Home Makala TRAFIKI WAELIMISHE UMMA, WASIKIMBILIE ADHABU

TRAFIKI WAELIMISHE UMMA, WASIKIMBILIE ADHABU

993
0
SHARE
Askari wa usalama barabara akiandika maelezo ya ajali

“..hivi kila ajali ni mwendokasi? Huo mwendokasi ni upi?? Gari ikiwa kwenye mwendo upi ndio haitakuwa kwenye mwendokasi?? Mbona hamsemi labda itilafu ya gari? Woote mnawaza makosa ya dereva tu, hebu tupeni chanzo cha ajali ni nini na sio jibu la jumla la mwendokasi!!”

Nukuu hiyo hapo juu nimeichukua katika mtandao wa FB katika majadiliano kuhusu suala zima la usalama barabarani ambalo katika siku za mwisho wa mwaka huwa ni nyeti.

Mjadala umekuwa ukiendelea katika kona mbalimbali hapa nchini kuhusu kile kinachoonekana kama ni serikali kukaza uzi katika kuwajaribu kukabiliana na ajali za kila uchao.

Hapana shaka hata kidogo kwamba ajali za barabarani zinatumaliza. Haipiti siku hujasikia kwamba kuna ajali imesababisha vifo na ulemavu kwa wananchi mbalimbali kote nchini hususan katika mazingira ambayo barabara nyingi kubwa ni nzuri na zinazoweza kupitika kwa kasi kubwa.

Ajali za barabarani ni tishio. Maisha ya watu wetu yamekatishwa kutokana na ajali za barabarani. Maswali hayo hapo juu nimeyakuta katika mjadala wa Mabalozi wa Usalama Barabani (RSA) mwisho wa wiki iliyopita. Bila shaka ni hoja za msingi sana.

Mjadala kuhusu usalama barabarani na hatua ambazo serikali imeamua kuzichukua katika harakati za kupambana na adha hiyo hivi sasa ni suala la kila siku.

Kwamba ajali za barabarani zimemaliza maisha ya wapendwa wetu bila shaka halina ubishi. Lakini pia ni kweli kwamba hatua zinazochukuliwa na serikali katika jitihada za kupambana na adha hiyo zimeibua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu musharabu.

Baadhi ya madereva wanadai kwamba mwendokasi si tatizo. Kwamba mwendokasi hausababishi ajali na badala yake wanaosababisha ajali ni madereva walevi, wavuta bangi na wala mirungi.

Kuna madereva ambao wanahoji kwamba eti kama mwendokasi ni tatizo basi kwa nini waliotengeneza hayo magari wakayawezesha kukimbia kwa kasi ambayo imeoneshwa katika mita ya spidi. Inawezekana lisiwe swali linaloweza kujibiwa kirahisi lakini ni kwamba udhibiti wa huo mwendo unatokana kwa kiasi kikubwa na utafiti wa sababu za ajali.

Matokeo ya utafiti yameonesha kwamba idadi kubwa ya ajali za barabarani inatokana na mwendo kasi kwa sababu moja tu rahisi. Kwamba unapokuwa katika kasi kubwa kusimama au kukwepa ajali ni kazi ngumu. Ukitaka kujua ugumu wake jaribu kukimbia kwa kasi halafu ghjafla ukutane na korongo.

Hata hivyo, katika jitihada za serikali za kupunguza ajali za barabarani kama si kuzimaliza kabisa kuna maoni mbalimbali. Kuna wanaosema kwamba serikali imechukua hatua nzuri nazenye tija katika kukabiliana na tatizo hilo.

Lakini wapo wanaodai kwamba hatua ambazo hivi sasa zimechukuliwa hazina maana kabisa na kwamba hatua hizo ni za hovyo na zinazowakwaza madereva jambo ambalo si zuri na ni kinyume na haki za binadamu.

Kinachofanyika hivi sasa ni kwamba katika kudhibiti mwendokasi madereva wamelazimishwea kufuata sheria zote za usalama barabarani. Moja ya sheria ambazo zinasimamiwa vizuri na maaskari wa usalama barabarani ni mwendokasi.

Askari wanahakikisha kwamba kila dereva anafuata sheria alizofundishwa darasani na kuapa kuzitekeleza na moja ya sheria hizo ni kutambua maeneo ambayo anaweza au anatakiwa kuendesha kwa kasi fulani.

Imekuwa ni kawaida hapa nchini hususan kwa madereva wa mabasi ya abiria kutokufuata sheria na kuzigeuza barabara zote kwamba ni sawa na zile za mashindano ya magari ya langalanga. Kutokana na mchezo huo wa hatari taifa hili limekuwa likipata majanga ya vifo hususan baada ya jitihada za serikali za kuhakikisha kwamba mikoa yote inaunganishwa kwa barabara za lami.

Barabara za lami zimekuwa ni kivutio kwa madereva wetu kutaka kupima kasi ya magari wanayoyaendesha bila ya kujali kwamba kuna roho za watu kibao ndani ya magari yao, Watu ambao wangeulizwa kati ya kufika kwa mwendo mdogo ulio salama na kuwahi sana kwa mwendo ambao si salama bila shaka kama wana akili timamu wangechagua mwendo ulio salama.

Hivi sasa suala la mwendokasi limekuwa na mjadala mkubwa kote nchini. Mjadala wenyewe umetokana na baadhi ya wamiliki wa mabasi na madereva kudai kwamba kuwataka kuendesha magari kwa kutumia alama za barabarani zilizopo hivi sasa ambako katika baadhi ya maeneo wanatakiwa kuendesha kwa kasi ya kilomita 50 kwa saa ni kuwachelewesha na hiyo inawasababishia hasara.

La kushangaza ni kwamba hayo magari ambayo wanataka kuyakimbiza yanapofika yaendako yanalala na wala si kwamba wanapoteza biashara kwa sababu hawageuzi papo kwa hapo.

Dereva mmoja wa Hiace kutoka Moshi Mjini kwenda Machame alilalamika kwamba hakuna sababu yoyote ile ya kuwalazimisha madereva kutembea kilomita 50 kwa saa katika hayo maeneo ambayo alama za barabarani zimeoneshwa kwa sababu mwendo kasi si tatizo na badala yake tatizo ni ulevi.

Inawezekana kwamba tatizo ni ulevi. Lakini huo ulevi huwezi kuujua kama si kutokana na vitendo vya dereva vya kutotii sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.

Pamoja na kukubaliana na serikali na wadau wa usalama barabarani kwamba kuna tatizo la uendeshaji wa magari kwa kasi inayotishia maisha ya wananchi pia kuna haja ya kuangalia ni njia ipi au zipi sahihi za kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa.

Hivi utaratibu wa sasa hivi wa askari kujificha na kuvizia madereva wanaoendesha kwa kazi kubwa katika maeneo ambayo wanatakiwa kuwa na mwendokasi wa kilomita 50 kwa saa ni sahihi?

 

Suala la askari kujificha na kuzipiga tochi gari ambazo zinakiuka sheria linaweza kuonekana kama ni kuviziana. Lakini kuviziana huko kunatokana na ukweli kwamba wanaoviziwa kama walipata leseni kwa njia halali wanatambua kwamba wanachokifanya ni kosa. Sasa kama wanatambua kwamba alama za barabarani zinatakiwa kuheshimiwa na walifanya mtihani wa darasani na barabarani na kufaulu na ndiyo sababu wakapatiwa leseni kwa nini inakuwa vigumu kwao kuifuata hiyo sheria?

Pengine jambo ambalo linaweza kujadiliwa ni kuhakikisha kwamba askari wa usalama barabarani hawatumii sheria na kanuni zilizopo kuwakomoa madereva. Inamaanisha kwamba moja ya vitu ambavyo askari wanatakiwa kufanya ni kutoa elimu ya udereva na uraia kwa madereva na raia sawia katika kampeni hii ya kudumu ya kuhakikisha kwamba ajali za barabarani zinapungua kama si kutokomezwa.

Ni wazi kwamba abiria wanaotambua haki zao kama wasafiri hawatamruhusu dereva ye yote yule awaye kuendesha gari kwa kasi isiyokubalika. Kama abiria watatmbua wajibu wao kwa Mungu wao wa kulinda uhai wao bila shaka watahakikisha kwamba hakuna dereva ye yote awezaye kuyatishia hayo maisha kwani ni tunu ya kipekee kutoka kwa Mungu.

Abiria anayetambua kwamba maisha yake hayawezi kuwekwa rehani atakuwa ni kiongozi wa dereva. Hapana ubishi kwamba dereva anapotambua kwamba anaowaendesha humo ndani ya gari ni mabosi wake na kwamba inabidi awasikilize bila shaka hawezi kuthubutu kunywa viroba akiwa kwenye usukani au kutafuna miraa.

Hivi sasa askari wanalalamikiwa kwamba wameipoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) majukumu yake ya kukusanya mapato kutokana na faini wanazopigwa madereva katika siku za karibuni. Hapana ubishi hata kidogo kwamba kumekuwapo na mashindano ya kukusanya mapato kutokana na makosa ya usalama barabarani.

Hili la ukusanyaji wa mapato kupitia faini za makosa ya usalama barabarni lina utata kidogo kutokana na ukweli kwamba badala ya askari wa usalama barabarani kutoa elimu ya uraia badala yake wanaonekana kama ni wakusanyaji wa mapato zaidi. Haishangazi kusikia lawama zikitiupwa kwa askari wetu hao na watunga sheria, wasimamizi wa sheria na wengineo.

Haipendezi hata kidogo kuona askari analazimisha kosa wakati kila ushahidi unaonesha kwamba hakukuwapo na kosa lolote. Hili linaitwa kwa lugha nyepesi ni kubambikiza au kumkomoa dereva. Hii inaudhi na badala ya kusaidia kuondokana na tatizo inazidisha tatizo. Raia anayeonewa atajitahidi kujitetea na matokeo yake mara nyingi si chanya.

Yapo makosa ambayo si lazima kumpiga faini dereva. Kwa mfano hivi dereva ambaye yupo katika foleni anatoka Tangi Bovu unapomkuta hajafunga mkanda kuna sababu gani ya msingi ya kumwadhibu kwa faini? Ni kweli ni kosa kutokufunga mkanda lakini katika mazingira ambayo gari inatembea katika kasi ya kilomita 10 kwa saa kuna sababu yoyote ya msingi ya kumbana kwa faini dereva?

Au tujiulize ni kwa nini askari wa usalama barabarani anampiga faini mtu ambaye bima yake imeisha jana na yupo njiani kwenda katika kampuni ya bima ili apate nyingine?

Kwa nini askari wa usalama barabarani anamfokea dereva badala ya kumuelimisha? Anamfokea na halafu anampiga notifikesheni akalipe faini wakati kumbe angeliweza kumpa kisomo tu na kikamwingia.

Kama askari wetu wataendelea na tabia ya kukomoana ni wazi kwamba watakapokuwa hawapo barabarani kwa sababu moja au nyingine hao wanaowadhibiti watajitangazia uhuru na matokeo yake watakaoumia ni pamoja na wao kwani wao pia ni watumiaji wa huduma hizo hizo. Ni muhimu kujirekebisha.

Wananchi wakishirikishwa katika kampeni za usalama barabarani kwa asilimia mia moja bila shaka itakuwa rahisi kuwadhibiti madereva na makondakta kwa sababu maisha ya wananchi yatalindwa na wananchi wenyewe na pengine wananchi wakijua haki zao vizuri hakuna dereva atakayethubutu kucheza na maisha yao.