Home Makala Trump atashindaje Urais wa Marekani?

Trump atashindaje Urais wa Marekani?

926
0
SHARE

Wakati kura za maoni nchini Marekani zikiendelea kuonesha kuwa mgombea Urais kwa Tiketi ya chama cha Democrats Hillary Clinton anaongoza dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump, hali inaonekana kuendelea kuwa tete kwa mgombea huyo wa Republican na kinachobaka unaweza kusema ni muujiza tu ndio unaoweza kumfanya ashinde urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumanne ya Novemba 8, mwaka huu.

Trump anaonekana bayana kuwa hafanyi vizuri hata katika majimbo ambayo kitamaduni mara nyingi yamekuwa yakipigia wagombea wa Republican. Kutokana na hali hii, nafasi ya kuendelea kuandika historia kwa Mwanamama Hillary Clinton inaonekana iko wazi nan i siku tu zinazosubiriwa ili awe Mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa nafasi ya Urais nchini Marekani. Kura nyingi za maoni zinampa nafasi kubwa na inaonekana kuwa hana upinzani wa kutisha kama ilivyozoeleka katika chaguzi hizo.

Hadi sasa hali inaonekana kuwa murua kwa Clinton maana mazingira ya kupata kura (Electoral College votes) zinazohitajika 270 yapo wazi. Kura za maoni zinamuonesha akiwa juu hali inayotabiri kuwa anaweza kushinda na kupata zaidi ya kura hizo 270. Hii inaonekana kutokea hata kama hatashinda majimbo ya Ohio na Frolida. Ushindi kwa Clinton unaonekana kuwa dhahiri hata kama atapoteza majimbo yenye mrengo wa Kati wa Democrat ya Pennsylvania na Colorado.

Taarifa ya uchambuzi kutoka kituo cha Televisheni cha  ABC zilizotolewa wiki hii zinaonesha kuwa Clinton tayari amefikisha kura za ‘Electoral College’ 300. Uchambuzi huu umefanyika huku ukizingatia kuwa hata Trump akishinda majimbo yasiyotabirika bado haimfanyi Clinton kushindwa.

Uchambuzi huo pia unaonesha kuwa, yapo mazingira nadra yanayoweza kumfanya Trump kushinda. Inaelezwa licha ya mazingira hayo, hali haitakuwa rahisi kwa kuwa mgombea wa Democrat anaonekana kuzidi kufanya vizuri hata katika majimbo ambayo Trump lazima ashinde. Majimbo hayo ni pamoja na North Carolina, Ohio na Florida.

Kwa hali ilivyo sasa na kadri siku zinavyoyoyoma, kila mgombea anaonekana kuwa makini lakini hali kwa upande wa Trump inaonekana kuwa ngumu. Kosa dogo analoweza kufanya kuanzia leo hadi siku ya uchaguzi ni sawa na kumuwashia taa ya kijani mgombea wa Democrat kwenda Ikulu. Tena ikitokea akafanya kosa lolote itakuwa ni mara ya tatu mfululizo kwa chama cha Democrat kushinda uchaguzi mkuu wa Marekani.

Ni mambo yapi anayotakiwa kuyafanya Bilionea Donald Trump ili aweze kushinda? Yapo mambo kadhaa lakini yote ynabakia katika suala moja tu yaani kutegemea muujiza. Pia chambuzi mbalimbali zinaonesha kuwa ili Trump ashinde uchaguzi huu, basi karata zake zikae vema katika masuala yafuatayo:

Jambo la kwanza ni kuhakikisha anashinda majimbo yote aliyoshinda mgombea wa Republican mwaka 2012,  Mitt Romney. Donald Trump anatakiwa kushinda majimbo yote ambayo Mitt Romney alishinda mwaka 2012. Majimbo haya ni pamoja na yale ambayo kiutamaduni ni majimbo ya Republican. Majimbo haya ni kama Arizona na Georgia.

Historia za uchaguzi wa Marekani zinaonyesha kuwa majimbo hayo yaliwahi kwenda kwa Democrats mwaka 1996 wakati Bill Clinton akiwa mgombea. Katika uchaguzi wa mwaka huu, majimbo haya yanaonekana kugawanyika na Clinton anaonekana kujitahidi kuvutia wapiga kura na kura za maoni zinaonesha kuwa anayo nafasi ya kushinda.

Katika jimbo la Utah, mgombea binafsi Evan McMullin anaonekana kuwakamata vizuri wamormoni wa jimboni humo hali inayoonesha kuwa anaweza kushinda Uttah. Pia jimbo la North Carolina linaonekana kuwa na changamoto kubwa kwa Trump kushinda. Jimbo hili lilipigia Republican mwaka 2012 kwa asilimia mbili. Kwa mujibu wa kura za maoni za kituo cha CNN zilizotolewa mapema wiki hii, hali ya jimboni hapo inaonesha kuwa Clinton anaongoza kwa 48% dhidi ya Trump mwenye  47%.

Suala la pili ni lile linalomhitaji Trum kushinda jimbo la  Ohio. Hakujawahi kuwa na mgombea wa Republican aliyewahi kushinda urais bila kushinda jimbo la Ohio.

Kutokana na hali hii lazima Trump ashinde jimbo hili ili aweze kupata nafasi ya kushinda urais. Kura za awali zinaonesha mazingira ya Trump kushinda jimbio hilo. Hali hii inatokana na wapiga kura wachache wa Democrats.

Kura ya maoni iliyofanywa na ABC hivi karibuni inaonesha Trump anaongoza jimboni hapa kwa 42% huku Clinton akiwa na asilimia 41. Kura nyingine ya maoni iliyofanywa na Chuo Kikuu cha Quinnipiac inaonesha kuwa wagombea wote wanalingana nguvu kwa asilimia 45.

Jambo la tatu ni Trump kushinda jimbo la Florida. Jimbo hili linaonekana kuwa gumu kwa Clinton huku pia likiwa muhimu sana kwa Trump kushinda.

Kura za maoni mbili zilizofanywa na Chuo Kikuu cha Quinnipiac zilizofanyika wiki mbili zilizopita, zinaonesha Clinton akiwa na ushindi mwembamba jimboni hapa na Trump hajaonekana kushinda kura ya maoni yoyote Frolida tangu mwezi wa Julai. Hadi sasa kura za awali zinaonesha hali nzuri kwa Clinton na bila kushinda jimbo hili hali ya Trump kwenda ikulu inabaka kuwa ndoto.

Jambo la nne ni lile linalomtaka Trump kupata ushindi wa aina yake wa ‘Electoral Vote’ 17. Hata kama Trump atafanikwa katika majimbo yote hayo hapo juu, bado atatakiwa kutafuta kura 17 na mazingira ya kuzipata yanaonekana kuwa magumu mno. Anaonekana kuwa nyuma sana katika kura za maoni na ili afanikiwe atatakiwa kufanya yafuatayo: Mosi, atatakiwa kushinda Pennsylvania.

Idadi ya wafanyakazi wazungu katika jimbo hili wanaonekana kumbeba Trump. Lakini bado kampeni haijaisha na itampasa kuongeza matangazo mengi zaidi katika jimbo hili. Kura ya maoni ya hivi karibuni iliyofanywa na Bloomberg inaonesha Clinton akiwa mbele kwa asilimia 9. Jimbo hili linazo kura 20. Kama atafanikwa kuzipata zitakuwa zinampa ahueni kubwa Trump ili kushinda urais. Jambo la kuzingatia ni kuwa jimbo hili halijawahi kumpa ushindi mgombea wa Republican tangu mwaka 1988.

Ushindi katika majimbo yote madogo nalo ni jambo jingine analotakiwa kulifanya Trump ili ashinde. Kama atafanikiwa kushinda majimbo yote madogo inaweza kumsaidia kushinda. Majimbo haya ni kama Iowa, Nevada, New Hampshire na Maine  pamoja na hayo tuliyoyaorodhesha hapo juu yatampa kura 270. Japokuwa Iowa na Nevada yanaonekana nafuu kwa Trump lakini kura za maoni za  WMUR/UNH zinaonesha jimbo la New Hampshire ni jeupe kwa Clinton ambaye hadi sasa anaongoza kwa asilimia 15 katika jimbo hilo.

Pia Trump atatakiwa kushinda majimbo yasiyotabirika. Upo uwezekano Trump kushinda kama atafanya vema katika majimbo yasiyotabirika japo si rahisi. Kama itatokea basi itampa ahueni kufikia ushindi wa urais. Ushindi katika majimbo ambayo haitarajiwi Trump kushinda kunaweza pia kumnyanyua na hivyo kuongeza fasili ya ushindi wa miujiza. Kura za maoni za hivi karibuni zinaonesha majimbo ambayo yanaangukia Democrats kama Wisconsin, Virginia, Michigan na Colorado yataangukia kwa Clinton. Pia Trump hajaonekana kutumia muda wake pamoja na matangazo katika majimbo haya.

Suala lingine ni la kutumia karata yake ya mwisho katika kuyasaka majimbo yafuatayo: 1) Ashinde Wisconsin, Maine, pamoja na jimbo moja kati ya Nevada au Iowa 2) Ashinde majimbo ya Virginiana ama Nevada au Iowa au New Hampshire 3) Ashinde majimbo ya  Michigan na  Maine na pia 4) Ashinde majimbo ya Colorado, Iowa na ama Nevada au New Hampshire.