Home Makala Tusipuuze adha ya ‘misongamano’ hii mingine jijini Dar

Tusipuuze adha ya ‘misongamano’ hii mingine jijini Dar

1902
0
SHARE

‘Msongamano’ kwenye barabara za Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

NA HILAL K SUED

Akizindua, Alhamisi iliyopita, daraja la juu kwenye makutano ya Barabara za Nyerere na Mandela jijini Dar es Salaam lililopewa jina la “Daraja la Mfugale” lililogharimu Ts 107 bilioni, Rais John Magufuli, pamoja na mengine, alisema anataka kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa jipya kwa kuboresha miundombinu na kuweka madaraja ya juu ili kupunguza msongamano wa magari.

Rais Magufuli alisema nchi imekuwa ikipoteza zaidi ya Sh400 bilioni kila mwaka kutokana na watu kutumia muda mwingi katika foleni ambao wangeweza kufanya uzalishaji, na hivyo kwa kulitambua hilo, serikali imeamua kuifanya Dar es Salam kuwa mpya, kwa kuboresha miundombinu ili kuondoa msongamano.

Kwa muda mrefu suala la msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam – ambao ni bandari kuu na kitovu cha shughuli za uchumi na biashara – limekuwa la mjadala mkubwa. Hii inatokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la magari – wataalamu wanakadiria ongezeko ni la zaidi ya mara 10 (asilimia 1,000) katika miongo miwili iliyopita, huku uendelezaji wa miundombinu ukiwa unasuasua sana.

Pengine kabla sijaendelea na makala hii ni vyema nikazungumzia suala zima la msongamano, kwani lenyewe pia ni mjadala mkubwa katika nchi nyingine yoyote ile. Swali kubwa la kujiuliza ni iwapo foleni ndefu za magari katika barabara zetu ni ishara ya kushindwa kwa sera za serikali na viongozi wake. Kama tunakubali kwamba foleni katika mabenki, migahawa au sehemu za kununua tiketi ni alama ya mafanikio, kwa nini tuzione foleni za magari barabarani kwa mtazamo hasi?

Misongamano ya magari ni adha inayotokana na kuwepo kwa miji mikubwa ambayo ni makazi ya watu wengi. Kwani kama tusingekuwa na miji mikubwa misongamano ingekuwa hakuna au kuwapo ya kadri tu. Lakini miji mikubwa lazima iwepo kwa sababu ni vitovu vinayosukuma maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii nchini. Hivyo misongamano barabarani hutokea pale ambapo idadi kubwa ya watu hufuatilia malengo haya kwa wakati mmoja ndani ya maeneo madogo.

Hivyo kuna ukweli kwamba misongamano ya magari barabarani ni ishara ya maendeleo katika jamii na barabara zilizo tupu ni ishara ya kudorora kwa maendeleo.

Lakini upande wa pili wa sarafu, na kama alivyoeleza Rais Magufuli, misongamano ya magari barabarani husababisha hasara kubwa kwa jamii na kwa serikali – zikiwemo matumizi makubwa ya nishati ya mafuta yanayotumika bila tija yoyote wakati magari yamesimama katika foleni. Aidha wafanyakazi katika sekta ya umma kama vile serikalini, na watu wengine katika sekta za uzalishaji huchelewa kufika makazini.

Lakini wakati tunapoziafiki hatua za serikali katika kuboresha miundombinu inayolenga kupunguza misongamano ya magari na kulipendezesha jiji la Dar es Salaam, tusisahau eneo jingine la jiji hili hili ambalo tangu ujio wa serikali ya Awamu ya Tano, linazidi kuzorota na inavyoonesha hakuna suluhisho kupatikana katika muda wa karibuni.

Hili ni kuongezeka kwa wafanyabiashara ndogo ndogo – maarufu “wamachinga” katika barabara za jijini hususan maeneo ya katikati ya jiji hadi kuyafanya maeneo hayo kuharibika mandhari yake na kuanza kuchusha pamoja na kuwa adha kwa wakazi wengine. Tukubali hawa nao wanasababisha ‘misongamano’ ya aina yake katika barabara, na ili kulielewa hili vyema tembelea maeneo ya Kariakoo kwenye barabara kama za Tandamuti, Congo na Nyamwezi ambapo uwingi wa biashara za barabarani zinasababisha misongamano ya magari (na ya watu pia) kwenye barabara hizo.

Halafu kuna suala la ulipaji kodi – si tu kwamba wafanyibaiashara hawa ambao wanaweka biashara zao mbele ya maduka yaliyo rasmi hawalipi kodi yoyote kutokana na biashara zao – kana vile Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Kodi ya Mapato (Income Tax) au ada kutokana na liseni za biashara, pia wanawafanya baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka wanaotambulika rasmi katika ulipaji wa kodi hizo nao kutolipa kodi kutokana na kukosa wateja.

Tunaweza kusema ukweli kwamba jamii hiyo ya Watanzania kwenye barabara zetu ambao wengi wao ni vijana, hawapendi kufanya shughuli hizo za barabarani, bali wanalazimika – na hiki ni kielelezo tosha cha kufeli kwa utawala katika sekta nyingine muhimu (mbali na ile ya miundombinu) kwa maendeleo ya wananchi – kama vile elimu na ajira.

Lakini kila enzi ina mitume na vitabu vyake, methali inasema. Tafsiri ya methali hii kwa kifupi ni kwamba historia ina lazimu ya kuzeesha mambo, kuyapa muonekano wa kupitwa na wakati na hivyo kuyatupilia mbali.

Tawala mbali mbali, katika vipindi tofauti nazo hulazimika kubadili staili zao za utawala, sera na vipaumbele, bila shaka mazingira ya kisiasa yanalazimisha. Lakini hata hivyo, kuna mambo ambayo hayabadilishwi kwa utashi wa siasa, bali hutokana na kushindwa kwa watawala kufanikisha sera au jambo, na hivyo hucheza na matokeo ya mapungufu yake na kugeuzwa kuwa ndiyo sera yao mpya.

Sasa hivi, kwa mfano, tafsiri ya neno ‘ajira’ siyo kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere – pale alipoanzisha mamia ya mashirika ya serikali na viwanda na kumwaga maelfu ya ajira kwa wananchi, sasa hivi ‘ajira’ ni uchuuzi wa barabarani wa vijana “wamachinga’ shughuli ambayo sasa hivi inahesabiwa na kutambuliwa rasmi na serikali, na hata waziri kusimama na kujigamba Bungeni kwamba serikali yake imefanikisha kutoa ajira.

Katika kulielezea suala la ajira Bungeni miaka michache iliyopita, aliyekuwa Waziri wa Kazi Gaudencia Kabaka alisema serikali baada ya kuruhusu sekta binafsi ambayo ndiyo inatengeneza ajira, basi jukumu la serikali linaishia hapo.

Kama nilivyosema vijana hawa wa barabarani hawakuomba hiyo kazi, wanalazimishwa na sera mbovu za elimu ambazo kila mwaka huzalisha malaki ya vijana wenye elimu duni.

Aidha uwepo wao barabarani unahusishwa na masuala ya kisiasa. Mwanzoni tu mwa utawala wa awamu ya Tano Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alianzisha mchakato wa kuwaondoa wamachinga barabarani, hususan kutoka katikati ya jiji, lakini Rais Magufuli alisema waachwe walipo kwani ndiyo waliompigia kura. Hata hivyo alisema wanaweza kuondolewa iwapo tu watapatiwa sehemu nyingine iliyo afiki. Maeneo mengine yaliyo afiki hadi sasa hayajapatikana na tatizo hili linazidi kukua siku hadi siku.

Kwa mtazamo wowote ule haya mambo ni ya kisiasa tu na tusisahau pia siasa ilitumika katika ujenzi wa “Machinga Complex” wakati wa utawala wa Awamu ya Nne na ndiyo sababu kuu ya kushindwa kwa malengo ya mradi ule. Uamuzi wa ujenzi wa majengo yale yaliyotokana na kilichoitwa ‘mabilioni ya Kikwete’ haukutokana na uamuzi wa kitaalamu na kiuchumi uliofanyiwa utafiti wa kutosha, bali ulikuwa ni wa kisiasa tu.