Home Makala TUIGEUZE KOREA KASKAZINI KUWA DARASA LA MFANO

TUIGEUZE KOREA KASKAZINI KUWA DARASA LA MFANO

650
0
SHARE
Rais John Magufuli akikagua gwaride

NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA


APRIL 15 kila mwaka ni siku muhimu sana kwa Taifa dogo la Korea ya Kaskazini eneo ambalo lipo katika rasi ya Korea Mashariki ya mbali kwani ndiyo siku alipozaliwa mwasisi wa taifa hilo Kim Sung II.

Kiongozi huyo alizaliwa mwaka 1912 mwaka ule ambao meli kubwa ya kifahari Titanic ilipozama wakati ilipokuwa katika safari yake ya kwanza na nchini humo siku hiyo wanaita the day of the Sun.

Kupitia taarifa mbalimbali tulishuhudia nchi hiyo ikijipapatua kuonyesha zana zake kali na mpya za kijeshi ambazo ama walizitengeneza wao au walishirikiana na maswahiba wao Urusi na China kwa kunakili teknolojia nakadhalika.

Onyesho hilo lilikuwa ujumbe kwa ulimwengu kwamba yeyote atakayejaribu kuichezea nchi hiyo ndogo kwa eneo atakiona cha mtema kuni na hasahasa taifa la Marekani ambalo limekuwa adui mkubwa wa taifa hilo la Kikomunisti .

Yalikuwa maonyesho yaliyofana sana kuanzia makomandoo wale waliokuwa wakivunja mawe kwa vichwa, kukunja nondo, kurusha midege yao ya kisasa kabisa yenye marubani na isiyo nayo, ukakamavu wa askari wa miguu, mbwa, na farasi nao wakiwemo  huku kiongozi wao kijana barubaru Kim Jong-un akifuatilia tukio hilo huku usoni mwake akivaa tabasamu bandia.

Siku tisa baadaye yaani jana,Tanzania iliadhimisha miaka 53 ya Muungano wa nchi mbili,Tanganyika na Zanzibar japo viongozi hasa wa upande mmoja wanaona haya kuitaja nchi yao kwa jina lake na badala yake wanajibaraguza kwa kuita Tanzania bara, eneo ambalo halipo popote katika ramani ya dunia.

Jana katika uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma tulishuhudia onyesho la Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania, kama moja kati ya matukio ya kuadhimisha siku hii muhimu kwa taifa,  tuliona gwaride la ukakamavu mbele ya viongozi wakiongozwa na Amiri Jeshi Mkuu Rais John Magufuli, tulishuhudia zana tulizonazo  na mengineyo mengi.

Kama raia mzalendo napongeza Jeshi letu kwa kuendelea kuwa chombo cha wananchi kama ambavyo jina lake linajidhihirisha.Kazi kubwa ya Jeshi  letu ni kulinda mipaka yetu wakati wote bila kujali kuna adui anatutisha au laa.

Isipokuwa kwa wakati huu ambao ulimwengu na teknolojia zinakwenda kwa kasi sana, na nchi yetu iko katika mageuzi na kutaka kuwa nchi yenye viwanda na uchumi wa kati, badala ya kufanya kama Korea ya Kaskazini ambayo imeshajua adui yake, sisi tungefanya tofauti kidogo.

Sisi hatuna hasa adui aliyejitokeza waziwazi kiasi cha kuonyesha zana zetu chache ambazo kwanza hatutengenezi wenyewe, hakuna sababu ya wale makomandoo wetu kujulikana kwa maonyesho yao ambayo mengine yanaweza kuzusha maswali juu ya uwezo wao pale wanapokutana na adui wa kweli wa taifa letu.

Mimi na wananchi wenzangu ambao hatujazoea maigizo na mazoezi ya namna ile tunaweza kutishika, lakini ikiwa kila mara tutaonyesha mbinu zetu kidogo tuliyonayo hatuoni ni hatari sawasawa na kuuza ramani ya vita?

Badala ya kutisha raia walio kwenye nchi ambayo tunasema ni kisiwa cha amani kwa kurusha midege angani, vifaru ardhini, gwaride la vikosi vyote, utunishaji wa misuli, unyumbulishaji wa miili na kadhalika kwanini tusiwe na maonyesho ya ubunifu yaliyofanywa na jeshi letu katika teknolojia?

Kulikuwa na kiwanda cha Jeshi kilichokuwa kikitengeneza magari na mitambo, siku kama ya jana ilitakiwa badala ya Amiri Jeshi Mkuu kwenda uwanjani kuangalia zana zilizonunuliwa ilipaswa akague zana tunazotengeneza wenyewe! Vyombo vyote vya habari vingeonyesha mitambo ya ‘nyuklia’ walau inayoweza kutifua kichuguu kwa kuanzia.

Tunao vijana ambao akili zao zinachemka hasa kwenye Tehama, wengine ni ndugu na marafiki zetu wako huko jeshini hawa wangebuni namna ambavyo tunaweza kuwakamta wahuni wanaoteka na kutesa wananchi, au majambazi waliovamia Askari wetu huko Kibiti Mkoa wa Pwani.

Kama ambavyo siku zote Rais wetu Dk. John Magufuli anatueleza kuhusu dhamira ya kuigeuza nchi yetu kuwa taifa lenye uchumi imara unaotegemea uzalishaji viwandani, ndio ulikuwa wakati hasa wa kutumia Jeshi letu kimkakati likishirikiana na wasomi na wabunifu wengine ili kufanikisha hilo badala ya kuyafanya maonyesho haya kama uwanja wa kuzodoa wale ambao hatukubaliana nao kiitikadi.

Nimesema hapo juu tulikuwa na Nyumbu pale Kibaha, na nchi yetu ili ifanikiwe katika mapinduzi ya viwanda ni lazima suala hilo liende sambamba na kilimo. Hatuwezi kufanikiwa katika kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa taifa letu kama hatuwezi kuwa na viwanda vya zana za kiimo.

Badala ya kutegemea jembe la mkono kifaa kilichotumika kwa karne mbili zilizopita, wapo wasomi na wabunifu wengine ambao wanaweza kushirikiana na askari wetu kutengeneza zana hizo. Tunahitaji matrekta kwa ajili ya kilimo, watengeneze kwa kuanzia linalorudi nyuma kama alivyowahi kushauri Mwasisi wa Taifa hili na Amiri Jeshi wa Kwanza wa Majeshi Julius Nyerere.

Kuwe na kiwanda ambacho humo zitapatikana zana zote kuanzia matrekta, pampu za kumwagilia, madawa ya kilimo, mbegu, mbolea, nakadhalika. Inawezekana, juzi jeshi la Rwanda lilikuwa linahangaika kutengeneza dawa ya  kuangamiza wadudu waliovamia mazao, ni kazi ya jeshi kushiriki katika mambo fulani fulani sio lazima mpaka iwe dharura.

Ni matarajio ya wengi wetu kuwa katika sherehe kama hizi zinazoshirikisha majeshi yetu hasa siku ya Muungano, Uhuru wa Tanganyika, Uhuru wa Zanzibar  na Jamhuri tutashuhudia zana zilizotengenezwa katika viwanda vya Tanzania na watanzania wenyewe.

Huko tuendako itafika siku atakumbukwa aliyeanzisha ubunifu huo na huenda wakati huo labda miaka 100 ijayo tutakuwa na adui wa kumtambishia zana zetu, makomandoo wetu na vyote ambavyo vilibuniwa na vijana waliosoma katika hizi shule za Kata chini ya mpango wa elimu bure.  Inshaalah tutafika.