Home Michezo Kimataifa TIMU HIZI TIMU HIZI ZIMEKALIA KUTI KAVU LIGI YA MABINGWA ULAYA

TIMU HIZI TIMU HIZI ZIMEKALIA KUTI KAVU LIGI YA MABINGWA ULAYA

647
0
SHARE

MWANDISHI WETU NA MITANDAO

LIGI ya Mabingwa Ulaya imeanza kukolea kasi na hadi kufikia sasa tayari maji yameanza kujitenga na mafuta ambapo timu zilizofuzu hatua ya 16 bora zishajulikana, na zile zitakazotoka mapema zishajionesha dhahiri.

Kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka Ulaya, katika makundi nane timu mbili za juu zitafuzu kuingia hatua hiyo na zile zitakazoshika nafasi ya tatu zitatupwa Ligi ya Europa.

Lakini je, ni timu zipi zilizo kwenye hatari ya kutoingia kwenye hatua ya mtoano msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya?

Ya kwanza ni Atletico Madrid ambayo ipo Kundi C lenye timu za Qarabag FK ya Azerbaijan, Chelsea na AS Roma.

Baada ya droo ya makundi iliyofanyika mapema Agosti mwaka huu, timu zilizopigiwa upatu kuvuka hatua ya hiyo ya makundi ni Atletico, Roma na Chelsea lakini wakali hao wa La Liga, Atletico, ndiyo walio kwenye hatari ya kutokwenda 16 bora, hasa baada ya sare yao dhidi ya Qarabag.

Mbaya zaidi, michezo miwili iliyobaki inayoweza kufufua matumaini ni dhidi ya Roma na Chelsea.

Atletico wana mabao mawili pekee katika michezo yao miwili waliyocheza, wanashika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo linaloongozwa na Roma ambao hawajapoteza hata mchezo mmoja, huku Chelsea wakiwa nafasi ya pili.

Timu nyingine ambayo huenda wadau wengi wa soka waliovutiwa na soka lao msimu huu wakasikitishhwa sana kusikia imetoka mapema ni Napoli.

Katika Kundi F, Napoli wako na Feyenoord, Shakhtar Donetsk na Man City walioko kileleni.

Licha ya kiwango kizuri walichonacho Ligi Kuu Italia, Napoli yenye pointi tatu pekee, imeshindwa kutamba kwenye kundi lao ikiziacha Man City (12) na Shakhtar (9).

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Napoli hawaitolei jicho michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa kuwa wanaona kuna uhakika wa kubeba taji la Serie A.

Mpango alionao kocha wao, Maurizio Sarri ni kuhakikisha wanaikaba koo Juve na kutwaa taji la Serie A ambalo kwa mara ya mwisho waliinyakua katika msimu wa 1989-90.

Wakali wa Bundesliga, Borussia Dortmund ambao walipangwa Kundi H, wakiwa na Tottenham, Real Madrid na Apoel Nicosia, nao hali yao ni tete na wana hatari ya kutupwa Ligi ya Europa.

Ni Spurs pekee ambayo haijapoteza mchezo, hivyo imefuzu moja kwa moja kwenda 16 bora na ili Dortmund ifuzu, italazimika kuichapa Madrid inayoshika nafasi ya pili, lakini pia iombe Apoel nao waifunge timu hiyo ya La Liga kitu ambacho ni ngumu kuamini kama kitatokea.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Ufaransa, AS Monaco ambao msimu uliopita walifika nusu fainali, hali yao ni mbaya msimu huu sababu kuu ikitajwa kuwa ni kuondokewa na mastaa wao watatu wa kikosi cha kwanza; Kylian Mbappe, Tiemoue Bakayoko na Bernardo Silva.

Katika mechi sita za ugenini zilizopita kwenye michuano hiyo, Monaco imeshinda mara moja pekee.

Mshambuliaji wao, Ramadel Falcao, hajawa kwenye ubora wake Ligi ya Mabingwa msimu huu, akiwa amefunga bao moja pekee hadi sasa, licha ya kuwa na 13 kwenye ligi.

Monaco wanaburuza mkia Kundi G, wakiwa hawajashinda hata mchezo mmoja kati ya minne, wakitoa sare mbili.

Ili kufuzu, Monaco wanatakiwa wazifunge RB Leipzig na Besiktas, ambazo zina nafasi kubwa ya kufuzu.

Kundi D nalo lina timu iliyopo hatarini kukosa nafasi ya kucheza hatua ya 16 bora ambayo ni Sporting Lisbon.

Tangu mwanzo, kundi hilo lilikuwa linatabirika kwa kuwa lina Barcelona na Juventus, ambazo ndizo zilizokuwa zikipewa nafasi ya kwenda 16 bora.

Uzembe wa Lisbon ya Ureno ulikuwa ni kupata ushindi mwembamba wa mabao 3-2 dhidi ya Olympiacos licha ya kwamba walikuwa wanaongoza kwa mabao 3-0 katika kipindi cha kwanza.

Katika mchezo wa pili, waliweza kuibana mbavu Barca lakini wakajikuta wakipoteza matokeo kwa bao la kujifunga la Sebastian Coates.

Ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Juve na Barca, Lisbon sasa watahitaji ushindi katika michezo yao miwili iliyobaki ukiwamo mmoja dhidi ya Barca.

Michuano hiyo itaendelea kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi huu kwa timu zote kuingia mzunguko wa tano wa hatua hiyo ya makundi.