Home Latest News ‘Tunao binaadamu kisura ila roho za shetani’

‘Tunao binaadamu kisura ila roho za shetani’

964
0
SHARE

Na Rashid Abdallah,

Ikiwa kuna watu wanadiriki hata kuiba pesa ambazo zilipelekwa Kagera kwa ajili ya kuwasaidia walioathirika na tetemeko la ardhi, hapa kuna tafsiri nyingi: Moja ni kuwa miongoni mwetu hatuna hata chembe ya utu na kwamba tunaishi kama  binadamu kisura tu lakini roho zetu ni za kishetani. Kwa roho hizi umasikini utazidi tu!

Katika kuutathmini umasikini wa Afrika, wapo waliokaa kitako na kisha kuja na hitimisho kuwa umasikini wetu haupo tu katika chochoro za miji yetu, bali hata ukiperuzi/google kati ya ‘African Children’ na ‘American Children’, (watoto wa ki-Afrika na waki-Marekani) basi utapata picha tofauti.

Sizungumzii utofauti wa rangi, rangi ni jambo lisilo na maana hata kidogo, ila ukweli ‘google’ itakuonesha watoto wa Afrika walikonda miili, ngozi za mbavu zikiwa zimekamatana na mifupa, wengine wakiwa wameshika silaha wako vitani, utaona pia picha za watoto waliochakaa ngozi hadi mavazi, wakiishi katika mitaa iliyochoka.

Tabasamu zao haziashirii lolote zuri isipokuwa wanazichekelea tu zile kamera za Wazungu waliokuja kuwatembelea katika magheto yao (mitaa ya watu masikini), ila mioyoni mwao wamesongwa na matatizo ya umasikini, njaa, vita, majanga yanayozikumba nchi wanazoishi.

Lakini ‘google’ hiyo hiyo itaakuonesha watoto wa Ulaya ama Marekani, wakiwa wamenawiri miili, wamekaa madarasani wakijisomea, tabasamu zilizoshiba zikitoka mioyoni mwao, wengine wakiwa kwenye bustani nzuri na hali zao zikipendeza machoni.

Utofauti huu wa watoto wa Kiafrika na mataifa mengine, hatuwezi kuwalaumu waendeshaji wa mitandao hii, ila tunapaswa kujitathmini na kujilaumu sisi wenyewe, kuanzia viongozi wetu na kila anayehusika na hali ngumu ya bara hili.

Lililo wazi ni kuwa, wenye nguvu mara nyingi hujifikiria wao kwanza, na ndio ripoti ya hivi karibuni imefichua jinsi rais  Salva Kiir wa Sudani Kusini anavyojitajirisha yeye na viongozi wengine na familia yake, huku nchi ikiwa katika umwagikaji mkubwa wa damu na umasikini ulioota mizizi.

Wakati kuna mamilioni ya watu masikini, watoto, wanawake nchini Sudan Kusini, huku wakimbizi wakiongezeka kila siku lakini bado kiongozi mkubwa anafikiria kupata yeye kwanza na familia yake. Inasikitisha!

Hayo si Sudan tu, hata hapa kwetu kunadhihirika kuwa wenye nguvu na roho za shetani wanajifikiria wao kwanza kabla ya walala hoi mitaani, sio ajabu ukisikia mtu mmoja kaiba mamilioni ya pesa kutoka serikali yetu.

Mioyo ya kufikiriana haipo, ndio utawala wa sasa unaendelea kufichua mengi ya upoteaji wa pesa kiholela, kisha unajaribu kuziba mianya ya namna hiyo, (ushukuriwe kwa hilo),  ila ukweli utabaki kuwa nchi nyingi za ki-afrika hali bado ni tete, zulia la ufisadi, rushwa, ukwepaji kodi la balaa nyingine nyingine bado limetandikwa ndani ya mataifa yetu.

Naamini raisi aliyepita hata kama  angepewa karne nyengine ya kuongoza nchi hii, basi maendeleo tungeendelea kuyasikia tu kwenye redio (tena za kimataifa) ama kuyaona mara moja moja kwenye runinga za Ulaya, lakini katu kwetu yasingefika.

Tuki-google watoto wa Kiafrika na waki-Tanzania wakiwemo, tungeendelea kuona watoto wenye hali ngumu za kimaisha, wakiwa na nguo chakavu,  ngozi zilizosinyaa zikiashiria umasikini uliosongo mikono yao tena kwa nyuma.

Hatukuwa tukijuwa wengi wetu, lakini kumbe kila kona ya taasisi ya nchi hii ni ulaji kwenda mbele, bandari ilijaa upotevu wa pesa, taasisi nyingi zilibeba wafanyakazi hewa, rushwa ilikithiri, pesa zinaingia na kuishia kwenye mikono ya wababe wachache. Bado ungetengemea maendeleo hapo? Au kiongozi anayeongoza taifa kama hilo akuletee maendeleo? Tungesubiri sana!

Serekali ya iliyopita, ukweli usiofichika ni kuwa ilijisahau kupita maelezo, kila linalofichuliwa linawaacha watu vinywa wazi, kumbe nchi imeanza kutafunwa na wachache miaka mingi sana?

La kusikitisha ni kuwa hadi wanafunzi ambao ni tegemeo la kesho kuwa viongozi, wapo miongoni mwao waliokwepa kulipa mikopo yao, ni zaidi ya masikitiko. Walaji na wakwepaji majukumu yao wapo kila kona.

Huwezi ku-google na ukakuta maisha watoto wa Kiafrika yananawirika kwa hali kama hizi za sasa, nchi zetu nyingi ni kama vile zinaogozwa na magenge ya wenye elimu za kula, wanaojua zaidi kula kuliko kutenda.

Maisha yetu kama yataingizwa katika simulizi, kisha mtunzi mahiri wa hadithi tukampa kazi ya kutuandalia hiyo hadithi, basi hakuna shaka wasomaji wangekuwa wanabubujikwa na machozi ya kutuonea huruma; wengine wangefura kwa hasira wakitoa maneno mazito na  laaza kwa kwa ambao wanatuongoza.

Ashukuruwe JK kwamba nchi aliiacha salama, amani ya kwenda dukani na kurudi ipo, lakini ni aibu kwake kila raisi wa sasa anapofichua upotevu wa pesa mbao ulikuwa unamwagika wakati wa utawala wake.

Udhaifu wa serekali iliyopita ndio uliosababisha fedha nyingi za umma kupotea, ikiwa serekali ya sasa inajitahidi kufichua na kuibana mianya ya upotevu wa pesa basi hata serekali iliyopita isingeshindwa kufanya hivyo. Ila ilikunywa mvinyo wa Amarula, ikalewa na kulala, wajanja wakajikombea.

Abdullatiff Abdallah katika sanaa yake ya,”Sauti ya Dhiki” akieleza juu ya nyani waliotengeza ngazi kwa kushikana mikia hadi kileleni mwa Mnazi, ili kwamba wachache wao wapande juu ya migongo ya nyani wenzao.

Pindi wafikapo kwenye nazi wazichume na kuziachilia zianguke chini, ili wazikusanye na kuzigawa miongoni mwao.

Lakini wale waliofika juu ya mnazi wakaanza kula nazi huko huko juu na kuwasahau waliochini na waliounda ngazi. Nyani wa chini walipouliza; “nini cha mno? Wale Nyani wa juu walijibu,”tuacheni tujikimu kwanza maana sisi tuko hapa juu ilhali nyinyi mko hapo chini.”

Sanaa hii haina tofauti na uendeshaji wa mambo katika nchi yetu, serikali itabeba lawama kwanini kuna watu wanapata visivyo halali kwa kivuli cha serikali, lakini hawa wanaokula nao pia wanalaumika kwa nini wanakula vyao na visivyokuwa vyao!

Kinachotokea ni kile ambacho Abdullatiff Abdallah amekieleza, Nyani waliotengeneza ngazi kwa kushikana mikia, ili kiendacho kuchumwa juu ya mnazi kiangushwe na kiwanufaishe wote la kusikitisha ni kuwa, waliofika kileleni walianza kula na kuwaacha wengine na njaa.

Ni Watanzania waliopiga kura, wametengeneza ngazi ili wengine wao wawe viongozi kisha mafanikio ya uongozi yaangushwe chini wanufaike wote, lakini viongozi baada ya kukaa madarakni wanakuwa mafisadi papa na wizi na kula peke yao?

Ufisadi, rushwa, wizi, ukwepaji wa kodi yamekuwa yakipoteza pesa nyingi mno kila siku, watekelezaji wa mambo hayo miongoni mwao ni hao hao wanasiasa ambao wamewekwa kutumikia raia lakini kumbe wanatumikia matumbo yao.

Nchi inayopewa mikopo, inasamehewa madeni, raia wanalipa kodi, inapewa misaada, ardhi ya kutosha, madini, misitu, utalii na mengine mengi ambayo ni sehemu ya rasilimali lakini bado hayajatumika na kumnufaisha raia wa chini, ukiambiwa nchi hiyo bado ni masikini yakupasa ukune kichwa.

Kuna nyani wako kwenye minazi, ndio wanaozuia nazi kuja chini, kwa hiyo siku zote maendeleo yetu hayatokwenda kwa kasi ya Usain Bolt, la kushukuru ni kuwa kuna mwanga wa hawa Nyani kushushwa sasa.

No:0773526254