Home Makala TUMESHINDA UKABILA, UDINI, SIASA INATUPELEKA WAPI?

TUMESHINDA UKABILA, UDINI, SIASA INATUPELEKA WAPI?

2467
0
SHARE

 

Na Goodhope Amani


 Zaidi ya miongo minne, Tanzania imekuwa ikitembea kifua mbele hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki, kutokana na kuwa na historia ya kipekee na kuvutia kama kisiwa cha Amani na utulivu. Pili,  utengamano wa Kitaifa.

Misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume—ndio hasa inatajwa kuifanya Tanzania kuwa nchi pekee Afrika Mashariki kufanya siasa zake kwa mapana, bila ubaguzi wa kidini, Kabila, wala rangi—suala ambalo limechangia  Watanzania kuwa wamoja kwa miongo sasa.

Kama utakuwa mfuatiliaji mzuri wa siasa za Tanzania, lazima utagundua, mabadiliko ya kasi sana yanayokuja, na moja ya mabadiliko hayo huenda yakaondoa ujasiri wa Tanzania kutembea kifua mbele –mbele ya mataifa, kama nchi isiyo na siasa za kibaguzi.

Serikali ya awamu ya tano, imekuwa ikijinasibu kama serikali ya ‘Hapa kazi tu’ huku viongozi wake wakuu wakieleza wananchi kuwa maendeleo hayachagui chama, dini wala kabila, jambo la msingi ni kuwa wazalendo na kupigania maslahi mapana ya Taifa kwanza—jambo  ambalo kimsingi linapaswa kuungwa mkono.

Wakati hayo yakijiri, wapo viongozi aidha kwa kujua, kwa maksudi, au kwa kutojua, wanataka kutuingiza Tanzania katika siasa zile ambazo waasisi wa Taifa hili walizichimbia kaburi. Mathalani, hivi karibuni Mkuu wa mkoa wa Manyara, amenukuliwa na vyombo vya habari akiwahakikishia  wananchi kwamba yupo tayari kupokea simu ya Diwani wa chama chake hata usiku wa maanane ili kutoa msaada, lakini sio Diwani wa Chadema.

Suala hili, japo laweza kuchukuliwa kirahisi, ila maana yake ni kwamba wapo viongozi ambao hawapo tayari kushirikiana na viongozi wa vyama vya upinzani  waliochaguliwa kihalali katika kuendeleza shughuli za maendeleo.

Kama hilo halitoshi, Hivi karibuni katika kampeni za uchaguzi wa marudio wa nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Kinondoni jijini Dar es salaam,  Mgombea wa Chama cha CCM Maulid Mtulia alijinasibu mbele ya hadhara kuwa, wananchi wampigie kura yeye kwani kabla ya kujiunga kwenye chama tawala, hakuwa na namba ya simu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini sasa anayo hivyo anaweza kumpigia na kumweleza shida za wananchi wake.

Tujiulize kidogo, kweli Tanzania tumefikia pahala tuanze kupima maendeleo ya watu kwa vyama vyao walivyovichagua? Kweli tunataka kutengeneza ukuta wa maendeleo kati ya maeneo na maeneo kwa sababu tu ya maamuzi halali ya jamii husika?

Mwishoni mwa mwaka 2017, tumeshuhudia viongozi wengi na wanachama wa vyama vya upinzani, wakiwemo Wabunge na Madiwani wakihama vyama vyao, kwa kile walichokiita kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli ambaye pia ni mwanachama wa CCM.

Najiuliza tu, ni kweli kwamba viongozi hawa wa vyama vya upinzani, wameona wanakosa ushirikiano katika shughuli za maendeleo katika jamii zao, hivyo wakaona ni bora wajiunge na chama tawala, ili shida za wananchi wao ziweze kusikilizwa?

Maendeleo na Kodi

Taifa lolote, ili liweze kuendelea, lazima likusanye kodi. Serikali ya awamu ya tano imejizatiti kuhakikisha ukusanyaji kodi unafikia kiwango stahiki, ili shughuli za maendeleo ziweze kufanyika. Itakumbukwa kwamba  kila mwananchi analo jukumu la kulipa kodi kutokana na shughuli anayoifanya, ili kuipatia serikali mapato.

Kinachofurahisha zaidi ni kwamba, suala la kodi halichagui, kama wewe ni chama gani, kabila gani au dini gani. Swali tu la kujiuliza, iweje viongozi hawa wanataka kutuaminisha kwamba vyama wanavyoviwakilisha  haviwezi kushirikiana na vyama vingine vyema katika shughuli za maendeleo, ilihali katika ulipaji wa kodi kila raia ana wajibu bila kutazama tofauti zao?

 Somo kutoka Kenya

 Nchini Kenya, nchi ambayo ni jirani yetu, kwa muda mrefu imekuwa ikifanya siasa zake zinazoaminika kuwa ni za kikabila. Mwaka 2017, siasa hizo za kibaguzi, ziliibua hoja ya  kutaka kugawanywa taifa la Kenya kulingana na jamii zinavyounga mkono vyama vya NASA na Jubilee.  Wazo hilo likitokea ngome ya NASA, huko Pwani ambako pamoja na madai mengine, ilikuwa ikiona imetengwa katika shughuli za kimaendeleo.

Aidha, hivi karibuni Kenya imekuwa katika wakati mgumu—hasa  kisiasa kutokana na namna inavyoendesha siasa zake, hadi kufikia kiongozi wa upinzani Raila Amolo Odinga, kuwataka wafuasi wake kususia baadhi ya huduma ambazo zinaratibiwa kwa ukaribu na chama, au serikali ya Jubilee.

Huu ni mfano mdogo tu kwa majirani zetu, ambao wamekuwa wakiendesha siasa zenye maswali na zinazoibua sintofahamu mara kwa mara—siasa za kutengana tengana. Swali ni je, Tanzania tunataka kufika sehemu ambapo tutaweza kutengana kutokana na tofautiana zetu za vyama vya siasa?

Hali ya kutojaliwa.

Ipo dhana ya mtu kuwa mtumwa kwenye taifa huru, dhana hii inaonyesha kuwa sababu ya kuwa mtumwa kwenye nchi huru, ni pamoja na kutojaliwa, kuhisi kutengwa kwenye shughuli za kimaendeleo, suala linalo umiza vichwa vya wengi.

Kama wewe ni raia halali wa nchi hii, mlipa kodi kwa serikali—lakini inapokuja suala la maendeleo unajikuta unaamuliwa na chama cha siasa. Uhuru wako wa kufanya maamuzi, si unakuwa hauna maana?

Hatari ya kuhisi kutengwa na kutokukujali, ni kuibuka kwa kundi, au makundi ambayo si rafiki katika usalama wa nchi yoyote ile. Makundi haya yanapohisi kutengwa yanainuka na kuunganisha nguvu kudai usawa—na  inapofikia hapo, utengamano wa taifa unaondoka kabisa. Mathalani, serikali ya Kenya hivi karibuni, ilipiga marufuku kundi linalojiita National Resistance Movement (NRM)—kundi ambalo ni zao la siasa za kibaguzi.

Naamini jambo hili linapaswa kukemewa vikali. Viongozi wa namna hii, wanaojiona wao wana hatimiliki ya nchi hii, kwa kuamua cha kufanya mambo bila kuheshimu maamuzi ya wananchi, hawapaswi kuachwa waendelee na maamuzi yao—hata kwa dakika moja mbele. Lazima  wakemewe vikali, kwani kunyamaza kimya, au kunong’ona kunazidi kutengeneza ombwe, ambalo viongozi hao hujiona wanastahili kuliko wengine.

Hata hivyo, kama misingi ya Taifa hili ilivyo, na vile Rais Magufuli anavyoamini kwamba maendeleo hayana Chama, ni lazima viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia maendeleo, walitambue hilo kwa uhalisia wake, na wanapotumia mamlaka yao kuhujumu maendeleo kwa kisingizio cha uchama, wakemewe.

Upo ukweli usiopingika kwamba, amani yetu, upendo wetu baina ya  jamii moja na nyingine, umeendelea kuwepo kwa miongo takriban sita, kutokana na kutokuwapo na hali ya ubaguzi wa aina yoyote—imani, kabila, rangi au chama cha siasa.

Hivyo basi, kama tunataka kutembea kifua mbele, kama taifa lenye Umoja na mshikamano, lazima tuweke kando na kukemea kwa dhati, chokochoko za ubaguzi zinazopandwa na baadhi ya viongozi.

Naamini Tanzania inaweza kuendelea, kufikia uchumi wa viwanda katika hali yake ya kuheshimiana, kukukubali kutofautiana kisiasa, huku tukishirikiana katika juhudi za kujiletea maendeleo.