Home Habari Tume ya Madini yaokoa mabilioni ya fedha

Tume ya Madini yaokoa mabilioni ya fedha

278
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

JITIHADA za kulinda rasilimali za nchi hasa madini zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano, zinaelekea kuzaa matunda baada ya Tume iliyopewa jukumu la kusimamia Madini kufanikisha kuokoa kiasi kikubwa cha madini kilichokuwa kinasafirishwa nje ya nchi. RAI linachambua.

Mara baada ya Rais Dk. John Magufuli kuingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015 alionesha nia na dhamira ya kulinda rasilimali za nchi kwa vitendo, kutokana na kuwapo kwa ombwe kwenye usimamizi ya mali za nchi.

Eneo la madini lilionekana kuwa kichaka kikubwa cha baadhi ya watu kujinufaisha kutokana na sheria kuwa na mianya inayowawezesha watu wachache kunufaika zaidi huku Serikali ikiambulia kidogo.

Mwaka 2017 ilipitishwa sheria Mpya ya madini iliyoruhusu kuundwa kwa Tume ya Madini iliyopewa jukumu la kusimamia kwa karibu rasilimali hiyo.

Bila kuchelewa Rais Magufuli aliunda Tume hiyo Aprili 18, mwaka jana kwa kumteua Profesa Idris Kikula kuwa Mwenyekiti wake.

Matokeo ya Tume hiyo yameanza kuonekana ndani ya kipindi kifupi cha miezi sita, kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana kwa kufanikiwa kuokoza zaidi ya kilo 400 za madini mbalimbali ikiwamo dhahabu.

Kazi hiyo ya Tume pia imesaidia kuokoa zaidi ya shilingi Bilioni 30 ambazo zimekadiriwa kuwa thamani ya rasilimali hiyo.

Hivi karibuni Tume ya Madini ilitoa taarifa iliyoweka bayana kuwa dhahabu na madini mengine yenye thamani ya jumla ya sh. bilioni 30.8 yalikamatwa wakati yakitoroshwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana.

Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Profesa Shukuru Manya, alieleza kuwa mbali na dhahabu, madini mengine yaliyokamatwa ni vito ghafi, vito vilivyokatwa na kusanifiwa pamoja na almasi.

Katika mazungumzo yake na waandishi wa Habari mwishoni mwa wiki iliyopita Profesa Manya, alisema madini hayo yalipatikana kutoka kwa watuhumiwa wa utoroshaji kwenye mikoa ya Tanga, Dodoma, Arusha, Geita, Mwanza, Tabora na Dar es Salaam.

Alibainisha kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya jitihada zinazoendelea kufanywa pamoja na tasisi yao kuwa na wakaguzi waaminifu kwenye maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege.

“Uwepo wa wakaguzi wazuri umesaidia kukamata madini yaliyokuwa yakitoroshwa kupitia viwanja vya ndege, mipaka ya Namanga na maeneo mengine kwa maslahi ya taifa,” alisema Profesa Manya.

JUMLA YA KILICHOKAMATWA

Kwa mujibu wa Prof. Manya madini yaliyokamatwa ni  dhahabu kilo 5.72 zenye thamani ya Sh. milioni 389.7 (Geita).

Kilo 323 za dhahabu yenye thamani ya Sh. bilioni 26 zilikamatwa na wakaguzi wa madini katika mkoa wa Mwanza na nyingine yenye uzito wa gramu 77.2 ikiwa na thamani ya Sh. milioni sita ikikamatwa mkoani Tabora.

Vito ghafi kiasi cha gramu 11.4, vito vilivyokatwa na kusanifiwa karati 1,351, vikiwa na thamani ya sh. milioni 206, vilikamatwa mkoani Arusha, vito ghafi kilo 75.9 vyenye thamani ya sh. bilioni 4.1 vilikamatwa jijini Dar es Salaam na almasi kiasi cha karati 66.6, yenye thamani ya sh. Milioni 79.6 ilikamatwa jijini Dodoma.

Kwa Mkoa wa Tanga, dhahabu kiasi cha gramu 168.7, ikiwa na thamani ya sh. Milioni 14.3, ilikamatwa.

Mbali ya utendaji mzuri wa ofisi yake, lakini pia Profesa Manya alikiri kuwa uwapo wa sheria nzuri ya madini umesaidia kufanikisha hatua hiyo ya kudhibiti utoroshwaji wa madini nje ya nchi.

MAFANIKIO ZAIDI

Mbali ya utendaji kazi na sheria, lakini Prof. Manya alisema anaamini wamefanikiwa zaidi kutokana na kujengwa kwa ukuta wa Mirerani.

Alisema tangu kujengwa kwa ukuta huo na kuanza kufanya kazi rasmi Aprili 6, mwaka jana, umeonesha mafanikio makubwa.

Alisema kabla ya kujengwa kwa ukuta huo, mwaka 2016, mapato ya jumla yalikuwa  sh. milioni 71, lakini  kuanzia Januari hadi Desemba, mapato yamekuwa ni sh. milioni 166 na mapato hayo yamekuwa yakiongezeka hadi kufikia sh. bilioni 1.4 katika kipindi cha mwaka jana.

“Kwa ujumla, kwa kipindi cha mwaka mmoja, Tume imejiwekea malengo ya kukusanya sh. bilioni 301, mwakani ni sh. bilioni 430,” alisema.

Kuhusiana na leseni za madini, Profesa Manya alisema hadi sasa leseni 74 za mamdini zimeshatolewa kwa wachimbaji wa ndani na nje ya nchi.

Alisema mwakani serikali inatarajia kutoa leseni kubwa za uchimbaji wa madini kwa kampuni tatu za nje.