Home Latest News TUNASAMBAZA CHAKULA KWAKUWA HAKUNA NJAA?

TUNASAMBAZA CHAKULA KWAKUWA HAKUNA NJAA?

707
0
SHARE
Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, akikagua maghala ya chakula

Na Markus Mpangala,

TAARIFA rasmi ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema hakuna njaa. Wiki kadhaa zilizopita tulitaarifiwa na Rais John Magufuli akiwa mkoani Simiyu alisema yeye ndiye mwenye mamlaka ya kusema kama kuna njaa au haipo.

Kauli yake ilisababisha majadiliano makali kila kona ya nchi. Makundi mawili yalijigawa katika mantiki tofauti. kundi la kwanza lilipingana na kauli ya Rais na kudai kuwa kuna baa la njaa.

Kundi hilo liliongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye alieleza bayana kwenye kampeni za uchaguzi mdogo kuwa nchi yeti inabiliwa na tatizo la njaa hivyo kila mwananchi anatakiwa kufahamu ukweli huo.

Vilevile kundi hili lilitumia taarifa ya ukame ya Afrika, ambapo Mbunge wa zamani wa Kigoma kusini, David Kafulila, katika andiko lake kwenye gazeti dada na hili la Mtanzania, alidai ifikapo mwezi Machi mwaka huu kutakuwa na njaa kali miongoni mwa wakulima.

Kundi la pili lilimuunga mkono Rais Magufuli na kudai hakukuwa na njaa, lakini likakubali kuwa na tatizo la ukame kwa baadhi ya maeneo. Inadaiwa kuwa ukame huo umechangia baadhi ya kaya kukosa chakula.

Kundi hilo limesema hayo huku likisisitiza kuwa usambazaji wa chakula unaofanywa na serikali unalenga kukabiliana na kupanda bei.

Ukiyasikiliza makundi hayo kila mmoja anajaribu kuwa na hoja. Kila kundi linawaona wengine ni wavurugaji, lakini kati yao wote hakuna anayekubaliana na mwenzake.

Labda tujiulize swali, je ukame umesababisha ukosefu wa mazao? Kama jawabu ni ndiyo, ina maana kuna shida ya chakula ambayo haitakiwi kusemwa baa la njaa?

Kama jawabu ni hapana, ni kwanini chakula kinasambazwa kwa minajili inayoitwa kukabiliana na kupanda bei? Ina maana kupanda kwa bei hiyo ni jibu la kukosekana kwa chakula?

Si nia yangu kuendeleza malumbano, lakini nakiri kuwa makundi hayo yote yametukanganya sisi wananchi. Makundi hayo yamekuwa na sababu mbalimbali.

Kwa mfano kundi la pili linadai kuwa Mamlaka ya Chakula inayo hifadhi ya tani 90,000 na baadaye chama cha CCM kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole walitueleza kuwa zipo takribani tani milioni 1 na nusu kwenye ghala ya chakula. Ilikuwa idadi ambayo haikuonyeshwa kwa picha bali maneno. Twende mbele zaidi katika tafakuri.

NJAA IPO AU HAIPO?

Swali kuu ndilo hilo; njaa ipo au haipo nchini? Ili kuhitimisha uchambuzi wa leo napenda kutumia mfano huu madhubuti wa kisa kilichotokea katika nchi fulani, kisha unayesoma itakulazimu kufikiri na kuamua jawabu la swali letu.

Mosi, siku ya kwanza toleo la kwanza la gazeti moja la ughaibuni la miaka fulani katika nchi moja hivi liliandika kichwa cha habari kisemacho: “Ni waziri shoga?

Gazeti hilo likaeleza kuwa Waziri fulani katika nchi hiyo alikuwa anatabia inayodaiwa kujihusisha na wapenzi wa jinsia moja. Gazeti halikutaja jina la Waziri husika. Likasema amewahi kuwachukua mashoga na makahaba kulala nao.

Msingi wa hoja ya gazeti ilikuwa matumizi mabaya ya mali za umma zilizofanywa na Waziri husika. Chama chake kikaanza kulikasirikia gazeti na kudai limtaje. Gazeti halikutaja.

Pili, toleo la pili la gazeti hilo hilo likabeba kichwa cha habari  “Waziri akesha kwenye danguro.” Ulikuwa mwendelezo wa habari ya Waziri aliyekuwa anaandikwa. Kama kawaida gazeti halikutaja jina la Waziri.

Ilisemwa Waziri husika alikuwa akiwachukua makahaba kulala nao. Ikawa imechochea ghadhabu kwa chama chake na wabunge wake wakalitaka gazeti limtaje. Gazeti halikupoteza dira yake. Liliendelea kukusanya taarifa za Waziri husika.

Tatu, toleo la tatu la gazeti hilo likaanza kutaja maeneo anayowachukua mashoga na makahaba. Kama kawaida halikutaja jina la Waziri husika. Kumbuka awali haikusemwa ni maeneo gani. Kuona hivyo chama tawala kilipiga kelele na kudai gazeti lithibitishe madai yake.

Miongoni mwa wapigakelele alikuwepo yule Waziri. Gazeti likaendelea na dira yake, halikumtaja. Lakini kolidoni fununu zilikuwa bayana miongoni mwa wanasiasa wakaambizana mlengwa ni nani. Wakajua ila walitaka uthibitisho wa gazeti.

Nne, toleo la nne la gazeti likamtaja Waziri husika na maeneo yake aliyokuwa akichukua makahaba au mashoga. Likachapa na picha zilizowahi kumnasa katika nyendo zake.

Baada ya kuchapwa hayo yote, wale wanasiasa wakanyamza. Wakajua habari iko hadharani. Wale wabunge wa chama chake hawakupanua midomo tena. Wakanyamaza, wakamwambia hilo lako kabiliana nalo. Mwishowe Waziri akajiuzulu wadhifa wake na kuomba radhi kwa kukosa staha Mbele ya jamii.

Kimsingi swali linatujia, je tunasambaza chakula kwakuwa njaa ipo au haipo? Hilo ndilo swali langu kuu kwenye safu hii leo. Ndio tafakuri ninayokuachia msomaji wangu. Muda utasema. Nawatakia wakati mwema. Kwaherini kwa leo.