Home Tukumbushane TUMEJITAYARISHA VIPI KWA TUKIO HILI KUBWA LA KIHISTORIA?

TUMEJITAYARISHA VIPI KWA TUKIO HILI KUBWA LA KIHISTORIA?

2179
0
SHARE

Makaburi ya askari wa Uingereza waliopigana katika Vita ya Kwanza ya Dunia hapa nchini.

NA HILAL K SUED

Nchi jirani yetu ya Kenya haina vivutio vingi vya utalii ukilinganisha na Tanzania lakini wanaonekana kuwa na ubunifu mkubwa wa kuvifanya vivutio vichache walivyo navyo katika kupata tija.

Sina hakika iwapo mamlaka na taasisi zetu zinazoshughulikia utalii zinafanya matayarisho ya tukio kubwa la kihistoria nchini mwetu miezi miwili ijayo kwa lengo la kuwavutia watalii.

Kama zimelala, basi nawakumbusha tu jirani zetu Kenya wako macho na hilo kwani kwa miezi kadha sasa wamekuwa katika matayarisho makubwa kutumia tukio hilo kiutalii na kulitangaza sana.

Mwezi Novemba mwaka huu (2018) dunia inaadhimisha karne moja (miaka 100) tangu kumalizika kwa Vita ya Kuu ya Kwanza ya Dunia ambapo majeshi ya Ujerumani ya Mfalme (Kaiser) Wilhelm II yaliposalimu amri kwa yale ya washirika waa Marekani, Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya.

Tukio hilo ndilo liliipokonya Ujerumani makoloni yake katika Bara la Afrika ikiwemo nchi yetu Tanzania – wakati huo ikiitwa Germna East Afrika au Deutsch Ostafrika). Nchi nyingine ni Namibia (South West Africa) na Cameroon.

Nchi yetu ndiyo ilihusika kikubwa katika Vita hiyo ya Kwanza ya Dunia nje ya Ulaya kwani ilikuwa uwanja wa mapambano makali baina ya majeshi ya nchi mbili za kikoloni – Ujerumani na Uingereza, ingawa askari wazalendo ndiyo waliokuwa sehemu kubwa sana ya askari katika majeshi ya wakoloni hao.

Baada tu ya vita hiyo kuzuka Ulaya Uingereza ilijiona haiko salama katika makoloni yake Afrika ya Mashariki, hususan Kenya (na pia Rhodesia na Nyasaland – sasa Malawi). Ilifanya matayarisho kulishambulia kivita koloni hili sambamba na mashambulizi dhidi ya Ujerumani kule Ulaya.

Hata hivyo kwa kuwa mapambano makubwa baina ya Uingereza na Ujerumani yalifanyika katika ardhi yetu na siyo Kenya, haitaingia akilini iwapo Kenya watatupiku katika kutumia vita hiyo ya kihistoria kwa kujinufaisha kiutalii.

Ukilinganisha na Tanzania, Kenya wana eneo moja tu la vita – pale ambapo pambano kubwa na la kwanza la vita hiyo lilifanyika – maeneo ya Taita-Taveta karibu na Mbuga ya Wanyama ya Tsavo ambako kwa muda mrefu wenzetu wamekuwa katika matayarisho ya kuweka vivutio vya kitalii.

Vivutio hivyo ni pamoja na Mwashoti Hill – sehemu iliyokuwa ngome ya vikosi vya Waingereza na pia makaburi ya pamoja ya askari wa Ujerumani na Waingereza. Aidha kampuni moja ya hoteli – Saravo Hotels Ltd imejenga mnara mpya katika eneo hilo kama kumbukumbu ya askari wa Kiafrika waliokufa wakiwapigania Waingereza.

Sehemu nyingine ambayo wenzetu Kenya wanaifanya kuwa kivutio cha utalii ni reli ya kutoka Voi hadi Taveta mpakani mwa Tanzania ambayo Waingereza waliijenga kwa madhumuni ya ya kupamnana na Wajerumani waliokuwa wamejichimbia katika Vilima vya Salaita (Salaita Hills).

Kivutio kingine cha watalii ni nyumba moja katika mji wa Taveta ambako inadaiwa ndiyo risasi ya kwanza ya vita hiyo katika eneo hili la dunia ilifyatuliwa. Humo kumehifadhiwa maganda ya risasi, mabaki ya mizinga inayodaiwa kutumika wakati ule na kumbukumbu nyingine za vita.

Sasa hapa Tanzania ambako ndiyo vita kubwa ilipiganwa kuna sehemu nyingi sana za kumbukumbu ya vita hiyo ambazo watalii kutoka nje wangependa kuziona hasa katika maadhamisho ya miaka 100 tangu kumalizika kwa vita hiyo.

Askari wa Uingereza waliingia kupitia maeneo ya mpaka wa kaskazini – eneo hilo la Taveta na Tanga kwa hiyo mapambano makali yalitokea maeneo hayo. Kwa mfano kuna makaburi ya askari waliokufa vitani Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na sehemu nyingine.

Aidha kuna mnara maarufu jijini Dar es Salaam – Mnara wa Askari (Askari Monument) ambao ni kumbukumbu ya vikosi vya askari waliokuwa wabeba zana za kivita wa majeshi ya Uingereza (Carriers Corps).

Maeneo mengine kulikokuwa mapambano ni maeneo ya kusini mwa Tanzania pale askari wa Ujerumani walipokuwa wanayakimbia majeshi ya Uingereza hadi ndani ya nchi ya Msumbiji iliyokuwa ikitawaliwa na Wareno.

Na katika sehemu ya Mto Rufiji unapoingia Bahari ya Hindi bado yako mabaki ya meli ya kivita SMS Konigsberg ambayo ilikuwa meli kubwa ya kivita katika eneo hili la dunia wakati wa vita ile ambayo nayo yanaweza kuwa kivutio cha watalii kutoka nje katika kipindi cha maadhimisho ya miaka 100 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Kwanza.

Meli hilyo ilifichwa na Wajerumani kuogopa kushambuliwa na Waingereza, ingawa baadaye meli za kivita za Uingereza ziliigundua ikiwa mafichoni na kuizamisha kwa makombora mwaka 1915.

Mbali na meli hiyo kuna nmeli nyingine ya kivita ya Wajerumani iliyokuwa ikiitwa SMS Graf von Gotzen katika Ziwa Tanganyika ambayo pia Wajerumani waliizamisha kwa hofu ya kutekwa na Waingereza.

Lakini baada ya Wajerumani kuondoka, Waingereza waliinua na kuifanya kuwa meli ya kubeba abiria na wakaipa jina la MV Liemba. Nayo pia watalii wangependa kuiona katika kipindi cha maadhimisho ya miaka 100.

Kwa bahati mbaya baada ya kumalizika vita hiyo huko Ulaya makubaliano ya kusalimu amri kwa majeshi ya Ujerumani katika eneo hili la Afrika Mashariki hayakufanyika katika ardhi yetu, yalifanyika karibu na mji wa Mbala (zamani Abercorn), Zambia wakati ule Rhodesia tarehe 18 Novemba 1918.

Hapo ndipo majeshi ya Wajerumani chini ya kamanda wao machachari Von Lettow Vorbeck yalipofikia yalipokuwa yakikimbizwa na majeshi ya Uingereza na ambako kumejengwa mnara wa kumbukumbu la tukio hilo.