Home Makala TRUMP  ATAZIBUA MITARO MICHAFU TANZANIA?

TRUMP  ATAZIBUA MITARO MICHAFU TANZANIA?

640
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA


DONALD Trump anatarajiwa kuapishwa Januari 20 mwaka huu. Trump amepata mashabiki wengi hapa nchini. Baadhi yao wanaamini atatekeleza mambo mengi aliyoahidi wakati wa kampeni za kuwania urais wa Marekani.

Matumaini ya baadhi ya watanzania wenzetu yamevuka mipaka kiasi kwamba wanajiwekea kiwango cha juu cha hisia za kumpenda kana kwamba walikuwa sehemu ya wapigakura wake.

Kwamba watanzania wenzetu wamehamaishia mahaba kwa Trump ikiwa ni njia ya kutimiza matamanio yao.  Ni matamanio hayo wengi wanaamini kuwa Trump atatekeleza mambo yake ikiwemo hata kuzibua mitaro ya kutiririsha maji machafu kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

Chukulia mfano jiji la Dar es salaam, mvua zinaponyesha kunakuwa na vurumai nyingi mno.  Mfumo wa utiririshaji maji taka nao umekuwa wa hovyo kiasi kwamba harufu kali inaweza kuleta matatizo katika afya za wakazi wake.

Si hilo tu, maeneo mengi yaliyoko hapa nchini yanakabiliwa na changamoto ya kutiririsha maji. Aidha, kumekuwa na mfumo mbovu wa ukusanyaji wa takataka katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Miji mingi inekuwa imekuwa ikisongwa na uchafu unaotupwa hovyo na wakazi wao. Licha ya uchafu huo kumekuwa na kampeni kadhaa zinazopewa tenda ya kuzoa takataka na kuhakikisha miji inakuwa safi.

Lakini  kumekuwa na changamoto kubwa sana ya kusafisha miji yetu. Viongozi wa  vitongoji, vijiji, kata, tarafa, wilaya, mikoa, kanda hadi taifa wamefeli kutatua suala hilo. Wananchi nao wamezidisha kasi ya utupaji takataka bila kujali maeneo husika kama yanastahili au la.

Katika muktadha huo wapo watu wanalalamika suala hilo kwa uongozi. Wengine wamefika mahali kuamini kuwa viongozi wao hawana uwezo tena wa kuzoea takataka hizo.

Kwa hiyo kinachofanyika ni kujizoesha lawama huku tukizidisha kasi ya kutupa takataka hovyo. Swali moja ambalo tunatakiwa kujiuliza, ni nani atakuwa na wajibu wa kusimamia masuala yetu katika nchi?

Ni kwa namna gani wananchi na viongozi tunashirikiana katika kusafisha mazingira? Pamoja na juhudi za taasisi binafsi kutumia wafanyakazi wao kusafisha mazingira kama njia ya kuhimiza usafi, bado juhudi hizo zimekuwa chache mno kiasi kwamba kasi ya utupaji wa takataka na usafi havilingani.

Kuna baadhi ya miji kama Dar es salaam wapo wakazi ambao wanadhani suala la kusafisha mitaro inayopita kwenye nyumba zao na kusababisha harufu mbaya na kali yenye madhara kwa afya zao ni hadi afike kiongozi wa kitaifa.

Ni katika dhana hiyo wapo watanzania wanaamini mitaro michafu iliyopo mitaani itasafishwa na Donald Trump. Kwa sababu tangu mwanzo wa kampeni zake huko Marekani, Trump alionyesha kukerwa na mambo mbalimbali yanayofanyika barani humu.

Licha ya kwamba ugomvi wake ulikuwa ni dhidi ya Nigeria na Kenya, lakini ilijumuishwa waafrika wengi wapo hivyo. Tunalea uchafu, uzembe, ubadhirifu, uhaba wa nidhamu ya muda, uongozi mbovu na kadhalika.

Tukitathimini masuala hayo tunajikuta tunaulizana hapa, ni mambo gani yanaashiria kuwa sisi kama watanzania na waafrika tunaenenda katika kanuni sahihi?

Mantiki inasema kuwa suala la usafi ni miongoni mwa ishara ya uongozi bora kuanzia ngazi ya familia na kwenda juu.

Kama tunashindwa kuhakikisha mambo hayo yanafanyika ni kwanini tuendelee kuwabebesha mizigo watawala ambao wanatokana na jamii zetu huku wakifahamu kuwa tumekuwa wavivu, wazembe, kutojali na kila mtu anakwepa majukumu.

Kuendelea kumfikiria Trump kama mtu mwenye kuleta matumaini ni kusimika mizizi ya utumwa wa akili. Tunajijengea mazoea mabaya ya kukwepa majukumu yetu ikiwemo kuhakikisha wanajamii tunashiriki kusafisha mazingira yetu.

Jambo la pili kuhusu ujio wa Trump ni suala la kuwatimua madarakani viongozi wanaotajwa kuwa hawafai ama wanatafsiriwa kuwa madikteta.

Wapo watanzania wanaamini kwamba Trump atamwondoa madarakani Robert Mugabe  wa Zimbabwe.  Kwamba atamwondoa madarakani Yoweri Museveni  wa Uganda.

Vilevile wanaamini wamba Trump atamwondoa madarakani Paul Kagame wa Rwanda, na kuhakikisha bara la Afrika linatawaliwa tena na ukoloni wa Kimarekani.

Aidha, wanaamini kuwa  atamwondoa madarakani Rais Omar al Bashir wa Sudan. Na wengine wanashadidia kuwa atamtimua mamlakani Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Pierre Nkurunziza wa Burundi.

Aidha, wanaamini kwamba atawarudisha nyumbani raia wa Nigeria na Kenya walioko Marekani. Binafsi ninaona hayo ni matumaini hewa kama ilivyo suala la kushindwa kwetu kulinda mazingira.

Tumeshindwa kuyafanya amzingira kuwa rafiki. Tumekata miti, tumeharibu vyanzo vya maji. Hatutaki kusafisha vitongoji vyetu na sasa tunamtegemea Donald Trump aje kuzibua mitaro michafu huko mitaani ili tuishi kwa raha mustarehe.

Hivi ni vituko na dalili ya jamii isiyopenda kusimamia mambo yake. Tunatakiwa kujielimisha mimi na wewe ili tukubaliane kuwa mazingira yetu yanatusaidia kuepukana na magonjwa sambamba na matatizo mengine.

Inatakiwa tuone aibu kumtegemea mpiga kura Chicago, Iowa, California, Texas, na kwingineko Marekani eti atuwezeshe kutuletea kiongozi wa kuzibua mitaro yetu mitaani.  Tuone soni.