Home KIMATAIFA TRUMP ASHAURIWA KUTOA MSAMAHA KWA ASSANGE WA WIKILEAKS

TRUMP ASHAURIWA KUTOA MSAMAHA KWA ASSANGE WA WIKILEAKS

667
0
SHARE

HILAL K SUED

Wiki iliyopita habari zilienea kule Marekani kwamba rais Donald Trump alikuwa anafikira kutoa msamaha kwa Julian Assange muasisi wa mtandao wa Wikileaks.

Julian Assange, raia wa Australia na mtaalamu wa masuala ya kutengeneza programu za computer amepata hifadhi katika jengo la Ubalozi wa Euador, London Uingereza tangu 2012 na amekuwa akitafutwa na mamlaka za mashitaka za Sweden kwa makosa ya kubaka na pia serikali ya Marekani inamtaka kwa mashitaka ya kuvujisha siri za serikali kupitia mtandao wake wa Wikileaks.

Habari hizi sa sasa hivi zimejiri baada ya Mjumbe wa Baraza la Uwakilishi la Marekani kutoka Jimbo la California Dana Rohrabacher wa chama cha Republican kukutana na assange kujadili masuala muhimu yanayotakiwa yafanyike ili kumuondoa kutoka huifadhi ya ubalozi huo.

Assange amekana tuhuma hizo za ubakaji na alikuwa tayari kwenda Sweden kukabiliana na mashitaka hayo lakini amekuwa na hofu kwamba tuhuma za ubakaji ni kiini macho tu kwani lengo hasa ni baadaye kumsafirisha hadi Marekani kuyakabili mashitaka ya kuvujisha siri za serikali ya nchi hiyo.

Aidha kutokana na mikataba ya kimataifa kuhusu masuala ya kidiplomasia serikali ya Uingereza haiwezi kumkamata Assange akiwa ndani ya ubalozi wa Ecuador kwani ubalozi huo unahesabiwa kama ni ardhi ya nchi hiyo ya Amerika ya Kusini.

Mwakilishi Dana Rohrabacher katika mahojiano na mtandao wa Daily Caller alisema alikua anatoa ushauri kwamba Assange anaweza kupewa msamaha ya kutoshitakiwa nchini Marekani iwapo tu atatoa habari kuhusu barua-pepe za chama cha Democrati mwaka jana kuhusu uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi wa marekani uliompa ushindi Donald Trump.

Alisema barua pepe hizo zinaweza kumsaidia trump kujinasua katika tuhuma kwamba ushindi wake uligubikwa na uingiliaji wa Urusi.

Yote haya yanakuja miezi miwili baada ya Mwanasheria Mkuu wa Marekani Jeff Sessions kusema serikali yake ilikuwa inamwandalia mashitaka Julian Assange.

Kauli ya kutaka kumfungulia mashitaka Assange – hata kama uwezekano wa kumtia mbaroni bado ulionekana kuwa mgumu – uliibua maswali ambapo wachunguzi wa mambo waliona kama vile Trump anakosa shukurani.

Wachunguzi wa mambo walisema wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana mtandao wa Assange wa Wikileaks ulifanya kazi kubwa ya kumkandamiza mgombea wa chama cha Democrat Hillary Clinton hasa kutokana na lile suala la barua pepe (email).

Wikileaks ulikuwa unaweka wazi mawasiliano ya kikazi ya Clinton aliyokuwa akifanya kupitia barua pepe za msaidizi wake binafsi badala ya kutumia zile za kiserikali, na Trump, wakati wa kampeni, alikuwa anayataja sana mapungufu ya mshindani wake huyo wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje chini ya utawala Barack Obama.
Aidha ikumbukwe kwamba baada ya uchaguzi tu Rais Trump aliusifia sana mtandao wa Wikilieaks kwa kazi yake kubwa wakati wa uchaguzi pale ulipokuwa unamwaga hadharani barua pepe hizo za Clinton. Baadaye Hillary Clinton alisema suala hilo lilichangia sana katika kushindwa kwake uchaguzi.

Taasisi za kijasusi za Marekani zilisema kwamba Urusi ilihusika katika udukuzi wa barua pepe hizo na kwamba nchi hiyo ya Putin iliutumia sana kumdhhoofisha Clinton na kumkweza Trump.

Wadukuzi walikuwa katika ajira ya mashirika ya kijasusi ya Urusi walidukua maelfu ya barua pepe kutoka mitandao ya chama cha Democratic na mitandao ya maafisa wa kampeni ya Clinton na walitumia mawakala kuziwasilisha Wikileaks ambako zilichapishwa.

Hata hivyo kwa upande wake Assange alisema kuziweka hadharani barua pepe zilizodukuliwa haukuwa na lengo la kuuathiri uchaguzi.

Lakini hivi sasa utawala wa Trump umeanza kuwa na mtazamo hasi wa shughuli za Wikileaks.

Kwa mfano Machi mwaka huu mtandao wa Wikileaks ulisambaza habari kuhusu namna Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) lilivyokuwa linafanya udukuzi wa mitandao ya watu wengine, habari ambazo utawala wa Trump haukupenda watu wengine wajue.

Na wiki iliyopita Mkurugenzi wa CIA Mike Pompeo alizianisha habari za kiintellijensia zinazoenezwa na Urusi ikishirikiana na mtandao wa Wikileaks kuwa ni uongo mtupu na  hasi kwa Marekani.

Aliongeza kwa kusema kwamba kuibuka kwa habari hizi mpya za udukuzi wa Wikileaks kunaifanya Marekani “isiwe salama hivyo wakati umefika wa kuuainisha mtandao huo jinsi ulivyo – kwamba una malengo maovu na unasaidiwa na nchi adui kama vile Urusi.”

Assange aliuanzisha mtandao wa Wikileaks mwaka 2006 ambapo ulianza kuchapisha milolongo ya uvujaji wa habari za siri alizopatiwa na askari mmoja wa Marekani Chelsea Manning aliyeziiba.

Awali habari nyingi za uvujaji zilihusu vita ya Afghanistan na ile ya Iraq. Baada ya uvujaji wa mwaka 2010 serikali ya Marekani ilianza uchunguzi kuhusu Wikileaks hususan nani mhusika na kuomba mataifa mengine rafiki kusaidia.

Novemba mwaka huo ombi lilitolewa na serikali ya Sweden ili Assange apelekwe nchini humo kujibu mashitaka ya ubakaji aliyofanya alipokuwa kule siku za nyuma.

Assange alikuwa akikana tuhuma hizo za ubakaji na aliona hizo ni njama kati ya serikali za Sweden na Marekani ili baadaye apelekwe Marekani kwa kosa la kuchapisha siri za serikali ya nchi hiyo.

Desemba 7 2010 Assange alijisalimisha kwa mamlaka za kipolisi za Uingereza na alishikiliwa kwa siku 10 na baadaye kuachiwa kwa dhamana. Baadaye aliomba na kukubaliwa rasmi hifadhi katika ubalozi wa Ecuador Agosti 2012.

Hawezi kuondoka ubalozini hapo kwa sababu akifanya hivyo atatiwa mbaroni kwa kosa la kukiuka masharti ya dhamana chini ya Sheria ya Dhamana (Bail Act).