Home Habari Tibaijuka afichua Bunge analotamani

Tibaijuka afichua Bunge analotamani

1188
0
SHARE

*Aeleza mfumo bado kuruhusu Rais mwanamke

ANDREW MSECHU

MBUNGE wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka, ameendelea kusisitiza dhamira yake ya kutogombea tena ubunge mwakani, huku akitoa ya moyoni kuhusu mabadiliko makubwa ambayo yanahitaji kufanywa, ili suala la wabunge kupeleka hoja binafsi bungeni liwe na tija.

Akizungumza na Rai wiki hii, Profesa Tibaijuka ambaye pia amewahi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), alisema katika muda wake aliokaa bungeni, amebaini utaratibu wa upelekaji hoja binafsi za wabunge una vikwazo.

 “Kwa kweli katika muda niliokaa bungeni, katika miaka yangu yote nimebaini kuwa ili kuwapa wabunge uhuru katika kuwakilisha hoja binafsi, utaratibu wake unahitaji kuboreshwa ili kuondoa ukiritimba na kuwapa wabunge uhuru zaidi katika eneo hilo.

 “Katika hili, ni muhimu kulisimamia ili kuhakikisha kuwa sheria zinazotungwa ziwe zinawasilishwa kutoka pande zote, siyo kutoka upande wa Serikali tu,” alisema.

Pia alisema anaona utamaduni wa kutoa hukumu bila kuwasililiza watu ni tatizo bungeni, suala ambalo linatakiwa pia litazamwe upya na kuwekwa katika utaratibu mzuri wa kuwasikiliza wanaotuhumiwa kabla ya kutoa hukumu.

Profesa Tibaijuka alisema bungeni kulizuka utamaduni wa watu kuteka nyara hoja na wakati mwingine kutoa hukumu bila kuzifanyia tafiti, ambao lazima ufanyiwe kazi ili urekebishwe na kuruhusu haki itendeke.

Alisema Bunge ndicho chombo kinachotunga sheria ambazo kwa pamoja zinatoa mwanya wa kusikilizwa kwa pande zote kabla ya kutoa hukumu, lakini pia ndilo lenye mamlaka ya mahakama ya mwisho kubadilisha Katiba, hivyo si vyema kuzuia nafasi ya kusikilizwa kwa walalamikiwa kabla ya kutoa hukumu.

 “Lakini kwa upande mwingine ningependa kuona Bunge liwe linaangalia masuala muhimu kwa undani bila kuangalia itikadi. Japokuwa mwisho wa siku Serikali lazima iendelee kuwepo madarakani, lakini hiyo haimaanishi kuwa kusiwe na maboresho,” alisema.

Mwanasiasa huyo ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema anachikiona bungeni ni kwamba utendaji unachangia sana kuminya uhuru wa watu kupeleka hoja binafsi bungeni, ili kutoa fursa ya maboresho ya sheria zinazotoka kwa wawakilishi wa wananchi, kuliko kuangalia tu sheria zinazowasilishwa kwa mapendekezo ya Serikali.

Kuhusu suala la kubadilisha katiba katika kipengele za ukomo wa muda wa rais kukaa madarakani, alisema mambo hayo yanayozungumzwa mitaani hawezi kuyazungumzia, na atakuwa tayari kuzungumzia pale tu yatakapofika bungeni au katika vikao vya chama.

Akizungumza iwapo ana ndoto ya kuwania urais, Profesa Tibaujuka alisema suala muhimu analoliona kwa sasa ni kwamba nyakati haziruhusu, hivyo amechagua kupumzika ubunge na kuendelea na shughuli zake.

Hata hivyo, alisema hatua ya kupumzika kwa sasa haimwondoi katika wigo wa siasa na anaona italinda zaidi heshima yake, akiwa tayari kutoa ushauri na kushiriki kwa kutumia uzoefu wake kusaidia watu.

Alisema katika hilo, mfano mzuri ni mamlaka aliyojijengea Baba wa Taifa, Mwalimu Julisu Nyerere, ambaye aliamua kung’atuka na kuachia madaraka, lakini hadi leo mamlaka yake iko wazi, kutokana na mchango wake kwa taifa.

Profesa Tibaijuka alisema aliporejea nchini baada ya kutimiza majukumu yake Umoja wa Mataifa (UN), aliamua kuwatumikia Watanzania kwa kuwania ubunge kwa kuwa aliona ndio saizi yake kwa wakati huo.

 “Mimi sikugombea urais kwa sababu nilikuja kugombea ubunge nikijua kuwa kwa nyakati zile, nafasi ya mwanamke kuwa rais bado kwa kuwa tuko kwenye mapambano bado.

“Kwa hiyo sikuja kupoteza muda, ningeweza kuchukua fomu, lakini sikuchukua, nilikuwa ninajua kuwa wakati bado haujafika.

 “Mimi pia ni mwanaharakati wa kike, lakini sikuchukua fomu kwa sababu nilikuwa najua wakati haujafika, ni lazima ujipime, ndiyo maana niliamua kuwa nigombee ubunge wa Jimbo la Muleba Kusini.

“Ukienda kwenye hizi za kugombea urais unaweza kushindwa na ukishindwa si rahisi kuja kwenye ubunge, sasa hapo ndiyo linakuja suala la mtaka yote kwa pupa hukosa yote, mimi nilikuwa naenda kugombea ubunge,” alisema.

Alisisitiza kuwa anajiamini na anaona anatosha kwenye urais, lakini kwa sasa bado anaona ni suala la wakati kwa kuwa mfumo bado unawalinda wanaume zaidi.

 “Issue siyo kwamba sitoshi, si kweli, ila ni suala la wakati, bado haujafika, halafu unaangalia jamii, sikuona hao wanaume wa kuniweka, dunia inabadilika, lakini hadi sasa nyakati zinaonyesha bado wanaopata urais ni wanaume au kuna kundi la wanaume limewaunga mkono.

 “Ninaona hata kwenye ubunge wa jimbo bado wanaume wana nguvu sana katika kuhakikisha mtu anapita. Uzoefu unanionyesha kutokana na hata wapigakura wangu walivyo, kwamba kuna vijiwe vya wanaume, hasa vijana ambao ndio wana maamuzi, wakishasema hapa ni fulani lazima iwe,” alisema.

Alisema suala ni kwamba ukishanuia kwenye ubunge wa jimbo halafu ukaenda kwenye kuwania urais, ni lazima unashindwa kabisa.

“Ndiyo maana niliamua kabisa kuwania ubunge na kule Muleba Kusini, nilihakikisha pia kuwa natafuta kura za kutosha za Rais Dk. John Magufuli, ambaye pia ni jirani yangu katika Jimbo la Chato,” alisema.

Katika kipindi cha pili cha Rais Jakaya Kikwete, Profesa Tibaijuka aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na alijiuzulu wadhifa huo kabla ya muda wake kwisha.