Home kitaifa Tulitaka mabadiliko ya chama au mtu?

Tulitaka mabadiliko ya chama au mtu?

783
0
SHARE

Na Adrian Mgaya,

WASWAHILI husema ukweli unauma, sikuwahi kuufikiria kwa umakini msemo huu, lakini utendaji wa ‘mwendokasi’ wa Rais John Magufuli, unanifanya nianze kuelewa kinagaubaga maana halisi ya msemo huu.

Wakati wa kampeni za kujinadi kuamua nani ashike usukani wa kuliongoza taifa kulikuwa na ahadi kemkem, nyingi zikileta matumaini kwa Watanzania wa hali ya chini, huku zikiwa tishio kwa waliozoea kutumia vibaya mali za umma.

Tumeshuhudia vyama vyote, vilivyokuwa na nia ya kungoza nchi hasa chama tawala Chama Cha Mapinduzi -CCM na Chadema chini ya UKAWA, ACT – Wazalendo vilitoa ahadi zilizotoa mwanga wa kumkwamua Mtanzania, hata vile vyama vilivyoonekana vidogo navyo havikuwa nyuma katika kumwahidi Mtanzania hali nzuri.

Ni wazi kwamba hali ya mambo Tanzania haikuwa shwari, na ndio maana tukashuhudia majukwaa ya kisiasa yakiahidi neema kwa wananchi.

Si mgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa –Edward Lowasa wala John Magufuli –CCM au mama Anna Mghwira waliokuwa wakipendezwa na hali ya mambo ilivyokuwa ikiendelea nchini, ahadi zao zilithibitisha haya.

Wakati wa kampeni, mkoani Tanga Watanzania walimsikia Magufuli akiwaahidi Tanzania yenye viwanda, huku akiahidi mabadiliko, moja ya maneno alisema “Tanzania yetu inahitaji mabadiliko, na mabadiliko yawe bora, si bora mabadiliko…”

Maneno hayo yalikosolewa na watu wengi, wakidai Magufuli ameiba maneno ya mpinzani wake mkubwa kutoka Ukawa, ambaye alipendwa na wengi kwa kusisitiza mabadiliko.

Ilifikia wakati tukaamini na kufurahishwa na hamasa za wanasiasa wetu, kuwa na jicho la kuona mizizi iliyojikita ndani ya serikali, iliyohitaji nguvu ya kweli isiyo na soni kuing’oa mizizi hiyo.

Swali likaja ni nani ataleta mabadiliko ya kweli Tanzania?

Ni kama panya waliokuwa wakijiuliza nani atamfunga paka kengele? Ni busara na umakini wa hali ya juu uliofanywa na Watanzania kuamua ni nani aliongoze taifa lenye kiu ya mabadiliko.

Vijana ambao wengi walikuwa na hamu ya mabadiliko hayo walihitaji elimu kubwa kuamua nani anawafaa, katika moja ya makala nilizowah kuandika ilisomeka kwa kichwa “Watanzania chagueni mnaemtaka” ikatolewa na gazeti la Tanzania daima.

Makala hiyo ilikuwa na lengo kuwataka Watanzania wamchague kiongozi atakayewafaa na si kukaa vijiweni wakisubiri kubishana nani anawafaa nani hawafai.

Wingi wa wapiga kura waliojitokeza mwaka 2015 inathibitisha Watanzania walichoka na wanahitaji mabadiliko, kura zikapigwa, mshindi akatangazwa.

Utendaji ukaanza, Magufuli akiwa rais chini ya utawala wake nchi ikaanza kunyooshwa na taratibu shilingi ikageuka, utumbuaji majipu ukiwaumbua wale waliokuwa wakila keki ya taifa kwa uchoyo, huku ugumu wa maisha ukiwa ni kwa watu wa hali ya chini.

Ukwepaji kodi uliwahumiza wengi, nikiwa mmoja wa walioumizwa, sikuacha kutumia kalamu yangu kuwakumbusha watawala, katika gazeti la majira la Desemba 15 2015, toleo na. 8011, yenye kichwa “Imetosha sasa tusiruhusu mianya ya ukwepaji kodi”

Ujumbe huo ulikuwa ni salamu tosha kwa Rais Magufuli kumkumbusha moja ya ahadi zake.

Utendaji wa magufuli umetoa mwanga wa safari ndefu aliyonayo Rais wetu, kuleta yale mabadiliko yaliyokuwa yakihubiriwa na wanasiasa wakati wa kampeni.

Ubanaji wa matumizi katika serikali hii, ni moja ya mabadiliko yaliyokuwa yakitajwa na Magufuli na sasa anatimiza.

Hofu imetawala mitaani, wengi wakidai shilingi ‘imeadimika’ na ugumu wa maisha unaongezeka, tunapaswa tukumbuke kuwa subira yavuta heri, wengine watasema ngoja ngoja yaumiza tumbo, lakini tukumbuke pia haraka haraka haina baraka.

Tusubiri ‘kheri’ na ‘baraka’ katika kipindi hiki ambacho wafanyakazi hewa wanaondosha, mapato ya kodi yanaongezeka huku neema ya viwanda ikija Tanzania.

Rais Magufuli anatakiwa asimamie maneno yake wakati wa kampeni, huku Watanzania tukiwa nyuma yake.

Kuna maisha baada ya uchaguzi, na haya ndio maisha yenyewe sasa, siasa za kujinadi ziachwe ulipoishia uchaguzi, na sasa ziendelee siasa za kukumbushana.

Maisha baada ya uchaguzi ni kuacha itikadi za vyama vyetu na kuwaunga mkono viongozi waliopo madarakani wafanye kazi zao, tunachopaswa ni kuwakumbusha tu pale wanapoenda tusipopataka.

Tuanze kuelewa sasa Magufuli anaposema siasa marufuku, ni zile siasa za kukwamisha utendaji kazi, tusipotoshe wala kupotoshwa juu ya kuacha siasa katika kipindi hiki.

Ni mabadiliko yapi ambayo Watanzania tulikuwa tukiyatamani? Kubadilisha chama, mtu au hali ya mambo ilivyokuwa ikiendeshwa na wachache waliojilimbikizia mali kwa njia zisizo halali?

Ni ukweli usiopingika, kiu ya wengi ilikuwa ni mabadiliko yaliyokuwa yakihubiriwa na kina Lowasa na Magufuli.

Tuache unafiki, hakuna aliyekuwa anapendezwa na wachache kujilimbikizia mali ilhali wajawazito vijijini wanajifungua katika mazingira magumu, huku watoto wetu wakichafua sare zao kwa kukaa katika madarasa yasiyo na madawati wala sakafu.

Nchi iliyokuwa imeoza kwa rushwa, haikutoa taswira nzuri kwa wageni waliotutambua kwa amani na upendo tulionao.

Ni aibu kila kona, unapogusa kuna jipu, safari bado ni ndefu rais wetu Watanzania wamekuamini, si wa upinzani wala chama chako, kazi kwako kukata kiu ya walalahoi.

Ukweli unauma, hasa pale ambapo ukweli huu unamuumbua asiyependa kilichowekwa kweli, kusemwa kweli, lakini ukweli huo huo humweka mtu huru, ahadi zako tamu kipindi cha kampeni usiache kuzitimiza hata moja.

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi wa cho kikuu cha Dar es salaam anapatikana kwa namba 0656110670 au barua pepe mgayaadrian@gmail.com