Home Latest News TOC MPYA SULUHISHO LA MEDALI OLIMPIKI 2020?

TOC MPYA SULUHISHO LA MEDALI OLIMPIKI 2020?

1291
0
SHARE

NA ASHA MUHAJI,

HAKUNA kitu kibaya katika maisha kama kukata tamaa. Mara nyingi hatua hiyo huonesha wazi kabisa kwamba hakuna tena matumaini ya ufumbuzi wa tatizo.

Kama ni kilio katika sekta ya michezo basi kimeliliwa mno tena sana. Kila nyanja ya mchezo hali imekuwa ni mbaya, watu wamepiga kelele na sasa wamekata tamaa, si katika soka, si riadha, si ngumi, netiboli wala kikapu.

Kuna maneno hupendwa kutamkwa sana na wajuji wa michezo kwamba Tanzania imejaa vipaji lukuki lakini ajabu licha ya vipaji hivyo hakuna mafanikio yoyote na badala yake watu wamekuwa wakijivunia historia tu ambayo nayo kadri miaka inavyokwenda thamani yake inaanza kupungua.

Mwanamichezo gani hapa nchini asiyejua kama Tanzania ilivuna medali katika Olimpiki moja tu iliyofanyika Moscow Urusi mwaka 1980, ambapo Suleiman Nyambui alitwaa medali ya fedha katika mbio za mita 500 huku Filbert Bayi akiibuka na medali ya fedha katika mbio za mita 3000.

Hiyo ni mara ya kwanza na mwisho kwa Tanzania kunyakua medali katika mashindano makubwa duniani ya Olimpiki japokuwa ilijaribu kufikia hatua kama hizo katika michuano mingine.

Kupitia michuano mingine mikubwa ya Jumuiya ya Madola Tanzania iliyofanyika mwaka 1978 huko Edimonton, Canada, Gidamis Shahanga alitwaa medali ya dhahabu baada ya kuibuka mshindi katika riadha alipokimbia mbio za marathon huku pia Bayi akitwaa medali ya fedha katika mbio za mita 1500.

Katika michuano kama hiyo iliyofanyika mwaka 1982 huko…..Shahanga tena alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za mita 10000 na Zakaria Barie akibeba medali ya fedha katika mbio hizo hizo wakati Juma Ikangaa akiibuka na medali ya fedha katika mbio za marathon huku bondia Willy Isangura akiondoka na medali ya fedha katika ngumi uzito wa juu.

Historia inaweza kuwa tamu zaidi ukiendelea kuisoma na kubaini kuwa katika michuano hiyo hiyo iliyofanyika mwaka 2006 huko Melbourne Australia, mwanariadha Samson Ramadhani aliibuka mshindi katika mbio za marathon huku Fabian Joseph akitwaa medali ya fedha katika mbio za mita 10000.

Historia inaendelea kuwa tamu tukikumbuka kuwa Christopher Isegwe aliibuka mshindi wa pili katika mashindano ya Dunia ya Riadha yaliyofanyika Helsink Finland mwaka 2005 na kunyakua medali ya fedha.

Lakini toka toka mwaka 2006 baada ya Samson kurejea nchini na medali ya dhahabu hadi leo ikiwa ni miaka 10 sasa Tanzania haijaambulia medali yoyote katika mashindano hayo makubwa iwe ni Olimpiki, Madola au mashindano ya riadha ya dunia licha ya kujaa vipaji vya kila aina.

Wachambuzi wa masuala ya michezo wanaiangalia hali hiyo kama ikisababishwa zaidi na Kamati ya Olimpiki Tanzania ambayo ndiyo yenye jukumu la kusimamia vyama kuhakikisha vinatoa wanamichezo wengi wenye vigezo kushiriki michuano hiyo lakini hata hivyo mara zote imekuwa ikitoa wanamichezo wachache sana.

Kumekuwepo na kutupiana mpira kuhusiana na udhaifu mkubwa kuanzia maandalizi ndani ya vyama hadi yale yanayohusisha timu ya taifa kwa ujumla inapojiandaa na mashindano hayo.

Kuitupia lawama Serikali bila kujitathimini kamati husika ni dhambi kubwa inayopaswa kuwaingiza motoni wahusika wake.

Wakati kukiwa bado na simanzi kuhusiana na ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya Madola pamoja na yale ya  Olimpiki, TOC chombo chenye malaka na usimamizi mkuu wa timu ya nchi kama michuano hiyo, imefanya uchaguzi wake mkuu na kuingiza madarakani safu yake  ya uongozi.

Katika uongozi huo mpya wadadisi wa masuala ya michezo wanadhani hakuna jipya linaloweza kufanywa na uongozi huo kwa madai kuwa viongozi wakuu ni wale wale waliokuwepo kwa muda mrefu ndani ya taasisi hiyo na kushindwa kuleta mabadiliko.

Rais wa taasisi hiyo Ghulam Rashid na katibu mkuu wake Filbert Bayi walikuwepo katika vipindi kadhaa vya uongozi ndani ya TOC na ilishuhudiwa mara kadhaa kuwepo na kashfa mbalimbali kwa wanamichezo wa Tanzania ikiwemo maandalizi ya zima moto, wanamichezo kufafirishwa kwa mafungu, kuazima vifaa pamoja na malalamiko ya posho.

Kuingia madarakani kwa wanamichezo kama Henry Tandau ambaye ana uzoefu mkubwa ndani ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kunaweza kuamsha kasi ya mabadiliko kutokana na ukweli kuwa amekuwa na uzoefu mkubwa katika michezo tofauti.

Tandau ambaye ni Mkufunzi kutoka FIFA pamoja na IOC ni aina ya watu ambao wanaamini mafanikio yanawezekana, na ili uyapate ni lazima uwe na mpango mkakati sambamba na program zinazotekelezeka zikiwa na malengo kuanzia ya muda mfupi na mrefu.

Kuingia pia kwa mwanariadha wa zamani mwenye misimamo, Wilhelm Gidabuday ndani ya TOC kunaweza kusaidia kasi ya mabadiliko na kuleta mtazamo mpya kwa taasisi hiyo kutokana na ukweli kuwa ni mmoja kati ya wanaokerwa sana na kushuka kwa kiwango cha ushindani ndani ya mashindano hayo ya kimataifa.

Mkakati wa kwanza utakaowakabili ni viongozi hao  pamoja na safu nzima ya TOC ni kuhakikisha Tanzania inaanza kushirikisha wanamichezo wengi zaidi huku wakihusisha michezo mingi tofauti kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya ambayo hupeleka wanamichezo wasiopungua 70 katika kila michuano inayoshiriki.

Hilo litafanikiwa iwapo uongozi huo utasimamia wajibu wao ipasavyo sambamba na msukumo utakaowekwa na TOC ikiwemo ‘amsha amsha’ kwa vyama vya michezo.

Lakini pia mtihani wao wa kwanza ni kuhakikisha Tanzania inarudi na medali kadhaa katika michuano ya Madola mwakani pamoja na ile ya Olimpiki ya mwaka 2020 itakayofanyika Tokyo japan.

Licha ya ingizo hilo jipya la wanamichezo kama Tandau na Gidabuday je wanaweza kuleta mabadiliko katika taasisi hiyo na hatimaye mafanikio kurudia enzi za kuvuna medali katika mashindano mbalimbali?