Home Latest News TRUMP HATAIWEZA CHINA KIUCHUMI NA BIASHARA DUNIANI

TRUMP HATAIWEZA CHINA KIUCHUMI NA BIASHARA DUNIANI

1142
0
SHARE
Rais wa marekani Donald Trump

NA HILAL K SUED,

Marekani ya Rais Donald Trump haiwezi kuishi katika ombwe. Ni lazima nchi nyingine zinapiga hesabu na kujiweka sawa kuvuna kwa ujio wake.

Tayari mengi yamezungumzwa kuhusu Russia. Lakini hata hivyo nchi kubwa yenye nguvu inayoshindana na Marekani kwa uongozi katika maeneo ya Bara la Asia na Bahari ya Pacific na kujaribu kuweka mamlaka duniani kote ni China.

Hata hivyo utawala wa Beijing umeamua kwamba Trump ameleta nafasi kubwa kwa China katika kupata nguvu na ushawishi mkubwa kwa ‘hisani’ ya Marekani yenyewe.

Kwa mfano tayari katika mwaka huu tu Rais wa China, Xi Jinping ametoa hotuba mbili muhimu zikiilenga dunia kwa upana wake. Ameshaweka, kimakusudi kabisa na bayana, tofauti kati yake na Trump.

Trump alianza mwaka mpya kwa andiko katika ukurasa wake wa Twitter akisema: “Heri ya mwaka mpya, pamoja na maadui zangu na wale waliopambana nami na kushindwa vibaya sana na hata hawajui wafanye nini sasa. Nawapendeni nyote.”

Rais Xi alitoa hotuba yake ya Mwaka Mpya kwa taifa lake kupitia televisheni, hotuba ambayo ilitafsiriwa katika lugha 65. Hotuba hii ilikuwa ni ishara chanya ya kuhamasisha kuchukua hatua.

Mandhari ya Trump ni kudorora kwa Marekani, mandhari ya Xi ni mafanikio ya China. Xi amejigamba, kwa mfano, kwamba nchi yake imeendelea kukuza uchumi wake na kuwa wa kwanza duniani.

Na kuhusu kampeni yake dhidi ya ufisadi Xi alisema itakuwa ni “bila huruma kupambana na ‘mapapa’ na ’vidagaa’ wa ufisadi, vigogo na watu wa chini, ili kuusafisha kabisa mfumo wetu wa utawala na wa kisiasa.”

Xi aliorodhesha mafanikio yake katika medani ya sayansi yaliyopatikana mwaka uliopita. Kwa mfano, China imemaliza kujenga darubini (radio telescope) kubwa zaidi duniani, yenye upana wa nusu kilomita; ilirusha angani satelaiti ya kwanza ya aina ya ‘quantum’ yenye lengo la kuweka, kwa mara ya kwanza, mawasilianio yasiyoweza kudukuliwa, na mengineyo.

Na katika ahadi yake ya kuleta maendeleo hakumaananisha hiyo itakuwa kwa wananchi wake tu, bali kwa watu wa dunia nzima. Alisema: “Siku zote watu wa China wamekuwa wakiamini kwamba dunia ni jumuiya moja.

“Sisi Wachina siyo tu kwamba tunapigania maisha bora kwa watu wetu, lakini pia watu wa sehemu nyingine duniani nao waishi maisha mazuri.”

Miongoni mwa misaada ya China kwa mataifa mengine ni ule ushiriki katika mpango wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” – kama vile ile ya zamani Njia ya Hariri (Silk Road).

Njia hii ni kuunganisha Bara la Asia na la Ulaya si kwa nchi kavu tu, bali pia kwa njia ya bahari. Mpango huu unatazamiwa kugharimu matrilioni ya dola za Kimarekani katika kuendeleza miundombinu katika uwekezaji utakaoshirikisha nchi zaidi ya 60. Hii ilikuwa kama ‘saini’ ya Rais Xi na ndiyo maana alihakikisha kuitaja katika hotuba yake.

Baada ya hotuba yake hiyo alisafiri hadi mji wa Davos, Uswisi ambako ‘makasisi’ wakuu wa Utandawazi hukutana kila mwaka kuzungumzia masuala ya uchumi wa dunia.

Ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 45 ya World Economic Forum (WEF) kwa rais wa China kuhudhuria mkutano huo. Lakini Trump hakuwepo, alikuwa bado hajaapishwa. Gazeti la Guardian la Uingereza, likitoa nukuu kutoka tamthiliya moja ya William Shakespeare liliandika: “Ilikuwa kama Hamlet bila ya ya kuwepo mwanamfalme.”

Wakati anamtambulisha Xi Jinping mkutanoni, muasisi na Mwenyekiti wa WEF Klaus Schwab alisema: “Dunia nzima inaitazama China.”

Na kiongozi huyo wa China hakuwavunja moyo. Swakati Marekani ya Trump ikiahidi kuweka vikwazo vikali vya kibiashara, Xi Jinping aliziambia nchi za dunia kwamba China itaacha milango yake wazi kabisa ya biashara.

Na katika kuielezea zaidi hotuba yake, maafisa wa utawala wako huko Beijing walitangaza hatua mpya za kufungua milango ya China kwa uwekezaji kutoka nje katika sekta za huduma na teknolojia.

Hata hivyo mapoema wiki hii Trump kasha tangaza nchi yake kujitoa kutoka mkataba wa ushirikiano kibiashara na nchi za eneo la Bahari ya Pacific (Trans-Pacific Partnership – TPP), mkataba ulitiwa sahihi Februari mwaka jana na nchi 12 ambazo kwa pamoja zinazalisha uchumi wa asilimia 40 duniani.

Hata hivyo Xi Jinping alikuwa tayari kaliongelea hilo kwa kusema nchi yake kwa bidii itahakikisha ufunguaji milango kwa lengo la maendeleo ya kipamoja.

Jinsi Marekani inavyozidi kujitazama ndani kwake, na ndivyo China inavyozidi kutazama nje kwake.

Waziri Mkuu wa zamani wa Sweden carl Bildt alisema kwamba kuna ombwe katika uongozi wa kiuchumi duniani na kwamba Xi analenga kulijaza ombwe hilo, kwa mafanikio hadi sasa.