Home Latest News TUNAKWENDA KULE WENZETU WALIKOTOKA

TUNAKWENDA KULE WENZETU WALIKOTOKA

1726
0
SHARE

NA JOSEPH MIHANGWA


JAMII iliyojifunga ni ile isiyoruhusu mawazo huru kumea, ushindani wa fikra kushamiri, uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari na kuhabarishwa kutamba. Ni jamii isiyonufaika na dhana kongwe ya kidemokrasia yenye kuruhusu “maua mia moja kumea/kuchipuka; fikra kinzani mia moja kuibuka na kukinzana” ili kusafisha, kung’arisha na kupevusha jamii.  Kinyume cha hayo, ni kuihukumu jamii kuchakarika na kuteketea kwa kutu.

Jamii ya aina hiyo huendelea nyuma ya migongo ya wananchi; shughuli zote za umma hufanywa kwa siri inayolindwa kufanya wananchi kuwa watazamaji tu na “wapiga majungu” kwa kujaribu kubashiri kinachoendelea, badala ya kuwa washiriki na wachangiaji wa mawazo. Haki ya kujieleza hubinywa kwa njia ya kuhodhi [kubana] vyombo vya habari kwa Sheria kali za uchochezi [sedition]; haki ya mwananchi kujua juu ya Serikali yake hudhibitiwa au kutokuwepo kabisa; uwazi ambao ni moja ya misingi mikuu kwa jamii ya kidemokrasia huangamia.

Inapokuwa hivyo, nafasi na heshima katika jamii ya taasisi muhimu kama vile Mahakama, Bunge, vyombo vya habari, taasisi za kitaaluma na asasi za kiraia, hutoweka. Ndani ya makando kando ya giza ya mfumo huo, maamuzi huwa ya kuparanganya, “ukabila”, upendeleo na unafiki wa kisiasa hutia fora. Kwa ngazi ya uongozi, ueledi wa mtu, uadilifu, ukweli, uwazi na uaminifu huwa si vigezo muhimu tena vya uongozi bora; bali kinachotiliwa maana ni uwezo wa mtu wa kupepeta ulimi na kujipendekeza kwa sauti na kwa kutoa povu.

Hiyo ndiyo jamii iliyojifunga, yenye kubana uhuru wa habari kwa hofu ya kuzalisha umma wenye uelewa na uwezo wa kuhoji, kujadili na kutoa maoni juu ya kinachoendelea katika jamii kwa haki yake.

Suala la uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa habari ni historia ya mapambano kama ilivyo tu historia ya mapambano ya demokrasia na haki za binadamu dhidi ya watawala.  Kile kinachofanya vyombo vya habari viitwe “mhimili wa nne” katika nchi baada ya Bunge, Utawala na Mahakama, kinatokana na nguvu ya vyombo hivyo ambavyo siku zote ni tishio kwa watawala wadhalimu. Wakati nchi za dunia ya kwanza zilikwishaachana na udhibiti huo tangu miaka 130 iliyopita, Watanzania, chini ya mitizamo hasi inayoshamirishwa na tabaka la kifisadi katika kulinda maslahi yao wasiumbuliwe, kwa kubana uhuru wa Habari, tunajaribu kwenda kule wenzetu walikwishatoka zamani.

Uhuru wa mawazo na wa kupata habari ni biashara ya kuuza na kununua mawazo kwa bei ya soko kama lilivyo soko la bidhaa zozote zingine. Jamii hunufaika kwa njia ya kubadilishana mawazo kwani hakuna mtu aliye na jibu kamili juu ya matatizo yanayoikabili jamii. Kwa mtizamo huu, chombo cha habari kitasitawi tu kwa ubora wa habari zake, na kile chenye habari dhaifu na hafifu kitajifia ndani ya nguvu ya soko. Kwa mantiki hii, si jukumu la Serikali wala la mtu mmoja kuamua ni mawazo au habari ipi inafaa kuchapishwa na ipi haifai wala kusema ni habari ipi ni ya kweli na ipi ni ya uongo kwa sababu ule unaoweza kuitwa uongo leo, kesho unaweza kugeuka kuwa ukweli ukipewa nafasi ya kujidhihirisha na kujithibitisha.

Kwa mfano, kama tungekubali maelezo ya Serikali kwamba kashfa ya Akaunti ya Escrow ya IPTL, kashfa ya Rada, Richmond na zingine lukuki, kuwa zilikuwa za kutunga au za uongo na uchochezi, tungejuaje leo, kwamba yote hayo ulikuwa ufisadi wa kutisha ulioatamiwa na vigogo wa Serikali kwa mbinu za tabaka hilo kuficha maovu?. Mbona wanamstari wa mbele Bungeni dhidi ya udhalimu huu, walioitwa “Tumbili”, leo ndio mashujaa wa vita dhidi ya ufisadi baada ya ukweli kupewa nafasi kujidhihirisha?.

Jamii lazima ifike mahali iruhusu mtu mmoja kutangaza ukweli kwamba “Mfalme yuko uchi”, hata kama mtu huyo ataonekana “muongo”, kwa sababu kile kinachoitwa uongo leo, kesho kinaweza kugeuka kuwa ukweli, kama mtu huyo atapewa nafasi ya kusikilizwa.

Tutazame kwa ufupi tu historia ya uhuru wa kujieleza katika nchi zenye demokrasia komavu, yaani, Uingereza na Marekani, na ambazo kutoka kwao sisi tumeazima mfumo wa demokrasia; tuone kama uhuru huo kama sehemu ya demokrasia, unafanya kazi ipasavyo hapa kwetu.

Wakati wa enzi za Wafalme nchini Uingereza, adhabu kali ilitolewa kwa wale waliojaribu kuhoji vitendo au mamlaka ya Mfalme. Kwa mfano, karne ya 9, Mfalme Alfred wa Uingereza aliagiza kuwa, kila aliyejaribu kuihoji Serikali akatwe ulimi kwa kuwa ulimi ndio uliokuwa nyenzo pekee ya mawasiliano na ya kujieleza.  Hivi leo, ulimi huo ni vyombo vya habari vinavyoweza “kukatwa” kwa njia ya kufungiwa au kushitakiwa kwa makosa ya “uchochezi”, chini ya Sheria kandamizi. Na ingawa mwaka 1620, uhuru wa kujieleza ulipata sapoti kubwa kutoka kwa Mfalme James wa I, lakini hata hivyo, Mfalme huyo naye hakuweza kutoa uhuru kamili alipoonya kwamba “masuala ya Serikali si mambo ya kuzungumzwa mitaani; mtu hapashwi kumsema au kumkosoa mtawala na utawala wake”, aliagiza.

Kuibuka kwa uchapishaji wa habari kulitoa tishio jipya kwa watawala kwa vile maandishi ni kitu cha kudumu na uwezekano wa kuwafikia watu wengi ni mkubwa. Ili kudhibiti hali hiyo, dola ilitoa amri kuwa magazeti yote yaandikishwe na kudhibitiwa, na yale yasiyofanya hivyo yafungiwe au kufutwa kabisa. Ilikuwa mwaka 1689, pale Malkia Mary [na mumewe William], alipochukua madaraka kwamba Uingereza ilianzisha Sheria ya Haki za Binadamu [Bill of Rights] na kulipa Bunge ukuu [Parliamentary sovereignty] na hivyo uhuru wa kujieleza.  Kwa hatua hiyo, haki za raia zilitambuliwa, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa mawazo moja kwa moja au kupitia vyombo vya habari.

Huko Marekani, uhasama kati ya Serikali na vyombo vya habari uliyeyusha uhuru huo, hasa, kufuatia kesi ya uchochezi iliyomhusu mchapishaji, John Peter Zenger, mwaka 1735, pale Mahakama ilipotoa kwa raia [kwa chukizo la Serikali] uhuru na haki ya kujieleza au kupinga na kuikosoa dola ilipobidi. Kuanzia hapo, Sheria ya Uchochezi ilibakia kwa jina tu hadi mwaka 1801 ilipofutwa na Rais Thomas Jefferson alipoingia madarakani. Uingereza kwa upande wake ilifuta makosa yote yanayohusu “habari za uongo” [False News Offences] mwaka 1887.

Uhuru wa kujieleza kama ilivyo demokrasia, lazima uzingatie vigezo na viwango vya kimataifa.  Hivyo, kama kweli tumekubali kufuata mifumo ya demokrasia, uhuru, na haki za binadamu kwa mfumo wa nchi za Magharibi, kama vile demokrasia na utawala bora, utawala wa Sheria, soko, siasa na uchumi huria; iweje leo tuendeleze udhibiti kwa vyombo vya habari ambao kwa wenzetu ulipigwa marufuku zaidi ya karne mbili zilizopita, bila kuathiri ubora na uimara wa Serikali?. Je, ni kwa hofu ya kuambiwa “Mfalme yuko uchi” inapokuwa kweli Mfalme huyo hana nguo na kuwatuhumu wote wasioweza kuiona suti hiyo “hewa” kuwa ni wadhambi, na kwa dhambi zao eti wamenyimwa uono na uwezo wa kuiona suti ya Mfalme na hivyo waadhibiwe kwa kutobolewa macho?.

Jamii makini haiwezi kukubali kulazimishwa kushangilia au kusifia Mfalme asiye na nguo kwa sababu tu eti “suti” aliyovaa inaonekana kwa wasio na dhambi, wakati ukweli yuko uchi; au kwa vitisho kwamba “wasioiona” suti hiyo ni wadhambi, na hivyo watobolewe macho kama adhabu kwa “dhambi” za kufikirika. “Uchochezi” ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu [Penal Code], kifungu cha 50 na 55. Wakati Sheria hii inadhibiti uhuru wa kujieleza kwa kuupaisha kuwa “uchochezi” [sedition], lakini tofauti na hilo, Katiba ya nchi inatoa uhuru huo bila kikomo chini ya Ibara ya 18, kwamba, “….kila mtu yuko huru kuwa na maoni YOYOTE [yawe ya kweli, au kimuonekano kuwa sio ya kweli] na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati”.

Kwa kuzingatia matakwa ya ibara hii ya Katiba, je si kweli kwamba, yale yanayoitwa “makosa ya uchochezi”, si uchochezi bali ndio uhuru wenyewe wa kujieleza na wa kutoa maoni yoyote?.  Je, huko si kuingilia kati uhuru wa mawasiliano wa mtu?. Ni nani mwenye haki ya kuamua uhalali wa maoni [yoyote] na aina ya uhuru wa mawazo ya mtu katika kutekeleza haki hiyo ya Kikatiba?.  Je, ni halali kwa mtu kushitakiwa chini ya Sheria za Makosa ya jinai kama tulivyoona hapo juu?.  Ni kiwango gani cha uhuru kinachovumilika ili usiitwe “uchochezi”?. Maswali haya yanatufanya turejee kesi ya hivi karibuni nchini Uganda ya Charles Onyango – Obo na mwenzake dhidi ya Serikali.