Home Latest News TRUMP APINDUA MEZA YA OBAMA

TRUMP APINDUA MEZA YA OBAMA

1087
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU NA MITANDAO,

Jumatatu iliyopita ilikuwa ya kwanza kwa Donald Trump kuanza kazi rasmi ofisini kwake Ikulu ya White House na tayari, kama alivyoahidi wakati wa kampeni, ameanza kubadilisha sera na maagizo kadha ya mtangulizi wake Barack Obama.

Mabadiliko hayo, pamoja na mambo mengine ni pamoja na kujitoa mikataba ya kimataifa, na kubadilisha habari fulani katika tovuti rasmi ya Ikulu.

Trump alisema lengo kubwa la mabadiliko kama haya ni kuzifanya sera za Marekani kwanza kabisa zizisaidie nchi hiyo kiuchumi, kibiashara na kiulinzi.

Kwa mfano siku ya Jumatatu wiki hii ametia saini Agizo la Rais (Executive Order) la nchi yake kujitoa kutoka mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na nchi za eneo la Bahari ya Pacific (Trans-Pacific Partnership – TPP), mkataba uliotiwa sahihi Februari mwaka jana na nchi 12 ambazo kwa pamoja zinazalisha uchumi wa asilimia 40 duniani.

Na kama hiyo haitoshi Trump anatarajiwa kuanza mchakato wa kuuvunja mkataba wa kibiashara na nchi za Amerika ya Kaskazini – NAFTA ambazo wanachama ni yenyewe Marekani, Canada na Mexico – na kuanza mazungumzo ya mkataba mpya wa kibiashara baina ya nchi hizo.

Shoka lake pia limeelekezwa kwenye misaada ya kifedha iliyokuwa ikitolewa kwa taasisi zisizo za Kiserikali kugharamia utoaji mimba na uzazi wa mpango katika nchi mbali mbali duniani.

Kwa mfano tangu rais wa 40 wa nchi hiyo Ronald Reagan wa chama cha Republican mwaka 1984 alipotia sahihi Sheria iliyozuia ugharamiaji huo ya Global Gag Rule, ikawa kawaida kila rais wa chama cha Democratic anapoingia huifufua sheria hiyo, na kila rais wa chama cha Democratic anaposhika nchi huifuta.

Aidha Rais Trump amefanya mabadiliko makubwa kwenye tovuti rasmi ya Ikulu ya White House. Ameagiza kuondolewa kabisa lugha ya Kihispania iliyokuwa inatumika katika tovuti hiyo sambamba na ile ya Kiingereza.

Wakati wa kampeni Trump alikuwa anawakejeli wapinzani wake waliokuwa wakitumia lugha ya Kihispania ili kuwafikia wengi wasiokuwa wanafahamu Kiingereza. Asilimia 17 ya Wamarekani ni watu wa asili ya Hispania (Hispanics). Trump alisema: “Hii ni nchi yetu inayozungumza Kiingereza.”

Kingine kilichobadilishwa wiki iliyopita katika tovuti ya Ikulu ni katika sehemu kuhusu mazingira na tabia nchi. Kurasa zoteza habari kuhusu azma ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi zilizokuwa sera kuu ya Obama ziliondolewa bila maelezo.

Hata hivyo badala yake ikawekwa habari za sera za Trump za wakati wa kampeni kuhusu nishati iliyokuwa na kichwa cha habari ‘America First Energy Plan’ ambacho chini yake kilisema “Rais Trump anapigania kuondoa sera zisizo lazima na haribifu kama vile ‘Mpango Kuhusu Tabia Nchi na Sheria ya Matumuizi ya Maji nchini Marekani’ (Climate Action Plan and the Waters of the US rule).

Trump alisema kuondolewa kwa sera hizi alizoziita zuilifu zitasaidia nchi yake kuongeza mapato na ujira kwa kiwango cha zaidi ya Dola 30 bilioni katika miaka saba ijayo.

Kingine alichobadili wiki hii ni kuwarudisha nyumbani mabalozi wote wa Marekani walio nchi za nje na hivyo atachagua wengine.

Lakini sera kubwa ya mtangulizi wake Barack Obama ambayo Trump siku zote aliahidi kuiondoa ni ile kuhusu mpango wa bima ya afya — maarufu ‘Obamacare.’

Lakini suala hili, kwa kuwa lilikuwa ni la Sheria ya Bunge, basi Mabunge yote mawili ya nchi hiyo – Baraza la Wawakilishi na lile la Senate yaridhie. Chama chake cha Republicana kina uwingi (majority) katika mabunge yote hayo mawili.