Home Habari Tukomeshe lugha, tabia za kibaguzi wa kijinsia

Tukomeshe lugha, tabia za kibaguzi wa kijinsia

679
0
SHARE
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi

NA DK. HELLEN KIJO BISIMBA

WIKI iliyopita niliona video kwenye mitandao ya kijamii ambayo ilinifedhehesha na si mimi tu pia iliwafedhehesha wengi hasa wanawake kwa kilichokuwepo kwenye video hiyo.

Ninafahamu ni siku chache tu zimepita tangu tutoke katika kuadhimisha siku ya mwanamke duniani na maandalizi ya  kumbukizi ya miaka 25 ya Beijing. 

Kitendo cha Mkuu wa Mkoa  wa Iringa, Ally Hapi ambaye ni kiongozi mkuu katika mkoa, kumwita mbele mtaalamu ambaye ni mganga mfawidhi kutoa taarifa na wakati huo huo anazungumza lugha ya kibaguzi na ya maudhi haikupendeza. 

Katika video hiyo Hapi alisema: “Aaaah mgangaaa, mganga mfawidhi,….. jamani mimi bado nina mke mmoja na mganga naona bado, mganga umeolewa? mganga umeolewa?, ukiona hivyo ujue mambo niii”.

Hata kama nisingetaka kuwa mchambuzi wa masuala ya kijinsia, hii imenilazimu kwani hapa ni kitendo kinachoitwa lugha za kibaguzi kijinsia, hakuna neno moja rahisi la kiswahii la kuweza kuelezea lugha kama hii kwenye hadhira ya kikazi. 

Kwa kiingereza kuna neno linaitwa misogyny na lingine sexism. Kabla sijaanza kutoa uchambuzi ninajua wapo watu ambao wataanza kusema ‘kwani kuna shida gani hapo? , huyo alikuwa anamtania tu, kuna ubaya gani mtu akimtania?

Inabidi tujue kuwa matatizo ya ubaguzi na ukatili wa kijinsia yameanzia mbali na lugha kama hizi ndizo huzoeleka mpaka mwisho, watu huona ni sawa tu kwa kiongozi wa ngazi hiyo kumsemesha ofisa wake mbele ya kadamnasi kiasi kwamba ofisa yule alikosa cha kusema ikabidi acheke na watu wengine nao wacheke badala ya kuguna kwa mshangao.

Nirudi katika maana ya maneno niliyoyaangalia mwanzo neno misogyny kirahisi huweza kuonekana kama ukatili au chuki anaoweza kuwa nao mwanamume dhidi ya mwanamke. 

Lakini kwa upana ni hali ya mwanamume  kutaka kumtawala, kumwonyesha mwanamke kuwa yeye ni zaidi yake au hata kumuadhibu ikibidi. Hii mara nyingi ni pale mwanamke anapoonekana anafanya mambo au vitu ambavyo hastahili au si vya kike kama mfumo unavyomtegemea. 

Tukiangalia katika matamshi ya mkuu wa mkoa huyo na lugha yake ya mwili hatuwezi kusema chuki utaona labda kamfurahia, lakini ukweli kuna hali ya kumtazama daktari kama mtu ambaye hakupaswa kuwa daktari bali alifaa kuwa mke, ndiyo maana mkuu huyo anasema yeye bado ana mke mmoja kwa hiyo mbele yake ni mtu anayepaswa kuwa mke si mtaalamu bingwa aliyefika kutoa taarifa muhimu kutokana na utaalamu wake.

Maneno hayo pia yana hiyo hali ya sexism ambayo nayo ni aina ya hiyo ya juu, lugha za kumbagua mwanamke kijinsia unamshusha kutoka udaktari kumwangalia kama mke wa pili.  

Yaani kinachoonekana hapo ni kama kumwambia yule daktari kuwa ‘pamoja na utaalamu wako wewe ni mwanamke na nafasi yako ni kuwa mke na mimi ninaweza kuwa mume kwa vile bado nina nafasi ya kuoa mke mwingine’. 

Kwa hali hiyo watu wanaacha kumwangalia daktari wanamwona mwanamke anayeweza kuolewa na mkuu wa mkoa. Huu ni udhalilishaji wa kiwango cha juu. Huyu mtaalamu anayekwenda kutoa taarifa ya kitaalamu anakutana na swali  ‘umeolewa?’ Alitarajia ajibu ‘sijaolewa ?’ 

Na iwapo ameolewa huyu mkuu wa mkoa aliona maana ya kauli yake kwa mume wa huyu daktari?. Je iwapo ana watoto, wadogo zake, wazazi wake wanaweza kuchukuliaje maneno kama hayo?

Watu waliokuwa wanashuhudia maneno hayo yupo aliyeonekana kumpigapiga mkuu huyo mgongoni. Ile ingeweza kutafsiriwa kuwa alikuwa anamuashiria hapa si mahali pake au alikuwa anampongeza kwa kumtazama mtaalamu yule na kwa maneno yale. 

Mwingine pembeni alionekana kushangaa lakini baadaye ilibidi acheke na watu wengine walicheka wakiona hili ni sawa. Hali kama hii inatisha na inatilia shaka iwapo mkuu huyo angekutana na mtaalamu huyo katika sehemu ya ofisini angeweza kusema au hata kufanya nini? 

Uzoefu unaonyesha huwa wanaanzia hapo na hatimaye wanafikia vitendo vya kumgusa mtu pasi na ridhaa yake na wakati mwingine bughudha za kingono huendelea kutokea kwenye maneno kama haya ya kibaguzi na kiudhalilishaji. 

Inasikitisha kuwa watu wengi hapa nchini wanaweza kuona hayo maneno kwa urahisi sana, lakini ukweli ni kuwa huu ni udhalilishaji wa daraja la juu. 

Ninavyowajua baadhi ya watu wanaweza kusema ‘mbona mwenyewe hakukasirika?’. Hapa si suala la mtu kukasirika kwani kwa jinsi ilivyotokea na huyo ni kiongozi wake ilibidi tu ajichekee huku akijipanga kufanya wajibu uliompeleka. 

Wale tulioona ndio tumeona ubaya wake na hata mhusika angesema ‘hamna neno’ sisi tunasema kuna neno. Safari ya kutafuta haki na usawa wa wanawake imetoka mbali kiasi kwamba tunao wanawake wataalamu   kama huyu daktari ambaye sasa tunashuhudia akishushwa kiasi hiki mbele ya hadhara. Hii haikubaliki. 

Tunategemea viongozi wawe na weledi wa hali ya juu na waheshimu wataalamu walioko mbele yao wawe wa kike au wa kiume.  Wakati wa kazi si wakati wa mzaha. Mzaha wa kibaguzi kama huo ambao ni mzaha ambao mtu mmoja ameuita mzaha didimizi unadidimiza utu wa mwanamke.

Sitegemei tustahimili lugha na hali kama hii tena kwa mtaalamu wa ngazi hiyo au nyingine yoyote. Mtambue kuwa kuua mfumo dume unaomtazama mwanamke kama chombo cha matumizi kulianza kwa kukataa lugha za watu wazima kuwaita watoto wa kike  ‘mchumba’. 

Uzoefu unaonyesha wao wanaowaita watoto hivyo, ni rahisi baadaye kuweza  kuwabaka au kuwafanyia matendo mabaya ya kingono. 

Nimeona kwenye mitandao ya kijamii kauli za kukemea kama ile ya Mkuu wa Mkoa Hapi na kuna waliosema kuwa kama wanawake na hata wanaume wanaoheshimu wanawake, tukatae na kukemea na mkuu huyu wa mkoa kama amesikia ni vyema akaomba radhi si kwa mtaalamu tu hata kwa wanawake wa nchi hii. 

Mmoja wa wanawake akibezwa, wanawake wote wamebezwa hata mke wa mkuu huyo hakutendewa haki kabisa na mume wake kwa maneno yale.

Kuna waliosema maneno kama haya hutumiwa na viongozi mbalimbali wala si ajabu. Napenda kurudia kuwa haya maneno hayakustahili kutumiwa dhidi ya huyu mtaalamu mwanamke au hata mwanamke mwingine yeyote. 

Ningeshauri waliozoea kuwaangalia wanawake nje ya nyadhifa na sifa zao za kiutu waache na hili la Iringa liwe fundisho ili maneno ya aina hii yasitumike kwa mwanamke mwingine tena. 

Tukumbuke ndiyo kwanza tumetoka kujikumbusha tamko la Beijing na pia maendeleo endelevu ya kijamii  yanayoangaliwa wakati huu, lengo namba tano linakazia usawa wa kijinsia. Hatutaufikia kwa wakati kama miaka 25 baada ya Beijing tunaweza kusikia, kuona na kuvumilia lugha hizi za kibaguzi kwa wanawake. Utu wa mwanamke uheshimiwe.