Home Makala Tusikibeze Kiswahili na kukipamba Kiingereza

Tusikibeze Kiswahili na kukipamba Kiingereza

559
0
SHARE

NA HASSAN DAUDI

UNAPOUZUNGUMZIA utamaduni, hakuna namna ya kuiweka kando lugha kwani ndicho chombo cha mawasiliano kwa watu wake ndani ya jamii husika.

Kwa miaka mingi, vyombo vya habari (nyenzo za kufikishiana taarifa) vimekuwa silaha muhimu katika utamaduni wa jamii yake. Kwamba, ndiyo nyenzo ya kulinda, kuendeleza na kuzitangaza mila na desturi za watu wake.

Ni kwa maana hiyo basi, unapatikana uhusiano wa moja kwa moja kati ya lugha na vyombo vya habari. Kupitia magazeti, redio, televisheni na mitandao ya kijamii, maneno mapya yamekuwa yakiibuliwa, ambapo baadhi yao husanifishwa.

Hivyo, mchango wa vyombo vya habari si tu kuilinda na kuitangaza nje ya mipaka inamotumika, bali pia kuiendeleza lugha.

Mfano; ni ngumu kutenganisha mafanikio makubwa ya Lugha ya Kiswahili, hata kufikia hatua ya kutambulika kimataifa, ikifundishwa katika vyuo vikuu vikubwa barani Ulaya na kwingineko, na kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vya habari.

Katika kuelezea hilo, utakuwa sahihi kusema njia hizo za kufikishiana taarifa ndiyo mdau mkubwa wa Kiswahili, ingawa pia huwezi kuwasahau wasomi wa Lugha hiyo na wazalendo wengine.

Hata hivyo, wakati huu, ambapo Kiswahili kimeendelea kupigiwa chapuo kuwa lugha rasmi ya kufundishia kuanzia sekondari hadi elimu ya juu, waandishi wa habari wameonekana kujisahau kwa kiasi kikubwa.

Huenda nikawa karibu na ukweli kusema wao wameishia kuripoti juu ya jitihada zinazoendelea, huku wakiwa wamezipa kisogo kwa kuruhusu upotoshaji mkubwa wa lugha.

Ukiacha makosa mengi ya kisarufi yanayofanywa na waandishi na watangazaji kila uchwao, kero kubwa ni utumizi usio na tija wa maneno ya Kiingereza katika vipindi au magazeti ya Kiswahili.

Nikiwalenga zaidi waandishi wa habari za michezo, umekuwa ni utamaduni mpya kuona maneno ya Kiingereza yakipamba kurasa za mbele za magazeti kwa kigezo cha ubunifu.

Ukweli usio na chembe ya shaka, inashangaza kwa kiasi kikubwa kununua gazeti lenye kichwa cha habari ‘Fantastic’, ‘Yes We Can’, ‘goodbye’, ‘out’ au ‘deal done’ na kukutana na habari ya Kiswahili. Tuamini kwamba maneno hayo yalitumika baada ya kukosekana ya Kiswahili kuelezea dhana husika?

Hebu niulize, ni kweli waandishi au wahariri wanaofanya kazi katika magazeti ya Kiswahili ni wabunifu zaidi katika kutafuta vichwa vya habari wanapotumia Kiingereza? Sambamba na hilo, unaweza kujiuliza ni utafiti gani uliowathibitishia kuwa wateja wao huvutiwa na hilo?

Binafsi huwa najiuliza, hao wanaofanya hivyo ni kwa faida ya nani ikiwa msikilizaji, mtazamaji au msomaji, ambaye ndiye bosi wao, si mahiri wa Kiingereza?

Je, hawaoni kufanya hivyo ni kutomtendea haki endapo atashindwa kupata ujumbe lengwa (message) kwa kuwa tu alishindwa kuelewa maneno mawili ya lugha hiyo?

Pili, nikiwa mmoja kati ya wanataaluma wa uandishi wa habari, ni kweli utumizi wa Kiiingereza ndicho kigezo cha mwandishi au mtangazaji kuonekana ana weledi usio na shaka katika kazi yake? Sioni sababu ya kutowaita limbukeni!

Tatu, ikiwa wao ni mahiri wa Kiingereza, kwanini wasiende kufanya kazi katika vituo vya redio, televisheni au magazeti yanayotumia lugha hiyo pekee kufikisha ujumbe kwa hadhira?

Huenda waandishi wanaofanya hivyo hawana uelewa wa kutosha juu ya dhima ya chombo cha habari katika maendeleo ya Kiswahili, hasa karne hii ya 21, ambayo imeonekana kuwa ya mafanikio makubwa kwa lugha hiyo.

Mathalan, wanaojifunza Kiswahili kupitia magazeti, wanaanza kuipoteza fursa hiyo kwa kuwa nayo yamegeuka ya Kiingereza, jambo ambalo kwa kujua au kutojua, lina madhara makubwa katika safari iliyopo ya kuifanya lugha hii kuwa ya kufundishia elimu ya juu na kukubalika ulimwenguni kote.