Home Makala Tunataka Tanzania ya viwanda sio kebehi

Tunataka Tanzania ya viwanda sio kebehi

950
0
SHARE

NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

WAKATI akiwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Dk. John Magufuli, ambaye sasa ndiye Rais wa Tanzania, aliahidi mambo mengi ambayo sina hakika kama walau nusu ya hayo atayafanya kuwa halisi au ni ndoto, ni suala la muda kujua hilo.

Moja kati ya ahadi tamu ya Magufuli, ambayo ilivutia masikio ya wasikilizaji wengi wakati huo ni ile ndoto ya Tanzania ya viwanda. Hii haikuwa tu ahadi ya kawaida ya kisiasa bali walau ilionyesha ni kitu kinachowezekana kama utashi wa kisiasa utakuwepo.

Ni fursa nyingine ambayo chama chake inatakiwa kuitumia ili  kujisahihisha kwa kuwapatia watanzania nafasi za ajira, uhakika wa kuuza mazao yao ya kilimo, ingesaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa idadi kubwa ya vijana wanaomaliza elimu kutoka vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Hakutakuwa na fursa nyingine ambayo itapatikana huko mbeleni kwani idadi ya wananchi wanaohifadhi kumbukumbu inaongezeka, idadi ya wanaohoji na kutaka majawabu inazidi kuwa kubwa, wananchi wanaofikiri wanakuwa wengi na wajinga wanaotumiwa na wanasiasa wanapungua.

Tanzania ya viwanda ndio hasa iliyosubiriwa kwa miongo kadhaa tangu ile ya mwanzo ya Baba wa Taifa hili Mwalimu Julius Nyerere ilipouzwa kwa wakoloni wapya ambao siku hizi wamepewa jina lisilo na ukakasi.

Wanaitwa wawekezaji. Nchi ambayo mkulima na mfugaji watakuwa na uhakika wa kuuza mazao yao, nchi ambayo rasilimali na utajiri mwingine wa asili utainufaisha ndio hasa ilikuwa inasubiriwa.

Dalili za uwezekano wa kuzaliwa upya  kwa Tanzania ya viwanda zilianza kuonekana mara tu Rais alipoanza kuteuwa wasaidizi wake.

Tulishuhudia wasomi wabobevu wakiwemo Maprofesa, Madaktari wa falsafa, Wahandisi na wasomi wengine wakichomoza katika teuzi za zake na kushika nafasi za Uwaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi nakadhalika .

Tumeona bila kificho majemedari wa jeshi na majasusi waliobobea wakiteuliwa kuwa Ma RC na Ma DC, tumeona wengine wakishika nafasi za kuwa makatibu tawala wa mikoa na wilaya. Naam! Serikali imesheheni watu wenye weledi katika idara zote, kama ni timu ya mpira basi hii ubingwa uko wazi.

Wote wamesoma barabara, lakini hatujaona hasa elimu yao imesaidia vipi Tanzania iondoke hapa ilipo. Hakuna ugunduzi ambao tunaojivunia kuwa umetokana na wasomi hao na hakuna matarajio ya kuwepo kwa mabadiliko katika siku za usoni kama hali itaendelea kuwa hivi.

Ni bahati njema hata Rais wetu ni msomi, mwanakemia mbobevu, matarajio ya watanzania kwake na wasomi wenzake aliyowateua ni makubwa mno. Kila wakilala wakiamka wanatarajia kuishuhudia Tanzania ya viwanda. Tanzania ya Magufuli!

Watanzania wataka kusikia mipango na mikakati ya kuifikisha nchi yao  kuwa taifa la uchumi wa kati, uchumi unategemea viwanda vikubwa, viwanda vya kati na viwanda vidogo. Hawana haja na wajihi wala siha ya mtu binafsi katika kuifikia taifa hilo.

Suala na nani kafuga ndevu na kwa sababu gani sio haja yao, wala halisaidii kubadili hali yao iliyopo sasa,  uimara na kujidhatiti kwa silaha za kisasa kwa jeshi ni fahari yao wote, sio fahari ya chama kimoja cha siasa.

Wengi wanakumbuka kwamba Rais alishauri kuwa badala ya kuendekeza siasa, wachape kazi, tuwatumie wataalamu walioteuliwa katika nafasi mbalimbali ndani ya taasisi za serikali kuisaidia nchi kutoka katika mkwamo na udumavu huu.

Kuongoza ni kuonyesha njia, Rais wetu atuonyeshe njia ili tuifikie nchi ya ahadi. Nchi inayoitwa Tanzania ya viwanda, wananchi tumechoka na maneno na kebehi zenye chuki kutoka kwa wanasiasa, sio tu  kutoka kwa viongozi wa upinzani bali hata vinywa vya viongozi wa ngazi ya juu ya CCM.

Husda, chuki, choyo, ghilba, wivu, tamaa, maringo, majivuno ni nembo na alama kuu inayotambulisha kiongozi wa CCM ya leo. Badala ya upendo, ushirikiano, heri, uzalendo, amani na mapatano.

Wanasiasa wengi hasa kutoka CCM wanatamani wananchi wote wawaunge mkono wao na chama chao, kama sivyo basi hata uraia wao unatiliwa shaka, ama wataonekana kama watu wa daraja la chini wasio na maana wala kuhitajika.

Tunasikia kila wakati Rais anaomba aombewe ili aweze kuwa na afya njema na maisha marefu. Sina hakika kama yeye anarudisha fadhila kwenda kwa wale wanaomwombea na hata wanaomchukia. Rais ni muumini wa Kikristo tena Mkatoliki, bila shaka anaijua vyema Bibilia.

Wiki iliyopita Rais alikuwa ziarani Pemba na Unguja. Lengo la ziara yake ni kuwashukuru wananchi waliomchagua. Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali ziara hiyo ilifurahiwa sana na wanachama wa CCM ambao ndio hasa walijitokeza kumpokea ni kuibua maswali kama ziara ile ilikuwa ya kichama au ya kiserikali.

Pamoja na ziara hiyo kuibua shangwe kutoka kwa wanachama wa CCM, lakini upande mwingine wale wa chama kikuu cha upinzani visiwani humo walionekana wakinung’unika na hadi sasa wana maswali lukuki vichwani mwao.

Julius Mtatiro, Kaimu Mwenyekiti wa CUF alinukuliwa akisema kuwa  ziara hiyo ya Magufuli ilijaa maneno ya kebehi, dhihaka na vitisho kwa wananchi wa Visiwani hasa wale wasiounga mkono chama cha Rais Magufuli. Anasema badala ya kutoa hotuba yenye matumaini na inayounganisha wananchi, Rais amefanya kuta za masikilizano kuwa ndefu zaidi.

Serikali yetu imeahidi mambo mengi makubwa na magumu, mmoja ni hii Tanzania ya viwanda, kuna reli kwa viwango vya kimataifa, kuna kuhamia makao makuu ya nchi Dodoma, kuna kuifufua shirika la ndege la taifa ATCL, kuna kujenga uwanja wa ndege wa Chato, kuna kujenga barabara za juu kwa juu (flyover) elimu bure tangu msingi mpaka sekondari.

Yote haya na mengine ambayo sikuyataja yanahitaji matrilioni ya shilingi za kitanzania, hivi mipasho na kuzungumzia ndevu za mwanaume mkaazi wa Pemba ambaye kwa tamaduni zao ni jambo la kawaida itatusaidia? Mi nadhani ni matumizi mabaya ya muda na nguvu ambazo zingetumika katika kusema masuala mengine yenye manufaa kwa nchi yetu.

Ingefaa zaidi majeshi yetu yakatumika kufanya mambo yenye kujenga upendo na uzalendo kwa wananchi wote, badala ya kufanya mambo ambayo yanaonekana dhahiri hata kwa watoto wachanga kuwa ni vitisho dhidi ya  wote wasioiunga mkono CCM na Serikali yake.

Amani, mshikamano, muungano, na upendo, ni matunda yanayotokana na haki. Bila hivyo hata ikapita kizazi hiki, kile kinachokuja kitafukua makaburi yenu na kuwahoji kuhusu haya mnayofanya leo. Chonde chonde wasomi mnaoongoza nchi, jitofautisheni na kijiwe cha wacheza bao, tunangoja nchi ya viwanda.