Home Makala TID: NCHI YOTE IMEJAA MATEJA

TID: NCHI YOTE IMEJAA MATEJA

1117
0
SHARE
Msanii wa muziki wa Bonge fleva, TID akizungumzia namna matumizi ya dawa za kulevya yalivyoathiri maendeleo ya muziki wake

NA FARAJA MASINDE


MATUMIZI ya dawa za kulevya yameonekana bado ni changamoto kubwa inayowakabili vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa katika kusukuma gurudumu la maendeleo.

Kwa nyakati tofauti tumeshuhudia kwa namna ambavyo harakati mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika kuhakikisha kuwa changamoto hiyo inafikia ukomo.

Hata hivyo, tatizo hilo limeonekana kuwa kubwa kutokana na wingi wa vijana wanaofanikiwa kuondolewa kwenye kadhia hiyo kujikuta wakirejea tena kwa nguvu, licha ya kusema kuwa hata wao wamekuwa hawapendi kurejea kwenye hali hiyo isipokuwa wamekuwa hawawezi kuruka kihunzi hicho kulingana na mazoea na hata mazingira yanayowazunguka.

Itakumbukwa Februari 3, mwaka huu kuwa Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, iliamsha tena harakati za kupiga vita matumizi hayo ya dawa za kulevya kwa kuwagusa wale wote ambao wamekuwa wakijihusisha na utumiaji pamoja na wale wanaodhaniwa kuwa wanajihusisha na biashara hiyo haramu.

Katika mapambano hayo ambayo pia yamepata baraka za mkuu wa nchi, Rais Dk. Jonh Magufuli, kila mtu amekuwa na shauku ya kutaka kujua hatima ya nani na nani watabainika kuwa ndio vinara wa biashara hiyo, baada ya kuwapo kwa orodha mbalimbali za majina ambazo hata hivyo wengi wamekuwa wakidai kutokuhusika isipokuwa kundi la vijana hasa wasanii wa muziki ambao ndio wamekuwa wakionekana wazi kutumia dawa hizo zinazopigwa marufuku duniani.

Baadhi ya vijana ambao wamejikuta wakidumbukia kwenye dimbwi hilo mara baada ya kupitia kwenye mikono ya dola, wamekuwa wakionyesha nia ya kubadilika na kutamani kuwa watu safi kama anavyobainisha msanii, Khalid Mohamed ‘T.I.D’.

Anasema vijana wanahitaji kuwa na msaada kwa jamii kwa kuwa na matokeo chanya ikilinganishwa kuwa yeye ni msanii, amekuwa kioo cha jamii kwa muda mrefu na mambo mengi aliyoyafanya yamekuwa yakifanywa na vijana hao wanaompenda, hivyo kwa sasa amedhamiria kujiweka pembeni na dawa hizo na kujaribu kuwa mtu atakayekuwa msaada mkubwa kwa jamii.

“Kuna watu ambao wananiona mimi ni kioo, hivyo kwa vitu vingi nilivyofanya watu wengi wamefanya, utashangaa nilijaribu kutumia dawa za kulevya kwa siku moja tu lakini leo ni miaka minne na kama ningefahamu madhara ya dawa hizi, wala nisingethubutu kufanya hivi.

“Kwa sasa nimejitolea kuwa balozi kwa vijana wenzangu kuhakikisha kuwa wanaondokana na tatizo hili, wala sijalipwa na mtu yeyote, najua kuwa tatizo hili limeathiri vijana wengi kwa kiwango kikubwa sana nchini na najua kundi kubwa la vijana wameathirika, hivyo najua kwa kutumia ushawishi wangu wengi wataamka na kuondokana na dawa za kulevya.

“Tunahitaji kutoa msaada wa elimu kwa waathirika, wengi wamekuwa wakipelekwa kwenye nyumba za kusaidia waathirika na kisha baada ya muda mfupi wanarejea tena kwenye changamoto hii, jambo hili linatokana kwamba wengi wanarudi kuishi maisha yale yale,” anasema T.I.D.

Anasema iwapo asingeangukia kwenye utumiaji wa dawa hizo, basi angekuwa mbali kwenye taaluma yake hiyo ya muziki ikiwamo kupata mafanikio.

“Kiukweli maisha yangu yangekuwa mbali sana kwani nimetumia pesa nyingi, muda pia katika kupata dawa hizi, hivyo nimeshindwa kufanya muziki wangu uwe bora na kukubalika kimataifa, najua kwa kipindi hicho nilivyovuruga maisha yangu, ningekuwa mbali zaidi kwa maendeleo yangu binafsi na ya muziki kwa ujumla,” anasema T.I.D.

Msanii huyo anasema kuwa kupitia ushawishi wake alionao kwa vijana na jamii kwa ujumla, anaamini kuwa changamoto hiyo itapungua.

“Naamini kwa sasa nitakuwa mtu mwingine na hata kazi zangu zitajikita zaidi katika kutoa darasa kwa vijana ambao bado wanaamini katika kutumia dawa za kulevya ili waweze kufanya shughuli za kila siku.

“Hivyo naamini kuwa maisha bila dawa, muziki bila dawa vinawezekana, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa tunakuwa na jamii mpya kwani kwa sasa wasanii wengi tumejikuta kwenye janga hili, jambo ambalo linakuwa ni gumu kwa wazazi kuruhusu vijana wao kufanya sanaa kulingana na haya yanayoendelea,” anasema.

Msanii huyo ni mmoja tu kati ya kundi kubwa la wasanii ambao wamekuwa wakitajwa kujihusisha na dawa hizo ambapo wengine ni, Rashid Makwilo maarufu kama Chid Benzi, Rehema Chalamaila (Ray C) na wengine wengi.

Soba

Ni wazi kuwa mwanga umeanza kuonekana katika kuondoa kundi kubwa la vijana kwenye janga hilo la utumiaji dawa za kulevya, ambapo kwa sasa soba nyingi zinaelezwa kuwa na idadi kubwa ya waathirika hususan vijana.

Baadhi ya soba hizo ni pamoja na The ties that bind us Recovery (Kisiwani Sobar), Pedderef Sobar House (Vijibweni au kwa Nuru), South Beach Sobar House (Maeneo ya Soweto Kigamboni), Pili Misana foundation (Magogoni), Geti Jeusi Sobar (Amina Mbonde) zilizoko jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Ties that bind us Recovery Center (Kisiwani Sobar House), Dismas Munishi, anasema kabla ya kuanza kupamba moto kwa harakati za kukomesha dawa za kulevya, walikuwa wanapokea mtu mmoja hadi wawili kwa mwezi lakini kwa kipindi hiki, kwa siku wanapokea watu tisa hadi 10.

“Ni wazi kuwa sasa kumekuwa na changamoto kubwa  kwani hali ni mbaya, ndipo tumegundua kuwa nchi yetu imejaa mateja wengi kuliko kawaida, kwani hatukuzoea kupata waathirika wengi kiasi hiki kwa siku.

“Kila siku idadi inaongezeka na wote wamekuwa wakihitaji kusaidiwa ili waweze kuondokana na hali hii kutokana na kukosa unga, jambo linalowapelekea kupata maumivu makali,” anasema Munishi.