Home Michezo Tuiunge mkono taifa stars, furaha inakuja

Tuiunge mkono taifa stars, furaha inakuja

4271
0
SHARE

NA AYOUB HINJO

Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kucheza mchezo wa tatu wa michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afcon kwa kucheza dhidi ya Cape Verde wiki hii.

Mchezo huo ambao ni wa kundi L ikiwania nafasi hizo sambamba na timu za Uganda, Lesotho na Cape Verde ni muhimu zaidi kwa Taifa Stars ambayo inaisafa nafasi hiyo kwa mwaka wa 38 sasa bila mafanikio.

Taifa Stars ilicheza fainali hizo kwa mara ya kwanza na mwisho mwaka 1980 wakati  zilipofanyika jijini Lagos, Nigeria na kuishia katika hatua ya makundi.

wa kutafuta tiketi ya kushiriki michuano ya Mataifa Afrika ambayo itafanyika nchini Cameroon mwakani.

Mpaka sasa wakati kundi hilo kila timu imecheza mechi mbili kila moja, Taifa Stars imetoka sare mechi zake zote mbili dhidi ya  Lesotho hapa nchini mwaka jana pamoja na Uganda ‘The Cranes’ mwezi uliopita ikiwa ugenini hivyo kujikusanyia pointi mbili tu huku ikiiacha Uganda ikiongoza kundi hilo kutokana na pointi nne.

Lesotho na taifa Stars zote zina pointi mbili kila moja huku Cape Verde ikiwa mkiani kutokana na pointi moja tu.

Taifa Stars itacheza mchezo wa tatu dhidi ya  Cape Verde ugenini wiki hii kabla ya kurudiana baada ya siku nne jijini Dar es Salaam ambayo ni Oktoba 16 mwaka huu.

Tathimini inaonesha kila timu inayo nafasi ndani ya kundi hilo kusonga mbele na kufanya kuwa gumu kutokana na matokeo yaliyopatikana baada ya michezo miwili kuchezwa.

Ugumu wa Kundi L unakuja pale ambako mpaka sasa ni Uganda pekee ambao walifanikiwa kupata ushindi na timu zingine kutoa sare au kufungwa.

Taifa Stars ambao wana pointi mbili watacheza michezo miwili mfululizo dhidi ya Cape Verde, ni fursa pekee ambayo inatakiwa kutumiwa vizuri na Tanzania kupata matokeo ya ushindi ili kujiwekea mtaji wa pointi kuvuka hatua hii.

Kupoteza mchezo huo licha ya kuwa kimahesabu bado wanaweza kuwa na nafasi kama itatokea kushinda mechi zake zote zilizosalia huku ikiwaombea mabaya wapinzani wake

Hata ikitokea kufungwa katika mchezo wa kwanza ambao unachezwa kesho itavunja mioyo ya Watanzania lakini haitaondoa matumaini ya kutafuta nafasi ya kushiriki michuano hiyo mikubwa Afrika.

Lakini ushindi ni kitu pekee ambacho kitatuweka salama katika kundi hilo ambalo linatolewa macho na kila timu.

Huu ni muda wa kila Mtanzania kusimama nyuma ya Taifa Stars na kuiunga mkono ili kuwapa moyo wachezaji ambao wanaipigania bendera yetu.

Mchezo wa kwanza wa kundi hilo uliochezwa hapa katika Uwanja wa Chamanzi dhidi ya Lesotho, haukutumika vizuri baada ya kushindwa kutumia nafasi ambazo zilitengenezwa.

Washambuliaji wa Taifa Stars walikosa nafasi nyingi ambazo zilikuwa za uhakika wa kuipatia timu pointi tatu kwenye mchezo huo lakini ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Katika mchezo wa pili, Taifa Stars, hawakucheza vizuri kutokana na Kocha Mkuu, Emmanuel Amunike, kucheza kwa mtindo wa kuzuia na mipira mirefu kwa wachezaji waliopo mbele.

Kwa kiasi kikubwa aina ya mchezo ule uliifanya timu kuzidiwa lakini hata nafasi chache zilizopatikana kupitia kwa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu hazikutumika vizuri na kufanya mchezo kumalizika kwa suluhu.

Kwa namna moja au nyingine, michezo miwili iliyopita ya Taifa Stars ilishindwa kuamuliwa na washambuliaji ambao walikuwa na jukumu la kuingiza mpira kwenye nyavu za wapinzani.

Naamini kuelekea mchezo wa tatu hapo kesho itakuwa nafasi ya kipekee kwa timu ya Tanzania kufanikisha kile kilichoshindikana katika michezo miwili iliyopita.

Straika ambaye anasumbua barani Ulaya hivi sasa, Samatta, anayecheza KRC Genk naamini atatumia nafasi hiyo kujiandikia wasifu mzuri na kuzifanya timu nyingi kupanga foleni kuwania saini yake.

Pia, wapo akina Simon Msuva anayekipiga Difaa El Jadid ya Morocco na Thomas Ulimwengu anayekimbiza Al Hilal ya Sudan, ni wachezaji makini wanaoweza kutupa furaha Watanzania kwa kutumia uwezo na uzoefu wao kimataifa zaidi.

Lakini upande mwingine wapo yupo Shaaban Idd Chilunda, ambaye hivi karibuni alijiunga na kikosi cha CD Tenerife ya Hispania akitokea Azam FC ya hapa Tanzania.

Katika safu hiyo ya ushambuliaji ambayo kwa mechi zilizopita hawakuonyesha cheche, kesho itakuwa siku ya kipekee zaidi ya kuanza kutimiza ndoto za Watanzania wengi kuiona timu kwenye michuano ya Mataifa Afrika baada ya miaka mingi kupita.

Lakini hata Cape Verde ambao wana kamata mkia kwa kuvuna pointi moja katika Kundi L mpaka sasa, wanaweza kutumia mchezo huo kufufua matumaini yao kwa kutafuta ushindi.

Kikosi chao kilichocheza michezo miwili iliyopita kina wachezaji wanaokipiga katika nchi zilizoendelea kisoka kama Ureno, Ufaransa, Ugiriki, Uturuki, Falme za Kiarabu na kwingineko.

Katika viwango vya FIFA vilivyotolewa Septemba 20 mwaka huu, Cape Verde, inakamata nafasi ya 67 huku Tanzania ikisalia katika nafasi ya 140.

Mwaka 2013, walishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Mataifa Afrika ambayo ilifanyika nchini Afrika Kusini, walipata nafasi hiyo baada ya kuitungua Cameroon mabao 3-2.

Katika michuano hiyo, Cape Verde, walitolewa hatua ya 16 bora kwa kufungwa mabao 2-0 na Ghana na ndoto zao za kufika mbali zaidi ziliishia hapo.

Pia, mwaka 2015 walifanikiwa kushiriki kwa mara ya pili mfululizo, huku wakati huu michuano hiyo mikubwa Afrika ikifanyika nchini Equatorial Guinea.

Lakini katika michuano hiyo ya pili walitolewa katika hatua ya makundi ambalo lilikuwa na Tunisia, DR Congo na Zambia.

Cape Verde wamecheza michezo mingi migumu kwa kipindi chote hicho, kwa namna moja au nyingine timu hiyo wana uzoefu mkubwa kuliko Taifa Stars lakini haimaanishi kama watafanikiwa kupata ushindi mbele ya Tanzania kiurahisi tu.

Hawana historia ya kushirki fainali za Kombe la Dunia, lakini walikaribia kutinga zile za mwaka 2010 zilizofanyika Afrika Kusini baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Ivory Coast.