera na sheria ambazo zinatoa nafasi sawa kwa wanawake, wanaume, vijana na watu wenye ulemavu zikoje.

Tunalilia kila wakati hizo sera na sheria zitekelezwe na pale penye upungufu zirekebishwe ili tutengeneze uwanja ulio sawa ili watu wote waweze kwenda sawa, kwa sababu tukiangalia kihistoria wanawake waliachwa nyuma si kwa mapenzi yao ni kwa sababu ya mila na desturi pamoja na mfumo dume tunafanyaje kurekebisha hayo mapungufu ili na wao waweze kuingia kwenye uchaguzi kwa njia sahihi na isiyo na matatizo.

Hata viti maalumu ni katika kurekebisha hayo mapengo lakini hatujawekeza vya kutosha huko kwenye majimbo kuhakikisha kwamba uwanja uko sawa.

Hebu fikiria kwa kiwango ambacho watu wanavyopiga kampeni, kiwango cha fedha watu wanavyotumia, mitandao watu wanavyofanya, hata vyombo vya habari kutoa nafasi kwa wanawake ni kidogo.

Hata ule mtizamo wa jamii kusema huyu ni mke wangu, huyu ni dada yangu, huyu ni mama yangu nimwachilie aende akagombee bado kuna kigugumizi wengi wamepoteza ndoa zao, wengi wamepoteza mahusiano kwa sababu tu anataka kugombea nafasi ya uongozi fulani.

Kwa hiyo bado tunatakiwa turekebishe kuna rushwa ya ngono, mwanamke ukitaka kusimama kugombea bado kuna makando kando kama hayo ya rushwa za ngono ambayo mwanamke anaona kujiingiza huko mimi siko tayari, kwa hiyo unakuwa inawatoa huko na kuwaweka pembeni.

Safari hii katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tumeweza kuhamasisha wanawake wengi kutokana na mikakati yetu tunayofanya kila wakati na wengi wamejitokeza.

Kuna maeneo wanakueleza kabisa kwamba kabla hamjaja hapa wanawake waliokuwa wametia nia walikuwa 10 tu baada ya kuja wametia nia zaidi ya 70 katika kata moja tu, lakini wametia nia hao watapita, vyama vitaweza kuruhusu?

Kwa sababu vyama ndiyo lango la kuingilia kwenye nafasi za kisiasa sasa kama hili lango litakuwa linafunguliwa kwa baadhi ya watu na kufungwa kwa baadhi ya watu inakuwa ngumu kidogo.

Vyama vinatakiwa vione nia thabiti na ya dhati kwamba vinataka kusapoti wanawake kwa sababu unapozungumza kitu kioneshe kwa vitendo, ukiangalia hata kwenye miundo ya vyama unakuta nafasi nyingi za uongozi zimeshikiliwa na wanaume.

Sasa unaponiambia mimi nasapoti ajenda ya wanawake wakati huoneshi hata kwenye muundo wa chama chako hiyo inaonesha ni nia ya maneno lakini si ya dhati.

Vyama ni taasisi za umma kwa hiyo sisi tuna wajibu wa kudai na sheria hii mpya ya vyama vya siasa imeweka msingi wa usawa wa kijinsia. Sasa kama usawa wa kijinsia ni msingi mmoja wapo kwenye sharia ya vyama vya siasa basi walazimishwe waoneshe jinsi gani watatekeleza huo msingi.

RAI: Mmetoa elimu kiasi gani ili kuhakikisha watu wengi walio pembezoni wanafahamu na kutambua umuhumi wa wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi?

Lilian: Kwanza kuna changamoto, masuala ya elimu ya uraia uchaguzi ukuwamo ndani yake ni kitu kinachotakiwa kiwe cha kudumu na ni kitu kinachopaswa kipewe kipaumbele kuwe hata na vipindi kwenye vyombo mbalimbali vya habari, ikiwezekana vyombo vya habari viweze kupewa maelekezo kwamba hivi ni lazima vitolewe ikiwezekana kila wiki mara moja ili wananchi kwa ujumla wake wapate hiyo elimu.

Wanawake ambao tumewafikia bado uelewa ni mdogo, kwa mfano kanuni zimetolewa hawazijui na hawana. Kwa hiyo kuna vitu wanakosa haki zao kwa sababu tu hawana taarifa. Baada ya hizi kanuni zilizotolewa ni kwa kiwango gani imehakikishwa watu wana uelea japokuwa muda ulikuwa ni kidogo.

Kwa hiyo zitolewe mapema lakini pia kuhakikisha elimu inatolewa mpaka ngazi ya kitongoji wanakuwa na uelewa wapiga kura pamoja na wale wanaogombea kwa sababu taasisi zetu pamoja na kwamba zinajitahidi lakini haziwezi kufika kila mahali.

Tunatarajia Serikali ina nguvu, inaweza hata ikatoa maelekezo kwenye redio za kijamii, redio za kitaifa, TV za kitaifa, magazeti wakatoa hiyo elimu na wakawapa maelekezo kuwa hii ni lazima, wakatoa hiyo elimu na ikawafikia watu. Kwa kweli watu tunaowapitia wasiwasi ni mkubwa kwa sababu uelewa ni mdogo.

RAI: Mnatumia mfumo gani kufuatilia uhamasishaji mnaoufanya kuhakikisha unaleta matokeo chanya katika jamii?

Lilian: Ilani yetu ni nyenzo pia ya ufuatiliaji kwa sababu tunaofanya nao kazi wanaielewa na wakishaielewa wale ambao watapewa hiyo dhamana au Serikali itakayoingia madarakani ile ndiyo kipimo na safari hii tulivyoweka ni kwamba baada ya miaka miwili kutakuwa na hiyo mid term review, tutakuwa tunafanya tathmini tunapitia je ilani iliyoingia madarakani imetekeleza hii ilani kwa kiwango gani, lakini pia kuangalia kama wameingiza kwenye manifestal zao kwa sababu kama hawajaingiza kunakuwa na changamoto ya utekelezaji.

Tutakuwa tunafuatilia kwa karibu na kwa jinsi ilani ile tulivyoitengeneza mpaka kwenye ngazi ya kata wanaangalia vipaumbele na changamoto zao na wanawaambia wagombea wao bayana kwamba hizi ndiyo changamoto zetu tunatarajia tuweze kusaidiana kuzitatua kwa hiyo tunaomba mtuahidi tutakapowapa dhamana mtazitekelezaje.

Vilevile katika maeneo ambayo tumefanya tathimini kutoka kwa wadau mbalimbali kuwa ni wanawake gani wanaona wanaweza wakagombea baada ya kufanya hiyo tathimini tukawa na database ambayo inaonesha wanawake ambao ni potential kugombea au kutia nia.

Kwa hiyo walivyoanza kutia nia tunawaangalia wale ambao watu walisema huyu tunafikiri angekuwa mzuri je waliotia nia ni wangapi, halafu baada ya kutia nia katika maeneo tuliyopita tunaangalia waliotia nia ni wangapi katika hayo makundi.

Wakati wa kupitishwa na vyama tutaona ni chama gani ambacho kiliwapitisha wale waliotia nia na kiliwapitisha wangapi.

Katika kuchaguliwa tunaangalia katika yale makundi ya kipaumbele ni nani ambao walishinda, hiyo itatuonesha kama chama kina nia ya dhati.

Hatulazimishi chama kwamba lazima kipitishe wanawake kwa sababu wanaangalia uwezo na wataweka na vigezo ambavyo pia havitamtoa mwanamke nje ila vitaweza kuwapa wanawake kipaumbele wale ambao wana uwezo. Na chama kiweke mikakati ya kuwajengea uwezo kisiseme tu hawana uwezo alafu hakuna mikakati yoyote.

RAI: Ni sababu gani zinawafanya hata wanawake wenye uwezo kutojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi?

Lilian: Wengi wanasema wanatamani kungekuwa na mgombea huru kwamba wasibanwe na chama chochote lakini hali halisi ni kwamba lazima uwe mwanachama wa chama fulani ndiyo uweze kugombea.

Na kitu ambacho kinatokea ni kwamba katika baadhi ya maeneo wanawake walihamasika na kukawa na mwenzao walimpenda sana wakawa wanataka agombee lakini ilivyofika wakati wampigie kura ndani ya chama wanawake wakawa hawana kadi za chama chochote.

Kwa hiyo tunaendelea kujifunza na kuwahimiza wanawake wawe wanachama wa chama fulani kwa sababu mfumo uko hivyo na ili kuweza kumweka mwanamke kwenye nafasi ni lazima awe kwenye chama fulani.

Vyama vya siasa vijiulize kwanini watu hawataki kuingia kwenye vyama, kuna haja vyama vifanye kazi ya ziada kuhakiksha vinawaandaa wanawake vya kutosha kwa sababu wanawake hawana kadi na hawana chama.

Kwa hiyo hilo pia kwenye klabu zetu za jinsia huko mashuleni tutaendelea kuwafundisha tangu wakiwa wadogo kwamba ni muhimu mtu uwe na chama fulani yaani utakapofikisha miaka 18 ndipo utakapo pata haki vizuri haki yako ya kumchagua mtu kwenye chama fulani ua hata wewe mwenyewe kuchaguliwa vinginevyo tunakuwa tunapoteza hiyo haki yetu kwa sababu tu hatuna kadi.

RAI: Ni nini kinasababisha wanawake kutopenda kujiunga na vyama vya siasa?

Lilian: Ukiona hivyo ni kwamba mtu anaona hakuna umuhimu, mwingine tuliongea naye anasema sisi wakati wetu wakati unakwenda A’ level tayari lazima uingie kwenye vijana wa Tanu. Kwa hiyo watu walikuwa wanafurahia kuwa wanachama wa chama hicho.

Sasa hiyo imepotelea wapi na kwa sababu gani imepotea vyama vijiulize kwamba havivutii mbona watu hawajiungi hasa wanawake.

RAI: Kumekuwa na malalamiko ya kukosekana kwa uwanja huru wa kisiasa miongoni mwa vyama vya siasa nchini hili linaathiri vipi wanawake kujitokea kugombea nafasi za uongozi?

LILIAN: Wanawake wanapenda amani, wanapenda mazingira yaliyo sawa, kwa hiyo wanapoona kuna figisufigisu za kisiasa hawataonekana.

Hata tukiangalia hizi chaguzi ndogo ambazo zimefanyika ni wanawake wachache wamejitokeza kupiga kura kwa sababu hali haikuwa salama kwao, kwa hiyo wanawake wanashindwa kujitokeza kwa ajili ya kugombea. Wanakuwa na uwezo lakini hawawezi kujitokeza kwa sababu mazingira sio salama.

Suala la usalama wakati wa uchaguzi kwa wagombea na wapiga kura ni la msingi sana kwa sababu mwanamke atakapopanda jukwaani akaanza kutukanwa hayuko tayari kudhalilishwa, lakini pia hata wale wanaomzunguka, kumbuka huyu ni mwanamke na mfumo dume bado ni mkubwa.

Kwa hiyo hata mume wake anasema mimi siko tayari kuona mke wangu anadhalilishwa, ndugu, kaka, baba wenyewe watakwambia hatuko tayari uende kule ukadhalilishe.

Wito ninaoutoa katika hili ni kwamba ni muhimu kuheshimu Katiba lakini ni muhimu zaidi kuweka mazingira ambayo yako salama kwa watu wote kushiriki. Lakini kama mazingira hayako salama kusema kweli ushiriki wa wanawake utaendelea kuwa mdogo na itakuwa sio sahihi kwa sababu tunawanyima wanawake haki yao ya msingi ya kushiriki.

RAI: Kwa kuvitazama vyama vyenyewe vinao huo utashi wa kutoa nafasi kwa mwanamke kushikiri na kushika nafasi mbalimbali za uongozi?

Lilian: Tumefanya tathimini ya kuangalia muundo lakini pia sera kuu za vyama, vyama vyote ukisoma utakuta kuna vitu ambavyo wameweka vyenye nia ya kuleta usawa wa kijinsia japo sio vya kutosha lakini kwa kiwango fulani.

Lakini ukija kwenye utekelezaji hapo ndipo kuna tatizo kwa sababu hata vyama vyenyewe kufanya ile tathimini ya kile ambacho wamekiweka kwenye ile sera iwe kwenye muundo wao kwamba tutafanya hiki, ukiuliza ripoti ambayo inaonesha uchambuzi wa hicho kitu ambacho wanakisema kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia hakipo.