Home Uncategorized TUJADILI MUSTAKABALI WA NCHI, ELIMU BAADAYE

TUJADILI MUSTAKABALI WA NCHI, ELIMU BAADAYE

2375
0
SHARE

 

NA BALINAGWE MWAMBUNGU

“Eti mfalme hawezi kujisaidia vichakani. Kama atafanya hivyo, vicheche, ndege na wadudu watakuwa na shauku kutaka kuona ukubwa wa mwili wake. Watoto wa gizani wako na umoja zaidi, na wana nguvu kuliko watoto wa nuruni.”

Tulikuwa tunasikia na kusoma katika magazeti kuhusu mauaji ya kisiasa, hasa katika nchi zilizokuwa chini ya tawala za kijeshi kule Marekani, Amerika na Afrika Kusini. Lakini pia kulikuwa na mauaji ya hapa na pale katika baadhi ya nchi za Kiafrika zilizokuwa zinatawaliwa kijeshi.

Kwa upande wa Afrika Mashariki, mauaji ya  wanasiasa maarufu nchini Kenya. Mauaji hayo yaliendeshwa kwa siri kwa sababu  viongozi waliokuwa madarakani waliwaona kuwa tishio, au makundi ya ‘kimafia’ yalipenda kutobadlisha ‘the disturb the status quo’—yaliwaona kama wanaharakati wa mageuzi na  kuwa ni tishio kwao—kwa maana ya kuwanyang’anya ‘kitumbua’.

Bottom of Form

rEmailGoogle+WhatsAppTelegram

Wanasema siasa ni mchezo mchafu. Kwamba watu wote wanaoingia katika mchezo huo, wawe tayari kuchafua mikono yao. Lakini siasa hiyo hiyo inayoitwa mchezo mchafu, ni kitu muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi yoyote ile. Kwenye nchi yenye machafuko ya kisiasa, hakuna amani, utulivu na hakuna maendeleo kwa sababu kila mtu anajifikiria yeye na usalama wake na wa familia yake.

Tanzania hatujawahi kuwa na hali ya wasiwasi tangu tupate uhuru—hata wakati wa vita dhidi ya Iddi Amin wa Uganda, Taifa halikutaharuki—watu waliendelea na shughuli zao kama kawaida—utadhani nchi haikuwa vitani!

Walimu waliokuwa wamepitia mafunzo ya kivita kwenye Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walikusanyika Dar es Salaam na kutaka kuungana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kumng’oa nduli Iddi Amin kutoka ardhi ya Tanzania kule Misenyi, Kagera. Rais Mwalimu Julius Nyerere, akawaabia kuwa vita yao ni dhidi ya adui asiyeonekana—Ujinga. Akasema nendeni mkapigane na adui darasani na mukawafundishe vijana—uzalendo wa kuipenda nchi yao. Ndiyo Tanzania tuliyokuwa nayo.

Lakini tangu ya kuingia mfumo wa vyama vingi, hali ya kisiasa imebadilika—hasa katika miaka ya hivi karibuni. Taratibu tumeanza kuona mmomonyoko wa ukuta uliokuwa umetuweka pamoja unapasuka na kututenganisha—wao na sisi na kuanza kuviziana, kupiagana badala ya kupingana kwa hoja.

Hali ilivyo nchini hivi sasa, inaweza kuelezwa kwamba ni ya taharuki, wasiwasi na woga. Watu kupotea kutekwa na ‘watu wasiojulikana’ na Jeshi la Polisi kushindwa kutoa taarifa ya nini kinaendelea. Umwagikaji wa damu ambao Watanzania hawakuzoea, ni jambo ambalo yanaleta hofu na kuimarisha dhana kwamba watu wanaofanya vitendo hivi wamepewa baraka kutoka juu.

Tanzania haijawahi kuwa na historia kama jirani zetu—Kenya au Uganda—ambako wanasiasa na watu mashuhuri walikuwa wanatoweka, au wanapigwa risasi na ‘watu wasiojulikana’ au wanakufa katika ajali za magari au ndege. Lakini Uganda mambo kama hayo yalikuwa yanafanywa na taasisi ya serikali—the State Reseach Bureau.

Inakadiriwa kuwa watu kati ya 300,000 na 500,000 waliuwawa au kupotea, wakiwamo wanajeshi 9,000, wakati wa utawala wa Jenerali Iddi Amin wa Uganda.

Dk. Wibert Kleruu, ni mwanasiasa pekee Tanzania aliyeuwawa kwa risasi wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere. Alikuwa katika shughuli ya kikazi kama Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Mwandishi wa Habari, Asukile Kyando wa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA), alipotea Shinyanga akiwa katika majukumu yake ya kazi.

Katika utawala wa Jomo Kenyatta wa Kenya, wanasiasa mashukuri—mwandishi wa habari, na mwanasiasa, Pio Gama Pinto, Tom, JM. kwa sababu walikuwa watetezi wa haki na wapinga dhuluma.

Kwenye utawala wa Daniel arap Moi, kati ya mwaka 1990 hadi 2003, watu kadhaa waliuwawa, akiwamo kiongozi wa upinzani Masinde Muliro ambaye alifia uwanja wa ndege wa Kenyetta, akitokea London na Padre wa Kanisa Katoliki aliyekuwa mwiba kwa serikali, John Anthony Kaiser, aliuwawa kule Naivasha. Robert Ouko, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya.

Baada ya hapo kumekuwa na mauaji na ajali za ndege (zisizoeleweka) na kuua viongozi wakiwemo:- Kikalya Kones, Lorna Labaso, George Saitoti, Orwa Ojode, Otieno Kajwang, George Thuo.

Wote hawa waliuwawa kutokana na misimamo yao kuhusu mustakabali wa nchi na kuongezeka kwa mfarakano katika jamii—kwamba nchi ilikuwa na mamilionea 10 dhidi ya maskini milioni 10. Watoto wa gizani, waliwaona hawa kuwa tishio, na njia pekee ilikuwa ni kuwaondoa.

 

Hakuna aliyeachwa salama

 

Watoto wa gizani waliwamaliza watu waliokuwa na ‘kimbelembele’ dhidi ya serikali, hata wafanyabiashara—Jacob Juma, ambaye alitiishia kuwaumbua wakubwa waliochota mabilioni ya fedha katika kashfa iliyojulikana kama ‘Eurobond billions’, Askofu Alexander Kipsang Muge, na kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Titus Adungosi, na Mhadhiri wa Chuo hicho, Crispin Odhiambo Mbai. Pia risasi ziliwaua wabunge—Mugabe Were (Embarkasi) na David Kimutai (Ainamoi).

Hali kama hii imelikumba jimbo la KwaZulu-Natal, nchini Afrika Kusini, ambako tofauti na Tanzania, wanauwana viongozi wa chama tawala cha African National Congress (ANC), katika kile kinachoonekana kuwa ni kugombea madaraka.

Taarifa zinasema ushindani wa kisiasa sio wa kiafya tena. Ikijulikana kama mtu anataka kugombea uongozi, anajenga uwadui wa maisha.

Tangu Januari 2016, wanasiasa 22 wameuwawa na katika miaka minne kabla ya hapo, wengine 100 waliuwawa KwaZulu-Natal pekee, kufuatana na taarifa ya mtafiti Mary De Haas—wengi wao kwa kupigwa risasi wakiwa kwenye magari.

Lakini serikali haijakaa kimya—imeunda Tume ya Uchunguzi inayoongozwa na Mwanasheria Marumo Moerane.

Ni katika misingi hii, inapendekezwa kuundwa Tume ya Kimahakama hapa Tanzania, ili nchi isiendelee kuzama katika tope na kugubikwa na kiza linaloleta hofu kwa wananchi, Jeshi la Polisi, linawajibika kueleza matatizo ya watu mbali mbali waliokufa, kupotea au kujeruhiwa. Hawa ni pamoja na Azory Gwanda- Mwandishi wa habari wa Mwananchi, Ben Saanane wa Chadema, Josia Mzuri, Mfanyabiashara wa Mwanza,

Godfrey Luena wa Chadema, Morogoro, Daniel John, Chadema, Kinondoni Dar es Salaam, Tundu Lissu- Mbunge Singida Kaskazini (Chadema), Alphonce Mawazo wa Chadema, Geita na vijana wawili waliopigwa risasi Arusha, Daud Mwangosi, Mwaandishi wa Channel 10, Iringa, mwanafunzi Akwilina Akwilin, bila kuwasahau viongozi wa CCM waliouliwa na watu wasiojulikana Kibiti, Pwani na idadi inazidi kuongezeka. Wananchi wanataka wajue, ni haki yao kujua.

Mambo haya yakiachwa hivi hivi, ni sawa na kuwapelekea wananchi meseji kwamba vyombo vya usalama navyo vinapita katika hali ya sintofahamu—havijui nini cha kufanya. Hii inaweza kutafsiriwa na jamii kwamba watu wote ambao sio wa itikadi ya watawala, ni wahanga majaliwa—wako peke yao.

Kumetolewa wazo la kuitisha mdahalo wa wazi kuhusu kuanguka kwa elimu nchini, ni wazo zuri, lakini sio mwafaka. Hata kama yatatolewa mapendekezo mazuri ya namna ya kuiokoa elimu ya watoto wa Tanzania, hayataweza kutekelezwa katika hali ya nchi ya sasa ya wasiwasi, taharuki na hofu. Mambo mawili yanaweza kufanyika—Serikali kuitisha mjadala wa wazi wa hatima ya nchi yetu, au kuundwa kwa Tume ya Kimahakama itakayo aanika yaliyojiri na kupendekeza hatua za kuhukua. Nchi ikiisha tengemaa, tujadili mustakabali wa elimu yetu.

Naomba kutoa hoja.