Home Makala Tuendelee kumuenzi Baba wa taifa kwa vitendo

Tuendelee kumuenzi Baba wa taifa kwa vitendo

454
0
SHARE

NA SABINA WANDIBA


WATANZANIA kote nchini jana waliadhimika kumbukumbu ya miaka 21 ya kifo cha muasisi wa taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere huku wakiwa katika harakati za lala salama ya kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Maaadhimisho hayo hufanyika Oktoba 14 ya kila mwaka ambapo taifa hufanya shughuli mbalimbali kwa ajili ya kumuenzi muasisi huyo na kuangalia mwelekeo wa taifa tangu kuondokewa kwake.

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika kijiji cha Mwintongo Butiama, Wilaya ya Musoma, Mkoani Mara.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia nchini Uingereza alikokuwa amelazwa baada ya kusumbuliwa na maradhi ya saratani ya damu akiwa na miaka 77.

Baba yake mzazi alikuwa Nyerere Burito (1860 -1942), chifu wa kabila la Wazanaki, anafahamika zaidi kwa jina la Mwalimu kutokana na taaluma yake ya zamani kabla ya kujiunga na harakati za ukombozi.

Nyerere alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda na pia katika Chuo Kikuu cha Edinburg cha nchini Uingereza.

Mwalimu Nyerere alisaidia kuunda chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na Tanganyika ilipopewa serikali mwaka 1960, Nyerere alikuwa Waziri Kiongozi na aliiongoza nchi kwenye uhuru wake mwaka moja baadaye na kuwa waziri.

Julius Kambarage Nyerere alikuwa kiongozi wa Kitanzania aliyeiongoza Tanzania na kabla ya hapo Tanganyika, kuanzia mwaka 1960 hadi alipostaafu mwaka 1985 na anatambuliwa kuwa ndiye Baba wa Taifa sifa ambayo inaendelea kudumishwa vizazi hadi vizazi. 

Katika kuadhimisha miaka 21 tangu kifo chake, kwa siku nzima jana, vyombo mbalimbali vya habari kama vile vituo vya televisheni, redio vimekuwa vikipeperusha ujumbe wa sehemu za hotuba za Mwalimu Nyerere alizozitoa wakati wa kupigania uhuru, akiwa madarakani na baada ya kung’atuka kwenye uongozi.

Aidha, wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, waliungana kumkumbuka muasisi wa taifa la  Tanzania kwa kufanya majadiliano kwa kushiriki makongamano ya mbalimbali, kuendesha mijadala kupitia vyombo vya  habari na kushiriki majadiliano yasiyo rasmi kupitia majukwaa kama vile mitandao ya kijamii pamoja na kuendesha mashindano ya michezo kwa ajili ya maadhimisho hayo.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, anapaswa kukumbukwa na kuenziwa kwa vitendo kutokana na uhodari wake katika uongozi.

Wanasema kuwa, wakati Watanzania wakiwa kwenye kumbukizi ya miaka 21 ya kifo chake, kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka kwake na ni vyema tukatumia busara za Mwalimu Nyerere katika kipindi hiki cha kampeni za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka huu.

Rais Dk. John Magufuli alizungumza katika mkutano wa kampeni wa CCM katika Uwanja wa Barafu Mburahati jijini Dar es Salaam juzi kuwa, Baba wa taifa Mwalimu Nyerere, alikazania kwa nguvu zake zote na kuliongoza taifa hadi likapata uhuru.

“Wakati tunamkumbuka baba wa Taifa kutimiza miaka 21 tangu kifo chake, ni lazima tukumbuke kuwa, Nyerere  aliondoa ukabili, udini na hatukubaguana kabisa kwa hali yoyote si kwa ukabila wala udini, tuusimamie upendo huu wa muasisi wetu udumu.

“Katika Afrika tukichukua nchi kumi ambazo uchumi wake unakuwa, Tanzania tumo na ndio maana miradi mingi tunaitekeleza sisi wenyewe kwa fedha zetu,”alisema.

Mwalimu Nyerere ni moja ya viongozi wachache wa Afrika waliokuwa na ndoto ya kutaka kuinganisha Afrika kuwa kitu kimoja pia alikuwa mkali kwa chama alichokiasisi CCM na kwa viongozi wa serikali.

Mbali ya kuwa mstari wa mbele katika kupigania ukumbozi wa Kusini mwa Afrika, Mwalimu Nyerere pia alikuwa msemaji mkubwa wa nchi za dunia ya tatu akipigania usawa na haki za kiuchumi.

Katika makongamano mengi yaliyofanyika, wazungumzaji wamekuwa wakimtaja Mwalimu Nyerere kama kiongozi aliyedhubutu, mpenda watu mwadilifu na aliyependa kuheshimu utawala wa sheria.

Rais wa awamu ya nne,  Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kuzungumza kwenye kongamano moja na kumtaja Mwalimu Nyerere kama mtu muungwana aliyejawa na ubinadamu na kwa maana hiyo aliwasihi wanaotaka kumuenzi kwa vitendo basi wasiwe viongozi wa kujimwambafai akimaanisha kufanya mambo katika hali ya umwamba.

Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo wa kuona mbali, hata alipopingwa baadaye waliompinga walikiri ukweli wa maono yake.

Ni dhahiri kwamba Mwalimu Nyerere anakumbukwa kwa mambo mengi ya msingi aliyoyapa kipaumbele wakati wa uongozi wake, jambo mojawapo alilolisema Julai 29, 1985 ni kwamba.

Nanukuu,  “Kazi iliyokuwa muhimu kuliko zote kwangu mimi , ilikuwa ni kujenga Taifa lenye  umoja kwa msingi  wa  heshima  na usawa  wa Binadamu.”

Moja ya mambo muhimu Mwalimu Nyerere aliwahi kuyaandika na kuyapigania ni Azimio la Arusha mwaka 1967 ambapo moja ya azimio muhimu katika andiko lake.

Ni ujinga kutegemea pesa kama chombo cha maendeleo wakati tunafahamu vyema kwamba nchi yetu ni masikini, lakini ni ujinga zaidi kufikiria kwamba tutajikomboa kutoka kwenye umasikini wetu kwa kutegemea misaada ya kigeni badala ya juhudi zetu wenyewe,”alisema katika azimio hilo.

Tanganyika iligeuka na kuwa Jamhuri mwaka 1962 na Nyerere akawa rais wake wa kwanza pia mwaka 1964, Tanganyika iliungana kisiasa na Zanzibar na kuzaa Jamhuri ya Tanzania, ambako Nyerere aliendelea kuwa rais hadi alipon’gatuka mwaka 1985.

Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbainiana kilichopo mjini Roma nchi Italia, hivi karibuni kilimtafakari Mwalimu Nyerere kuwa fikra na mchango wake katika Jumuiya ya Kimataifa.

Katika hotuba iliyotolewa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, George Madafa ilibainisha kwamba, maisha, fikra na mawazo ya Mwalimu Nyerere yamefumbatwa na uadilifu, bidii, usawa, mshikamano na uvumilivu usio na kipimo.

Kama mtumishi wa serikali ya Tanzania, utendaji kazi wa Mwalimu Nyerere ulisadifu kwa dhati fadhila na tunu, msingi wa maisha na tunu za maisha ya kikristo yaani, imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na kwa unyenyekevu uliotukuka kwa watu aliowatumikia.

Ni vyema kwa viongozi walioko madarakani na wale wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi wananchi, kuwa wazalendo na kumuenzi hayati baba wa taifa kwa vitendo katika kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zinawanufaisha watanzania badala ya watu wachache.

Lakini pia wanapaswa kudumisha amani ya nchi kuepuka kuwagawa watanzania katika matabaka sambamba na kuepuka ukabila na udini hapa nchini.