Home Makala Kimataifa TOGO: NUSU KARNE YA MAUMIVU, WANANCHI WASEMA IMETOSHA

TOGO: NUSU KARNE YA MAUMIVU, WANANCHI WASEMA IMETOSHA

1159
0
SHARE

LOME, TOGO

Baada ya miaka mingi ya uvumilivu wananchi wa Togo wameanza kuingia mitaani kudai mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi na kurudisha ukomo wa vipindi vya urais.

Wiki iliyopita (Agosti 19), picha za kutisha za miili ya waandamanaji zilionekana kwenye mitandao ya kijamii ikibebwa kwa machela. Siku hiyo maelfu ya wananchi wa Togo waliingia mitaani wakidai mabadiliko ya demokrasia na kuirudisha katiba ya mwaka 1992.

Kwa miaka 50 iliyopita nchi hiyo ndogo pwani ya Afrika ya Magharibi imekuwa ikitawaliwa na familia moja tu – ya Gnassingbe, na wananchi sasa swanasema nusu karne ni muda mrefu mno.

Yalikuwa ni maandamano ya amani, lakini katika mji wa Sokode, maafisa wa usalama walifyatua risasi za moto kuwatawanya waandamanaji na habari kutoka maafisa wa serikali zilisema watu wawili waliuawa, ingawa kuna madai kwamba wengi zaidi walpoteza maisha.

Picha za ghasia hizi zilivyozidi kusambaa kwenye mitandao ya jamii, ziliibua kumbukumbu za miaka ya mwanzo ya 1990 pale maandamano ya aina hii yalivyokuwa yakipata nguvu kabla ya kuvunjwa kwa nguvu kubwa na utawala wa Jenerali Gnassingbe Eyadema.

Mbabe huyo mkandamizaji alikufa mwaka 2005 lakini kama ilivyo katika nchi nyingine Barani humu, mwanae, Faure Gnassingbe, alirithi kiti chake na kuendeleza aina ya utawala wa baba yake.

Na kwa muda mrefu, hali hii ilisababisha kuibuka kwa kizazi kipya cha Watogo ambacho kilianza kukosa uvumilivu dhidi ya kiongozi huyo hadi kufikia maandamano na ghasia za wiki iliyopita yakidai tena mabadiliko ya kidemokrasia.

Wakati Togo ilipopata uhuru wake mwaka 1960 kulikuwapo kipindi kifupi cha kusherehekea na matumaini makubwa chini ya muasisi wa taifa hilo – Sylvanus Olypmpio. Lakini kilikuwa ni kipindi kifupi sana kwani mwaka 1963 kikundi kimoja cha wanajeshi kikiongozwa na Eyadema kilifanya mapinduzi na kumuua Olympio.

Jeshi  lilitoa mafdaraka kwa serikali ya mpito iliyoongozwa na Nicolas Grunitzky  Mei 1963 Grunitzky alichaguliwa kuwa rais.

Hata hivyo katika hali ya kukosekana utulivu iliyokuwapo, mapinduzi ya pili yalifanyika mwaka 1967, safari hii yalimfanya Eyadema kuwa Rais na kujilimbikizia madaraka makubwa. Na hapo hapo akaanza kuvipiga marufuku vyama vya siasa, kuwakamata viongozi wa vijana na wanasiasa wengine na kuwafanya mamia wengine kuikimbia nchi.

Na katika miaka iliyofuatia, kiongozi huyo wa kijeshi alisuka utawala wa kikandamizaji kwa lengo hasa la kunufaisha jeshi lake, watu wa kabila lake na watu wengine wachache waliounga mkono sera zake.

Hakuwa na itikadi yoyote au sera zaidi ya ile ya kung’ang’ania madarakani na kupora mali za nchi. Na katika medani ile iliyokuwapo ya ‘Vita Baridi’ wakati ambapo nchi nyingi za magharibi zilikuwa zinawavumilia madikteta Barani Afrika kwa vile walikuwa wanaupinga Ukomunisti, utawala wa Eyadema ulizidi kuimarika.

Ilipofika miaka ya 80, minong’ono ya upinzani dhidi ya utawala wake ilianza kukua kwa sauti. Oktoba 1990, msukumo wa kuanguka kwa nchi za Kikomunisti za Ulaya Mashariki uliwafanya wanafunzi wa Togo kuingia mitaani kwa uwingi wakidai demokrasia zaidi.

Maandamano na migomo iliongezeka hadi Eyadema alipokubali kuitisha mkutano wa kitaifa kujadili hali ya baadaye ya nchi hiyo.

Awali ujumbe wa serikali yake ulijiondoa mkutanoni na kujaribu kuyasimamisha mazungumzo. Lakini wajumbe wengine walibakia na kupitisha maazimio hata pale Eyadema alipopeleka vikosi kuzungira eneo hilo la mkutano.

Lakini baadaye alisalimu amri na kukubaliana na maazimio ya mkutano yakiwamo kuundwa serikali ya mpito ya kusimamia uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi, uteuzi wa Waziri Mkuu wa mpito na uundwaji wa Tume ya kuandika Katiba mpya.

Hatimaye, mwaka 1992 Katiba mpya ilikubaliwa na wananchi kupitia kura ya maoni ya asilimia 99.

Hata hivyo miaka iliyofuatia Eyadema na chama chake walifanya kila njia kukwamisha maendeleo ya kidemokrasia. Alitumia mwanya uliojitokeza wa kipindi cha ghasia kilichokuwa na mauaji mengi ya wanasiasa na watu mashuhuri kuurudisha tena udikteta wake.

Mwaka 2002, chama chake cha Rally of the Tologese People (RPT), kiliondoa ukomo wa vipindi vya urais, kufanya uchaguzi wa urais uwe wa raundi moja tu badala ya mbili na kurudisha umri wa mtu kuwania urais kutoka miaka 45 hadi 35.

Badiliko hili la umri lilikuwa na lengo la kumuandaa mwanae Faure Gnassingbe, kushika madaraka kwani wakati ule alikuwa na umri wa miaka 33. Na ndivyo ilivyokuwa.

Miaka 38 baada ya kutwaa madaraka Eyadema alifariki kutokana na ugonjwa wa moyo. Saa chache baadaye jeshi lilitangaza kwamba mwanae ndiyo amekuwa rais mpya.

Baada ya shutuma kali kutoka ndani ya nchi na jumuiya za kimataifa kwamba hatua ile ilikuwa kinyume na katiba, Faure aliachia ngazi. Lakini muda mfupi baadaye alirejea tena madarakani baada ya uchaguzi ambao alishinda kwa asilimia 60.

Uchaguzi huo ulishutumiwa kwamba haukukwa huru na haki na kuwapo kwa wizi mkubwa wa kura. Maandamano yaliyofuatia yalisababisha vifo vya kati ya watu 500 – 800 na maelfu walikimbia nchi.

Baada ya matukio haya aliahidi kufanya mageuzi mengine ya kidemokrasia lakini hadi leo hii hakuna kilichokuja na hivyo wananchi wameanza tena kupambana naye.