Home Makala TUACHE MANENO, WATU HAWA WASHUGHULIKIWE

TUACHE MANENO, WATU HAWA WASHUGHULIKIWE

5086
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Kwa mara nyingine tena ni habari zile zile kuhusu takriban watu wale wale – wakubwa katika nyadhifa zile zile kutoka utawala ule ule. Haiwezekani wakawa watu wengine.

Na iwapo serikali itafanya uchunguzi wa kimya kimya miongoni mwa wananchi wa kawaida kujua wanasema nini kuhusu masuala haya yanayojirudia mara kwa mara kwa staili ile ile, itagundua kwamba wananchi wengi wamechoka kusikia habari zile zile huku hakuna hatua zozote za maana zinazochukuliwa dhidi ya wahusika, mbali na kuwatajataja tu.

Jumamosi iliyopita wananchi walipatiwa toleo jingine kuhusu kile kile ambacho wamekuwa wakiambiwa mara kwa mara, kwamba mikataba ambayo serikali hii imetiliana na makampuni ya nje ya uchimbaji madini na gesi asilia ni mibovu kiasi kwamba nchi imekuwa ikipunjwa na inaendelea kupunjwa mapato yake stahiki. Safari hii kumeongezwa na mikataba ya uvuvi katika maeneo yetu ya bahari.

Aidha ni sahihi kabisa hapa kusema kwamba suala la usimamiaji mbovu wa maliasili zetu kutokana na mikataba mibovu ya uchimbaji madini, mingine ikisainiwa katika vyumba vya hoteli mjini London, lilianza kupigiwa kelele na wapinzani zaidi ya muongo mmoja uliopita, lakini walipuuzwa, kwa sababu tu ni wapinzani wasiopaswa kulizungumza, achilia mbali kusikilizwa.

Lakini ilifika mahala ambapo serikali yenyewe iliona ianze kuchukua hatua – angalau katika kuonyesha tu kwamba ni yenyewe ndiyo imegundua madudu yote hayo na ndiyo inayopasa kuyasemea. Inaona haidhuru wananchi waipongeze kwa hilo (kuyagundua na kuyasemea) – kwani hatua stahiki zinazotakiwa kufuatwa ni mtihani mzito, ni kigugumizi – pamoja na kuahidiwa msaada, wakati fulani katika suala moja husika, kutoka mamlaka moja ya nje – kama nitakavyoeleza.

Mwaka 2012 habari zilivuja kutoka mamlaka za kibenki huko Uswisi kwamba baina ya Watanzania walioficha mabilioni katika mabenki ya nchi hiyo, wamo pia vigogo kadha wa serikali ya CCM. Ilidaiwa akaunti hizo zilifunguliwa na makampuni yanayojishughulisha na utafutaji/uchimbaji wa madini na gesi asilia kwa niaba ya baadhi ya Watanzania hao – kwa maneno mengine ni hela za milungula.

Hata hivyo hakuna majina yaliyotajwa. Lakini hata mtoto mdogo anaweza kuunganisha doti hapa – walioikosesha serikali mabilioni ya mapato kutokana na usimamizi mbovu wa maliasili zetu ni kina nani.

Namna ya suala hili (lililopachikwa jina la “Mabilioni ya Uswisi” lilivyopokelewa na ‘kushughulikiwa’ na serikali ilitoa picha kwamba haikuwa na nia ya dhati ya kulishughulikia na lilionekana kama vile ilikuwa limeiumbua. Ni kweli ilisema italifuatilia suala hilo lakini ilikuwa inafanya ionekane inafanya hivyo (Kiiengereza “going through the motions.”)

Julai 2014 gazeti moja hapa nchini liliandika kwamba serikali yetu ilipuuza kufuata ushauri kutoka kwa Jaji mmoja wa Ufaransa, Renaud Van Ruymbeke kuhusu hatua za kufuata ili iweze kubaini orodha ya Watanzania, wakiwemo viongozi wa juu wa serikali walioficha mabilioni ya fedha katika akaunti hizo za Uswisi.

Jaji huyo anasifika katika masuala hayo kutokana na jinsi alivyoweza kubaini akaunti za Wafaransa walioficha fedha nje ya nchi hiyo kinyume na sheria na utaratibu na hatimaye wahalifu hao kufunguliwa mashitaka.

Jaji huyo anayeheshimika katika ufuatiliaji wa fedha zinazofichwa na watawala kutoka nchi mbali mbali hasa zile zinazoendelea aliipa tipu serikali ya Tanzania kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Mahesabu ya Serikali (PAC) kwamba anazo data zote kuhusu Watanzania walioficha fedha hizo.

Hata hivyo aliweka sharti kwanza serikali ya Tanzania ipeleke maombi rasmi kwa Wizara ya Sheria ya Ufaransa, na baadaye kikosi kazi cha Wizara hiyo chini ya Jaji huyo mara moja kitafuatilia na kutoa taarifa zinazohitajika.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali wakati ule Frederick Werema (ambaye kama itakumbukwa alijiuzulu kutokana na kashfa ya Escrow) alinukuliwa na Shirika la habari la Uingereza Reuters akisema eti serikali yake bado inalifuatilia suala la urejeshwaji wa fedha hizo kupitia taasisi moja binafsi iitwayo ISCAR iliyopo Basel nchini Uswisi ambayo hufanya kazi za aina hiyo kwa gharama (kamisheni) kubwa sana kwa serikali.

Hadi sasa hatujapata mrejesho kuhusu suala la akaunti za Uswisi, na haijaelezwa iwapo serikali hii ya Awamu ya Tano ililirithi suala hilo kwa lengo la kuliendeleza na kulifikisha mwisho wake – na hatua stahiki kuchukuliwa kwa wahusika.

Twende: Ripoti ya makinikia na ile ya madini ya almasi na tanzanite zote zilitaja kwamba wakubwa kadha walihusika katika usimamizi mbovu wa maliasili zetu na hivyo kuinyima serikali mapato kwa mabilioni. ‘Taja-taja’ hii bila hatua za kisheria inatokana na ukweli mmoja ambao nimekuwa nikiusema mara kwa mara katika safu hii – kulindana kulikokithiri kwa wakubwa ndani ya utawala.

Wahusika ni majina makubwa katika serikali na/au chama tawala (CCM) na iwapo serikali itaanza kuwasimamisha wakubwa hao vizimbani, basi kesi hizo zinaweza kuchukua mkondo usiotabirika na majina makubwa zaidi kuibuka. Ni staili ya “funika kombe mwanaharashi apite.”

Wahusika ambao baadhi yao wamekuwa wakitajwa na wengine majina yao yanarudiwa rudiwa katika kila kashfa mpya ya usimamizi mbovu wa maliasili inayoibuliwa bado wanadunda mitaani na kupumua, kitu kinachochangiwa na sheria mbovu na usimamizi dhaifu wa taasisi zinazosimamia uchunguzi wa masuala haya.

Hawa wanakuwa wepesi zaidi kufuatilia jinai zinazodaiwa kufanywa na viongozi wa upinzani kuliko jinai kuhusu upotevu wa mabilioni kupitia usimamizi mbovu wa maliasili za taifa.

Hapo juu nimesema huenda kinachosababisha kigugumizi katika kuchangamkia uhusika wa wakubwa wanaotajwa na kuwasimimamisha kizimbani ni hofu ya vigogo wa ngazi za juu zaidi kubainika kuhusika. Kuna hoja inayoweza ikatolewa katika utetezi – kama vile “nilipata maagizo kutoka juu” na hata kuonyesha ushahidi wa hilo kimaandishi.

Kisheria hii haiwezi ikawa kinga. Katika utendaji kazi katika serikali kuna ‘wajibu wa pamoja’ (collective responsibility) lakini pia kuna ‘uwajibikaji wa mmoja mmoja’ (individual accountability.)

Katika issue ya Kashfa ya Watergate iliyomkumba rais wa 35 wa Marekani Richard Nixon miaka ya 1970 baadhi ya maafisa na wapambe wa rais huyo walipatikana na hatia ya uhusika wao na kuhukumiwa vifungo gerezani, pamoja na kujitetea kwamba walikuwa wanafuata maagizo kutoka juu.

Hali kadhalika, mara tu baada ya Vita ya Pili ya Dunia katika kesi zilizofanyika Nuremberg, Ujerumani dhidi ya majenerali wa Dikteta Adolf Hitler, utetezi kama huo ulikataliwa na majaji, na majenerali hao walihukumiwa vifo.