Home Makala Tusikubali wahisani walete misaada na kuirejesha kwa  mlango wa uani

Tusikubali wahisani walete misaada na kuirejesha kwa  mlango wa uani

4305
0
SHARE

NA ERICK SHIGONGO

Wamarekani kupitia maandiko mbalimbali wamenifundisha ukweli kwamba njia mojawapo ya  kuongeza mzunguko ya fedha katika taifa ni kuanzisha miradi mbalimbali, pale unapotokea ukata katika taifa la Marekani, nchi hiyo huwa haigawi fedha bure kwa wananchi wake bali huanzisha miradi mingi, mfano ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na kadhalika, kwa kufanya hivyo fedha hushuka chini kutoka serikalini mpaka kwa mwananchi wa kawaida na kupunguza kama si kuondoa kabisa ukata katika jamii.

Hali hii ni tofauti kabisa na bara letu la Afrika, ambako miradi mingi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara, reli na kadhalika  inaweza kuanzishwa lakini bado ukata ukawa mkali mtaani kuliko wakati kabla ya kuanzishwa kwa miradi hiyo.  Jambo hili husababisha wananchi wanaoteseka na ugumu wa maisha kuendelea kuichukuia serikali iliyoko madarakani hata kama inafanya mambo mengi ya maendeleo yanayoonekana kwa macho.

Jambo hili limekuwa likinisumbua sana kichwani mwangu, kwa nini Tanzania inajenga reli ya kisasa, imenunua ndege na kufufua shirika la ndege, barabara zinajengwa kila kona ya nchi, elimu ni bure, madawa yameongezeka mahospitalini, na kadhalika, mambo mengi ambayo kwa hakika yalitakiwa yawafanye Watanzania wote wawe wanaiimba vizuri serikali yao, lakini badala ya kufanya hivyo wameendelea kuwa wagumu, wakilalamika kila kukicha kama vile hakuna kinachofanyika.

Suala zima hapa ni mzunguko wa fedha, mafanikio yote yanayofanyika hayafiki moja kwa moja mezani kwa mwananchi wa kawaida na hivyo kumfanya aendelee kuona yote yanayofanyika ni kama hayamhusu, wakati kiukweli kazi inafanyika.  Mzunguko wa fedha unapokosekana, ukata huingia, wananchi hushindwa kumudu maisha na kinachofuata huwa ni malalamiko.

Fedha zinakwenda wapi wakati tuna miradi yote hii?  Kwanza kabisa lazima tukumbuke kwamba asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima na wanaishi vijijini, chanzo chao kikubwa cha mapato ni kilimo, hiki ndicho hutengeneza mzunguko wa fedha kwa Watanzania walio wengi, lakini inapotokea kwamba wamelima mazao yao, ukame ukajitokeza, ama soko la mazao likawa baya lazima mzunguko wa fedha utakosekana na tabu itaingia.

Ni kweli miradi ni mingi, swali la kujiuliza fedha wanazolipwa wakandarasi hawa ni kweli zinawafikia wananchi wa kawaida, zinatengeneza mzunguko?  Ukifuatilia sana miradi mingi mikubwa ya ujenzi inayofanyika katika nchi hii ambayo ingetakiwa kutengeneza mzunguko mkubwa inaendeshwa na kampuni za kigeni, ambazo zimekuja hapa kufanya biashara na kurejesha fedha na faida kwenye mataifa yao.

Reli ya ‘standard gauge’ inajengwa na Waturuki, daraja la juu ya Tazara limejengwa na Wachina.  Hii ni mifano michache tu ya kukonyesha kwamba kinachofanyika nchini Marekani cha kuanzisha miradi ili kutengeneza mzunguko wa fedha katika nchi nyingi za Afrika hakifanyiki, Waturuki hawa wanaojenga reli watachukua fedha hizi na kuzirejesha kwao wakiacha punje tu hapa nchini, vivyohivyo Wachina.

Mambo haya kwa mtazamo wangu ndiyo yanayofanya lengo la kutengeneza mzunguko wa fedha kwa kutumia uanzishaji wa miradi  lisifikiwe, swali ambalo kila siku najiuliza, je, hakuna Mtanzania wa hapahapa anayeweza kujenga mradi kama wa daraja la Tazara?    Kweli nchi yenye watu milioni 50 ikose mjasiriamali hata mmoja mwenye uwezo huo, siamini.

Hata kama hawapo, kuna tatizo gani iwapo hawa wawekezaji wa kigeni wanaokuja Afrika kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu wangeingia ubia na wazawa ili kubakiza sehemu ya mapato hapa nchini na kutengeneza mzunguko ili hatimaye kuondoa ukata mitaani?

Kinachofanyika nyuma ya utaratibu huu mbaya ni kampuni hizi za kigeni ni kutumika kurejesha fedha zote ambazo mataifa ya Magharibi huzileta Afrika kwa jina la misaada kupitia mlango wa nyuma, huku yakitarajia kulipwa fedha nyingine zaidi kama riba ya misaada hiyo.  Huu ni ujanja ambao umetumiwa sana na mataifa ya Magharibi lengo likiwa ni kuchota utajiri wa Afrika kuupeleka kwao, Afrika sasa ni lazima iamke.

Siku zote imeaminika kwamba nchi tajiri duniani zimekuwa zikitumia utajiri wake kuziondoa nchi za Kiafrika katika umaskini; misaada mingi imekuwa ikitiririka kuja Afrika na mataifa mengine yanayoendelea na kujenga taswira kuwa nchi tajiri zinafanya kila kinachowezekana kuzisaidia nchi maskini, jambo hili limekuja kuthibitika wazi kwamba ni kinyume chake kwani nchi tajiri huchota zaidi kutoka katika nchi maskini kuliko zinavyodai kupeleka misaada.

Kwa mujibu wa utafiti wa shirika la Kimarekani liitwalo Global Financial Integrity (GFI) pamoja na kituo cha utafiti cha Shule ya Uchumi  ya Norway uliotolewa hivi karibuni umeonyesha kwamba kiasi cha fedha kinachochotwa kutoka Afrika na nchi tajiri ni kikubwa kuliko kile ambacho nchi hizo zimekuwa zikipeleka.

Mfano kwa mwaka 2012 peke yake utafiti huu unaonyesha kuwa nchi zinazoendelea zilipokea jumla ya Dola trilioni 1.3 kutoka kwa mataifa tajiri katika misaada,  uwekezaji  na mapato mbalimbali kutoka ng’ambo, lakini katika mwaka huohuo kiasi cha Dola trilioni 3.3 zilichotwa kutoka katika mataifa maskini kwenda kwa mataifa tajiri.

Uchotaji huu hufanyika katika mfumo wa ulipaji madeni ambazo nchi za Afrika zinadaiwa, faida ambazo mataifa tajiri yanapata katika uwekezaji wa makapuni yake kwenye mataifa yanayoendelea, mfano kampuni za ujenzi, mafuta, mawasiliano, uchimbaji wa madini na kadhalika.

Lakini pia kuna aina mbalimbali za wizi ambazo makampuni ya nchi za Magharibi yanazifanyia nchi zinazoendelea na kutorosha kiasi kikubwa cha fedha kutoka katika nchi hizo na kuendelea kuzinyonya badala ya kuzisaidia ili zijikwamua kutoka katika umaskini kama ambavyo propaganda za nchi za Magharibi inataka dunia ielewe.

Kama nusu ya fedha zote ambazo nchi za Afrika zinatumia katika miradi mbalimbali zingebaki katika nchi hizo, hakika mzunguko wa fedha ungekuwa mkubwa mno na ukata mtaani ungepungua, lakini badala ya jambo hilo kufanyika mataifa makubwa yamekuwa yakiruhusiwa kutorosha fedha ambazo yamezileta Afrika kama msaada kupitia mlango wa nyuma, jambo ambalo ni hatari kabisa kwa maendeleo ya nchi maskini.

Makampuni haya ya ujenzi yatataka yaagize kila kitu kutoka nje, kama ni nguzo za umeme zitatakiwa ziingizwe kutoka nje, lengo likiwa ni kuongeza kiasi cha bei kwenye bidhaa hizo mwisho wa siku kampuni ionekane imepata faida kidogo na hatimaye kulipa kodi ndogo kwa serikali, si hilo tu makampuni mengi ya Magharibi yanafanya kazi Afrika, hufungua kampuni tanzu katika nchi zenye kodi kidogo au zisizotoza kodi kabisa, kama Mauritius na Visiwa vya Virginia, huko ndiko hutoroshea fedha nyingi wakijifanya kulipia huduma kumbe wanajilipa wenyewe na kukwepa kiasi kikubwa cha kodi.

Kwa nini mambo haya yanaachwa kuendelea, hivi hatuwezi kutunga sheria inayoyashinikiza makampuni haya kuingia ubia na kampuni za nyumbani, kulikuwa na tatizo gani kama Watanzania watatu wangeunganisha kampuni zao (JV) na kuunganisha nguvu na mwekezaji wa Uturuki kujenga reli?  Je, fedha ambazo Mturuki leo hii analipwa zisingebaki hapa nyumbani na kupunguza ukata mtaani?

Sina tatizo lolote na wageni  wanaomiminika hapa nchini kwetu, lakini nina tatizo nao tu pale ambapo wanaonekana kuchukua miradi yote mikubwa, mfano ya ujenzi na baadaye kurejesha tena fedha kwenye nchi walikotokea.  Au huwa ni sharti kwamba “tunawapa msaada, lakini mkandarasi lazima atokee katika nchi yetu?”

Kama hivyo ndivyo, basi ni vyema basi nchi za Kiafrika zianze kuikataa misaada yenye masharti ya namna hiyo kutoka nchi tajiri, hakuna jina jingine la kukiita kitendo hiki zaidi ya kuingizwa mjini, fedha zote zinarejea kwao kwa mlango wa nyuma,  halafu nchi maskini zinaendelea kuteseka kwa miaka mingi zikilipa madeni yasiyolipika, mwisho miundombinu hiyohiyo waliyoijenga kwa fedha ya wahisani itaishia tena kuwa kuwa mali yao kama iliwekwa dhamana.

Ni bora nchi yetu iendelee kutokuwemo katika orodha ya nchi zinazodaiwa na China kama misaada ya taifa hilo kwa Afrika inalazimisha kwamba miradi yote ijengwe na kampuni za China, wito wangu kwa taifa langu ni kwamba wakati umefika wa kuwawezesha wazawa kwa vitendo, siyo kuwa na tume ya uwezeshaji wazawa iliyo kwenye makaratasi, huku wazawa wakiendelea kuwa vibarua wa wageni ambao kila kukicha wanatorosha fedha kwenda kwao na kuacha njaa mtaani.

Hawa tunaowaachia njaa, tukumbuke ndiyo wapiga kura wetu watakaoamua nani atuongoze kesho, unaweza kuwapa madaraja, ndege, barabara, dawa, lakini kama hakuna mzunguko wa fedha unaoleta chakula mezani, mwisho wa siku wataishia kukuchukia tu hata kama uliwafanyia nini, na mtu mmoja akitokeza mbele yao na mkate na kuwalisha, watasahau kwamba uliwahi kuwanunulia ndege. Tuyadhibiti mataifa ya Magharibi yaache kutuibia kupitia mlango wa nyuma.