Home Makala TUNAHITAJI MAMLAKA YA KUDHIBITI ELIMU- TAMONGSCO

TUNAHITAJI MAMLAKA YA KUDHIBITI ELIMU- TAMONGSCO

715
0
SHARE

NA VERONICA ROMWALD


CHANGAMOTO kubwa inayoikabili sekta ya elimu nchini ni ubora, ingawa zipo nyingine ndogondogo kama vile uhaba wa walimu, uhaba wa miundombinu ya kutosha, mikopo ya elimu ya juu na nyinginezo.

Serikali ya awamu ya tano tangu ilipoingia madarakani imeonesha nia kuzikabili changamoto zilizopo na kila kukicha imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuzitatua. Kadri siku zinavyokwenda mbele, ndivyo ambavyo madudu mapya yaliyokuwa yamejificha katika sekta hiyo yanavyozidi kuibuliwa.

Kwa mfano, suala la mikopo hewa au uwepo wa wanafunzi hewa na matumizi mabovu ya fedha za serikali, ni vitu ambavyo vilikuwa vimejificha ndani ya sekta hii na hivyo kuwa kikwazo cha maendeleo ya elimu nchini kwa namna moja au nyingine.

RAI limezungumza na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali Tanzania (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya kuhusu sekta hii kwa ujumla wake.

Katibu huyu anasema kuwa, madudu yote yanayoibuliwa hii leo yanatokana na kukosekana kwa chombo maalumu cha kisheria cha kushughulikia changamoto zilizopo.

“Tatizo ambalo tunaliona sisi wamiliki wa shule binafsi ni kukosekana kwa chombo maalumu …‘reguratory authority’ kwa ajili ya kusimamia sekta hii. Tunaona sekta ya elimu ni sawa na mali ya mtu mmoja tu ambaye ni elimu, kwa namna ambavyo inaendeshwa nchini.

“Waziri wa elimu amepewa mamlaka makubwa mno ya usimamizi, ni jambo la ajabu sekta kuendeshwa na mtu mmoja kwa utashi wake mwenyewe,” anasema.

Anasema kwa sababu sheria iliyopo inampa mamlaka makubwa Waziri, ndiyo maana kila siku kumekuwa kukitolewa matamko ambayo wamiliki wamekuwa wakiyapinga kwa sababu yanatolewa bila wao kushirikishwa.

“Tunajiuliza kwa nini sekta ya elimu haijaundiwa chombo cha usimamizi hadi leo kama ilivyo kwa sekta nyingine? Kwa mfano sekta ya habari inaelekea huko. Zamani kulipokuwepo redio na televisheni za umma tu hapakuwapo na chombo cha usimamizi (TCRA) ikabidi iundwe.

“TCRA ina bodi yake ambayo inaundwa na wajumbe kutoka serikalini, sekta binafsi na watunga sera ambao hukaa kwa pamoja na kujadiliana na kutoka na msimamo mmoja,” anasema.

Anaongeza kuwa; “leo hii kwenye elimu kuna sekta binafsi na sekta ya umma ambazo zote kwa pamoja zinatoa elimu, lakini anayesimamia maamuzi ni serikali tu ambaye ndiye anafanya maamuzi yote huku sekta binafsi ikiachwa bila kushirikishwa.

Akitolea mfano anasema, hivi karibuni walipokea waraka kutoka serikalini kuhusu mwongozo wa uundaji wa kamati za shule pasipo kushirikishwa. Anasema jinsi wanavyoutazama na kuutafakari waraka huo namba nne wa mwaka 2016, unaonesha wazi kwamba umelenga kuzitaifisha shule zote za Msingi na unamuweka pembeni mmiliki husika.

“Unasema wajumbe wa kamati watachaguliwa na wazazi, watakuwa na uwezo wa kufanya kazi yote ya umiliki wa shule, kazi za mkuu wa shule, kazi za kudhibiti nidhamu na hata kusimamia mwalimu wa taaluma,” anasema.

Anasema kwa mujibu wa waraka huo, kamati hiyo ndiyo inayopaswa kusimamia kila kitu hadi suala la kutengeneza bajeti na hata usimamizi wa fedha.

“Sasa mambo kama haya kungekuwa na chombo maalumu cha usimamizi, tungekaa kwa pamoja wamiliki wa shule binafsi na serikali na kujadiliana jinsi gani tuboreshe sekta ya elimu nchini.

“Ni jambo la ajabu kwani serikali unaweza kukuta haijachangia hata senti mbili kujenga shule, lakini hiyo hiyo ndiyo inayokuja na kupanga bei bila kujua kwamba shule zimekaa na wazazi na kuelewana kulingana na mahitaji,” anasema.

Anasema pamoja na kukosekana kwa chombo cha udhibiti bado hata sheria zilizopo hazifuatwi na ndiyo maana kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wadau.

“Kwa mfano sheria iliyopo sasa inazungumzia juu ya Baraza la Ushauri, ambalo Mwenyekiti wake ni Waziri. Ni sheria isiyotekelezeka kwa sababu tayari usimamizi wote amepewa Waziri mwenye dhamana.

“Kwa msingi huu ndiyo maana tunaona wazi, kukosekana kwa chombo cha udhibiti ndiko kulikopelekea kuwapo kwa changamoto zote zilizopo kwenye sekta hii,” anasema.

Anaongeza kuwa; “leo hii unakuta mtu anachukua fedha za wizara na kuweka kwenye akaunti yake, waziri husika hajui… iwapo kungekuwa na chombo cha udhibiti yangejulikana mapema pengine hata yasingefika huko kwa Rais.

“Tunashuhudia mikopo hewa huko elimu ya juu wakati shule hazina madarasa, hii yote ni kutokana na maamuzi yanayotolewa na mtu mmoja, anakaa nyumbani kwake anaamua na baadae anakuja na kubadilisha mfumo wa elimu alioukuta,” anasema.

“Hata ‘grading system’ wanabadilisha tu leo ‘division’ kesho GPA bila kushirikisha wadau, shule ya Msingi tulikuwa na mihula mitatu, wamebadilisha na kutaka tuweke miwili, sisi tulifanya hivyo kwani Aprili huwa ni mwezi wa mvua na hivyo mabasi hushindwa kufika katika baadhi ya maeneo mfano Sinza kutokana na mafuriko.

“Sasa leo hii tumebadilishiwa matokeo yake ni kwamba watoto watakaposhindwa kufika shuleni, watashindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao, ikifika hapo watasema walimu wavivu, wazazi hawawafuatilii kumbe chanzo ni sera mbovu tu ambazo zipo kwenye elimu yetu,” anasema.

Katibu huyo anafafanua kuwa hata suala la kupigwa marufuku kwa uvaaji wa majoho ngazi za chini za madarasa ni suala lililopasa kushirikisha wadau.

“Hili nalo ni tatizo, ingawa sina jibu la moja kwa moja maana inawezekana Waziri ana sababu ya msingi lakini sisi wadau hatuijui. Wadau wana sababu zao labda waliona yakivalia watoto watafaulu vizuri, maana anayepewa vitu wakati wa sherehe ina mfanya afanye vizuri zaidi lakini hatujashirikishwa tunaona tu kwenye vyombo vya habari,” anasema.

Katibu huyo anasema, iwapo matamko yataendelea kutolewa katika hali ya namna hiyo ni wazi kwamba mfumo wa elimu nchini utaendelea kuwa mbovu.

“Tutazidi kuwa ombaomba, chukulia mfano tu kwamba kama leo ‘Daily News’ angelisimamia RAI, lisingekuwapo kabisa. Hata kwenye usafirishaji zamani UDA waliposimamia usafiri wa daladala hapa Dar es Salaam kabla ya kuundwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), daladala nyingi zilikufa.

“Kwa sababu UDA walijipangia njia za Kariakoo na Posta na daladala nyingine wakazipangia njia za Mbagala, Gongo la Mboto ambako zilikosa wateja lakini ilipoletwa SUMATRA imesimama kati ya hawa wawili na sasa mambo yanakwenda vizuri,” anasema.

Anaongeza kuwa; “elimu inahitaji chombo kama Sumatra na Ewura, chombo ambacho kitasimama kati ya sekta binafsi na serikali, kuliko sasa ambapo mtoaji mmoja wa huduma (Serikali) anamsimamia mtoaji wa huduma ambaye ni binafsi.

“Tuna mawazo na malalamiko mengi kutoka kwa wanachama kwa namna ambavyo serikali inafanya ambayo nayo yanapaswa kusikilizwa, sekta ya elimu haiwezi kuboreka iwapo hakutakuwa na chombo cha udhibiti kusimamia pande zote mbili, kitakachokusanya maoni yao na kuyafanyia kazi,” anasema.

Anasema sekta ya elimu ni pana inayojumuisha wadau wengi hivyo si sawa maamuzi kutolewa na mtu mmoja.

“Sekta ya elimu ina wanafunzi wapatao milioni 10, kila mwanafunzi ana watu wawili ambao wanamuangalia, ina wadau milioni 30 kati ya watanzania milioni 45 waliopo idadi ambayo ni zaidi ya asilimia 70.

“Ni ajabu kukosa chombo cha kusimamia wakati ndiyo sekta muhimu inayotegemea kuzalisha wataalamu wa kuisaidia nchi. Waziri hapaswi kufanya kila kitu, sheria iliyopo inapawa kufutwa itengenezwe nyingine ambayo itasimamia mfumo mzima wa elimu,” anasema.