Home Makala TPA ilivyorahisisha usafiri wa majini Ziwa Tanganyika

TPA ilivyorahisisha usafiri wa majini Ziwa Tanganyika

1446
0
SHARE
  • Yafanya ukarabati wa bandari, meli zake
  • Yajivunia ukusanyaji wa mapato
  • Kurasimisha bandari bubu

Na ESTHER MBUSSI

USAFIRI wa majini unatajwa kuwa usafiri rahisi na salama katika kusafirisha bidhaa mbalimbali duniani.

Licha ya baadhi ya watu kuogopa usafiri huo kupitia meli na vivuko, lakini umekuwa mkombozi wa wafanyabiashara wengi.

Kusitishwa kwa safari za meli katika baadhi ya bandari kwa sababu mbalimbali nchini imekuwa pigo kwa wafanyabiashara wengi kwani wamekuwa wakiingia gharama katika usafiri wa barabara ambao umekuwa ukitumia muda mwingi njiani.

Katika kuliona hilo, serikali ya awamu ya tano kupitia Mamlaka ya Usimamiz wa Bandari Tanzania (TPA), ikaamua kufufua na kurudisha kwenye chati usafiri wa majini kwa kukarabati na kujenga miundombinu na bandari mpya hususani bandari za maziwa makuu.

Moja ya ukanda unaohamasisha usafiri huo ni Ziwa Tanganyika ambayo makao makuu yake ni Kigoma na kwa upande wa Tanzania ziko katika mikoa mitatu, Kigoma yenyewe, Katavi na Rukwa.

Kigoma ndiyo bandari kuu na kongwe, lakini ziko bandari ndogo za Kibirizi, Kagunga, Kabwesa, Sibwesa na nyinginezo.

Katika Mkoa wa Katavi ndiyo kuna bandari chache zaidi ambazo ni Bandari ya Kalema ambayo iko katika ujenzi wake, Bandari ndogo ya Ikola.

Kwa upande wa Rukwa, kuna Kipili, Kabwe, Kirando, Kasanga, Mwampembe na nyingine ndogo ndogo.

Meneja wa Bandari ya Kigoma ambaye pia ndiyo Msimamizi wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese anasema bandari hiyo katika nafasi yake kijiografia ni muhimu sana katika ustawi wa uchumi wa nchi kwa sababu kwa Tanzania inapakana kupitia mpaka wa maji na nchi zinazotaka kuunganishwa na dunia ya mbali, nchi ambazo hazina bahari na zinatakiwa kuunganishwa na nchi nyingine ambazo ziko Ulaya na Mashariki ya mbali.

Meneja wa Bandari ya Kigoma, Ajuaye Msese.

Anazitaja nchi hizo kuwa ni Rwanda ambayo iko kaskazini mwa ziwa na Burundi, kwa hiyo Bandari ya Kigoma inahudumia nchi hizo na nyingine Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)

“Kigoma ndiyo bandari kubwa katika bandari za Kigoma, kimkakati tunataka kila mkoa tuwe na bandari kubwa moja ukiacha Kigoma ambayo ina zaidi ya miaka 100.

“Kwa upande wa Katavi tunataka kuwa na Bandari ya Kalema, tutaangalia upande wa pili wa Congo katika maeneo ya Moba na Kalemie na maeneo mengine ya mwambao wa Ziwa Tanganyika, lakini kwa Mkoa wa Rukwa kuna Bandari ya Kasanga, kwa sasa hivi si bandari kubwa sana lakini tutawaelezea nini TPA inafanya katika kuifanya Kasanga kuwa bandari kubwa ambayo itakuwa inahudumia Mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani kuweza kuiunganisha na nchi jirani za Zambia na Burundi,” anasema Msese.

Anazungumzia usafiri wa majini kuwa ndiyo njia ya usafirishaji zaidi ukilinganisha na reli au barabara.

Anasema Tanzania kwa sababu Mungu ametujaalia kuwa sehemu nzuri kijiopgrafia tumepata vyote, bahari na maziwa makubwa ya Nyasa, Tanganyika na Victoria.

“Kwa sababu hiyo tunayo nafasi ya kujihudumia sisi wenyewe kama Watanzania lakini tunayo nafasi ya kuwahudumia ambao hawajapata bahati ya kuwahudumia ambao hawana bahari.

Kwa maana hiyo Bandari ya Kigoma imepata umuhimu wa kipekee, kwanza kujihudumia na kuhudumia nchi jirani lakini vile vile kuongeza ufanisi katika bandari zetu za bahari.

“Bandari ya Kigoma ina zaidi ya miaka 100, ni historia ya kipekee sana tangu utawala wa Wajerumani, inaunganishwa na Reli ya Kati (TRC), kwa kuwa na muunganiko huo utaona kuwa sisi kama Watanzania tuna fursa kubwa ya kujihudumia lakini pia kuhudumia wenzetu kwa sababu tunaweza kutoa mzigo sehemu yoyote kutoka Dar es Salaam au Lamu na tukauleta Kigoma na kuupeleka katika nchi jirani.

“Hayo yamekuwa mambo ya kihistoria tumepita utawala wa namna tofauti katika kuendesha hizi bandari kuanzia kipindi cha wakoloni na baadaye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikaja kuvunjika, tukaingia sisi wenyewe kama Tanzania na tukaziendesha kupitia kampuni tofauti kama TRC, Kampuni ya Huduma za Meli ya Serikali (MSCL).

“Mwaka 2006 kupitia Sheria Namba 17 ya mwaka 2004, ya Mamlaka ya Bandari ilipewa jukumu la kusimamia bandari zote Tanzania ukiacha hapo awali ilipokuwa inasimamia bandari za bahari ikatoa majukumu zaidi ya kuisimamia na za kwenye maziwa.

“Kuanzia hapo tumeweza kusogea kutoka wenzetu walipkuwa wamefika katika kuendesha bandari hii ya Kigoma mwaka 2007 kupitia hii sheria,” anasema Msese.

Anasema kwa upande wa Mkoa wa Kigoma hasa Bandari ya Kigoma, imekuwa ikihudumia shehena kwa kiasi kikubwa ambazo asilimia zaidi ya 60 inakwenda Congo, Burundi nza Zambia lakini kutokea Kigoma hawapati shehena sana.

Kutokana na hilo anasema bandari hiyo ina umuhimu wa kipekee kwa sababu utaona shehena katika Bandari ya Dar es Salaam inahitaji ivutwe ili kuongeza mzunguko wa behewa na mzigo kukaa muda mfupi katika mzunguko wa bandari na hivyo kama nchi wanaweza kuchangia pato la taifa kwa ujumla wake.

Idadi ya Meli

Kuhusu idadi ya meli zilizohudumiwa katika Bandari ya Kigoma, kuanzia mwaka 2013/14, Msese anasema ilikuwa na meli 296 zenye ukubwa wa tani 200, mwaka 2014/15 walikuwa na meli 78 zenye uwezo wa kuchukua tani 244,000 lakini mwaka 2015/16 zilikuwa 315 zenye uwezo wa kuchukua tani 201,000, mwaka 2016/17 meli 307 zenye kubeba tani 146,000, na mwaka 2017/18 meli bandari hiyo ilikuwa na meli 434 zenye uwezo wa kuchukua tani 240,000.

“Kwa hiyo utaona kwamba tunaendelea kupata tofauti kwa kwenda juu na si kwenda chini.

“Lakini kwa upande wa mzigo meli zilikuwa na uwezo wa kupakia shehena mbalimbali ambapo mwaka 2013/14 tulihudumia tani 99,346, mwaka 2015/16 tani 137,570, 2016/17 tulishuka kidogo tukahudumia tani 36,573 na mwaka 2017/18 taqni 196,848.

“Kwa mwaka huu 2019, tumelenga kuhudumia tani 205,000 kwa maana hiyo hadi sasa hivi tuko asilimia 90 ya malengo yetu tutakayokamilisha.

“Kwa hiyo katika kipindi cha miaka mitano kunakuwa na ukuaji katika kwanza meli zinazokuja kwa idadi na ukubwa lakini pia kiwango cha mizigo tunayohudumia.

“Unaweza kuona tunapozungumzia shehena ya mizigo imeongezeka tafsiri yake inakuwa na maana kama pia na mizigo imeongezeka maana inaweza ikawepo tu lakini si kitu,” anasema.

Moja ya mashine ya kunyanyua mizigo kwa haraka katika Bandari ya Kigoma.

Mapato

Kuhusu mapato, Msese anasema kumekuwa na ongezeko la mapato kwa muda wote tangu wameanza ambapo mwaka 2013/14 walikusanya Sh bilioni 2.7, na mwaka 2014/15 kidogo walishuka wakakusanya Sh bilioni 2.1, 2015/16 walihudumia Sh bilioni 2.7, mwaka 2016/17 walipanda hadi Sh bilioni 4.14 na mwaka 2017/18 walikusanya Sh bilioni 6.75.

“Kwa hiyo kwa sasa hivi katika mwaka wa fedha 2019/20 tunataka kwenda zaidi ya asilimia 10, suala la ongezeko la meli na shehena tuliyohudumia inasadifu ukusanyaji pia wa mapato.

Tunatarajia pia katika miaka minne ijayo kwenda zaidi ya mara nne kuliko hapa kwa sababau kwenye shehena tunatarajia wenzetu wa Congo watapitisha shehena mbalimbali hususani madini.

“Hivi karibuni tumepata matumaini ya kuhudumia madini ya Lithium yanayotumika kutengenezea betri, na wao wana malengo ya kupitisha karibu tani milioni mbili hapa Kigoma,” anaeleza Msese.

Miradi ya maendeleo

Katika uboreshaji wa miradi mbalimbali katika bandari zake, TPA mkoani Kigoma imejipanga kufanya ukarabati na ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Bandari ya Kigoma

Kuna mradi wa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu yake katika bandari ndogo mbili zilizopo mkoani Kigoma.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa gati katika bandari hizo ambazo ni Bandari ya Kibirizi na Ujiji, na Ofisi ya Mkuu wa Bandari ambapo tayari mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la mradi na ameshaanza kazi karibu miezi mitatu iliyopita.

Msese anasema mradi huo unafanywa na Kampuni ya China Railway 15 Group Corporation ambapo kazi ilianza Februari 28, mwaka huu na umetekelezwa kwa asilimia tano.

Anasema pamoja na mambo mengine, wanatarajia kujenga gati ya vyombo vidogo yenye urefu wa mita 120, lakini bado jinsi ya kuhifadhi mizigo imekuwa changamoto watajenga maghala makubwa matatu ya kuhifadhi abiria.

“Mradi wa Kibirizi ni sehemu mojawapo ya mradi ambao una sehemu tatu, mradi wa Bandari ya kibirizi, Ujiji na mradi wa Ofisi ya Meneja wa Bandari.

“Ujenzi wa gati hili litakuwa na urefu wa mita 250, mradi huu kwa ujumla katika sehemu zote tatu unagharimu Sh bilioni 33, Ofisi ya Meneja wa Bandari ambayo itakuwa jengo la ghorofa moja, lakini sehemu kubwa ya mradi iko katika eneo hili la Kibirizi.

“Pia kuna changamoto ya watu kuingia bandarini hapo kiholela, kwa hiyo kwenye mradi huo kutakuwa na uzio wa kuzunguka eneo lote la bandari na hivyo kuruhusu watu pekee wanaokwenda kwa ajili ya shughuli za bandari au wafanyabiashara na abiri lakini wengine watakuwa wanafanya shughuli zao nje.

“Zamani watu walikuwa wakipanda na kushuka huku wanakanyaga maji lakini kwa hivyo sasa hivi tumeweka maboya ambayo yanaruhusu watu kwenda katika maeneo yao.

“Ni uwekezaji mkubwa takribani zaidi ya Sh bilioni 20 zitatumika katika kutekeleza mradi huo, ambazo manufaa yake yako wazi na wakati tunasubiri utekelezaji wa mradi huo kukamilika tumefanya jitihada za kuwafanya watu waendelee kuwa abiria wetu,” anasema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga anatoa wito kwa wafanyabiashara badala ya kupitisha mafuta barabarani kutoka Dar es Salaam kwenda Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutumia Bandari ya Kigoma.

“Kama kuna changamoto tukae tutatue Hilo tuone uzito uko wapi katika kutumia miundombinu ya bandari yetu.

“Tunawahimiza pia wenzetu wa TRC kumalizia ujenzi kwani kuimarika kwa reli kutaleta tija kwa sababu tunafahamu jitihada zinazoendelea,” anasema Anga.

Pamoja na Mambo mengine anasema bandari zote za Ziwa Tanganyika zimeunganishwa kwenye mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), unaotegemewa kupunguza muda mrefu wa kuhudumia wateja.

Mwonekano wa Bandari ya Kigoma.

Bandari ya Kagunga

Katika Bandari ya Kagunga inayounganisha mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Burundi, yenyewe imeenda mbali zaidi kwani licha ya ukarabati unaoendelea inajenga soko litakalohudumia wananchi katika bandari hiyo na maeneo jirani.

Jumla ya Sh milioni 930 zimetengwa na TPA, kwa ajili ya ujenzi wa barabara na kulipa fidia wakazi katika bandari hiyo.

Pia, imetoa Sh milioni 190 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa lililopo karibu na bandari hiyo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 45.

Msese anasema hatua hiyo inatokana na barabara ya lami kuishia katika mpaka wa Burundi huku njia ya kuifikia bandari hiyo ambayo ni mita 700 ikiwa ya vumbi.

“Katika bandari hii kuna barabara ya kiwango cha lami lakini imeishia katika mpaka wa Burundi hivyo barabara ya kuingia bandarini haijaunganishwa hivyo TPA imetenga fedha hizo kwa ajili ya kulipa fidia za wakazi na kujenga barabara za kiwango cha changarawe.

“Lakini pia tuna lengo la kushirikiana na halmashuari ya wilaya hii kufanya mradi wa ujenzi wa soko ni kufungua fursa za kibiashara katika bandari hiyo inayounganisha nchi za Tanzania, Burundi na Congo,” anasema.

Bandari ya Kagunga.

Bandari ya Kasanga

Bandari ya Kasanga iliyoko mkoani Rukwa nayo inatarajiwa kuwanufaisha wafanyabiashara na wasafirishaji wanaosafirisha mizigo hususani saruji kwenda nchini Burundi na Congo baada kukamilika kwa upanuzi wa gati la kisasa katika bandari hiyo.

Mradi huo pia unatekelezwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kwa gharama ya Sh bilioni 4.764, unatarajia kukamilika mwakani ambapo pamoja na mambo mengine utawezesha bandari hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuongeza mapato kutokana na kuongeza idadi ya meli zinazokuja na kuondoka nchini kupakia na kupakua shehena na abiria.

Msese anasema kwa sasa bandari hiyo ina gati lenye urefu wa mita 20 lenye uwezo wa kupokea meli moja huku mkakati wa TPA ukiwa ni  kuongeza gati lenye urefu wa mita 100 na kufikia mita 120, litakalowezesha kupokea meli tatu za mizigo na abiria kwa wakati mmoja na hivyo kuondoa msongamano wa meli bandarini hapo.

“Bandari hii ndiyo inategemewa na nchi za Congo na Burundi katika kusafirisha saruji kutoka Mbeya, kwa hiyo upanuzi wa bandari hii kwa ujumla utakaogharimu Sh. bilioni 4.7 utawezesha shehena kubwa ya saruji kusafirishwa kwenda nchi hizo kutoka tani 20,000 kwa mwaka hadi tani 100,000 kwa mwaka.

“Bidhaa kubwa inayosafirishwa kwenda nchi za Congo na Burundi ni saruji ambayo inazalishwa na Kiwanda cha Saruji cha Mbeya (Mbeya Cement), hivyo tunatarajia mizigo itakayosafirishwa itaongezeka mara tano zaidi” anasema.

Msese anasema kuboreshwa kwa bandari hiyo ambayo ni moja ya kimkakati inayotegemewa na mikoa ya Katavi, Mbeya, Songwe na Rukwa utawezesha kukuza uchumi wa taifa.

Bandari ya Kasanga.

Bandari bubu

Licha ya mafanikio mengi yaliyopo katika Kanda ya Ziwa Tanganyika, bado inakabiliwa na changamoto ya bandari bubu ambazo zinaikosesha nchi mapato.

Kutokana na hali hiyo, ukanda huo uko kwenye mchakato wa kurasimisha na kufunga bandari ambazo hazipo kwa mujibu wa sheria.

Msese anasema lengo la hatua hiyo ni kuzifanya bandari hizo zifanye kazi kulingana na kanuni na taratibu za kisheria na hivyo kuimarisha ulinzi na usalama.

“Utaratibu wa urasimishaji na kuzifunga bandari hizo bubu unaendelea na ukishamalizika tutazitangaza,” alisema.

Wilayani Nkasi, iko Bandari ya Kirando ambayo inadaiwa kuwa bandari bubu sugu licha ya kuzuiwa kufanya shughuli zake imekuwa ikiendelea kufanya kinyemela.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, anakemea bandari bubu huku akipiga marufuku matumizi yake bandari bubu wilayani humo na kuwataka watumiaji wa bandari hizo kutumia bandari rasmi ya Kapili.

 Anasema Bandari ya Kipili, imefanyiwa ukarabati na TPA kwa shughuli zote za bandari huku hivyo watu waache kutumia bandari bubu ya Kirando ambayo haina ofisi za taasisi muhimu za serikali ikiwamo Mamlaka ya Mapato (TRA).

Aidha, Mtanda ambaye alikuwa kwenye operesheni maalumu ya kutembelea bandari bubu wilayani humo, ameahidi kufanya operesheni maalumu kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kuzuia matumizi ya bandari bubu zote zilizopo na zinazofanya kazi katika maeneo ambayo hayajarasimishwa na kuisababisha Serikali kukosa mapato.

“Bandari ya Kipili, imejikamilisha kwa ofisi mbalimbali na miundombinu ikiwamo ya barabara, ambapo ukarabati na ujenzi huo umegharimu  Sh milioni 430 ikiwamo ujenzi wa eneo la kuegesha magari makubwa na madogo.

“Baada ya uboreshaji huu mkubwa kukamilika, bandari yetu imekuwa ya kisasa, hivyo ni wakati muafaka kwa wanaofanya shughuli za bandari kuanza kuitumia na kuachana na bandari bubu zote zinazozunguka wilaya hii ya Nkasi.

“Natoa wito kwa watumiaji wa bandari bubu zote kuacha kuzitumia mara moja hii bandari inajitosheleza. Tutafanya operesheni maalumu kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama tutakaowakamata wanatumia bandari zilizopigwa marufuku tutawachukulia hatua za kisheria,” anasema.

Mtanda anasema TPA wameshabaini bandari bubu 45 zilizopo katika wilayani hiyo na zitakazorasimishwa ni tano na nyingine zitafungwa ili kuongeza ufanisi wa mamlaka.

Hamis Mselemu ni msimamizi wa bandari hiyo ya Kapili, anasema gharama za kusafirisha mizigo zinalingana na zile wanazotozwa wafanyabiashara katika bandari bubu hivyo anawasihi kutumia kutumia bandari sahihi kwa mujibu wa sheria.

Mmoja wa mafundi wanaojenga gati ya Bandari ya Kabwe katika Ziwa Tanganyika, akitoka kupanga mawe chini ya maji.