Home Makala Kimataifa TRUMP BADO HANA KIPAUMBELE KUHUSU AFRIKA

TRUMP BADO HANA KIPAUMBELE KUHUSU AFRIKA

3382
0
SHARE

WASHINGTON, MAREKANI


Yanapokuja masuala ya Afrika, isitegemewe sana tija yoyote kutokana na mabadiliko yaliyotokea Wizara ya Nje ya Marekani kwani Ikulu ya Marekani haitilii maanani sana masuala ya Afrika.

Utawala wa Rais Donald Trump haujatoa kipaumbele kwa Afrika na ikulu ya nchi hiyo imeshindwa kuweka malengo yake halisi au kuanzisha sera yoyote mpya kuhusu Bara hili.

Hivyo basi uteuzi wa mapema mwezi huu wa Michael Pompeo kumrithi Rex Tillerson kama Waziri wa Mambo ya Nje hautabadili chochote katika mtazamo wa Trump kwa Afrika.

Sana sana, mabadiliko haya yatatia nguvu mtazamo wa Marekani katika masuala ya usalama na vita dhidi ya ugaidi, na mkazo huu utaishia kuzirudisha nyuma zaidi sera za Marekani kwa Bara la Afrika.

Hali inaweza kuifanya Marekani kuwa upande wa zile tawala za Afrika za kidikteta na za kifisadi. Hali hii pia inaweza kuunasa utawala wa Washington katika migogoro iliyopo ya muda mrefu ambayo haiwezi kupata ushindi kwa njia ya vita pekee. Aidha itaathiri sana ushawishi na hadhi ya Marekani katika Bara la Afrika.

Kuondolewa ghafla kwa Tillerson wakati akiwa ziarani katika nchi tano za Afrika haikuwa habari nzuri. Ingawa kuondolewa kwake haukukutokana na masuala ya Bara la Afrika, lakini alikuwa ni afisa pekee aliyeonyesha ari ya kushughulikia masuala ya Afrika.

Hata sasa hivi nyadhifa muhimu za kuhusu Afrika katika Wizara ya Nje ya Marekani bado hazijajazwa tangu uondoke itawala wa barack Obama.

Uteuzi wa Pompeo kumrithi Tillerson huenda ikawa habari mbaya kwa wale wanaotaka kuona Marekani inazidisha mahusiano yake na Afrika katika changamoto mabali mbali kama vile za kiuchumi, afya, na biashara.

Na kwa upande mwingine labda ni habari njema kwa wote wale wanaoamini kwamba kipaumbele cha Marekani kwa Afrika kiwe ni kuongeza ushirikiano katika mapambano ya matishio dhidi ya Somalia, Sahel (maeneo ya Mali na Nigeria) na sehemu nyingine.

Pompeo mwenye msimamo mkali hadi sasa ametoa kauli kiduchu tu kuhusu Afrika na kauli hizo zilihusu Libya na vita dhidi ya ugaidi.

Akiwa pia ni Mjumbe wa kamati ya Intelligensia katika Baraza la Wawakilishi (House of Representatives Intelligence Committee), alikuwa mpinzani mkubwa wa waziri wa zamani wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bi Hillary Clinton kuhusu lile sakata la kushambuliwa kwa ubalozi mdogo wa Marekani katika mji wa Benghazi, Libya kulikosababisha kuawa kwa Balozi Chris Stevens.

Ingawa amekuwa akiunga mkono utolewaji wa misaada ya chakula kwa nchi zenye mahitaji, kipaumbele chake cha kwanza kinatazamiwa kuwa uimarishaji wa usalama wa Bara la Afrika kwa kushirikiana na nchi zinazochangia vikosi vya kulinda amani chini ya Umoja wa Afrika (AU).