Home Maoni TUSIRUHUSU HOJA YA KUONGEZA MUDA WA UONGOZI IKOMAE

TUSIRUHUSU HOJA YA KUONGEZA MUDA WA UONGOZI IKOMAE

1896
0
SHARE

Upepo wa mabadiliko ya kisiasa (political wind of change) uliyoikumba dunia mwishoni mwa miaka ya 1980 ulioanzia Ulaya Mashariki, ulileta uboreshaji mdogo wa mifumo ya tawala za nchi kadhaa barani Afrika.

Mabadiliko hayo yalizikumba zile nchi zilizokuwa zimejikita katika utawala wa kidikteta hasa ukilenga chama au mtu mmoja.

Hali hiyo ilifungua milango ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi katika nchi mbalimbali na  Tanzania ikiwemo.

Hapo ndipo ilipoibuliwa hoja ya uwapo wa ukomo wa vipindi vya watawala katika nchi kadhaa hasa zile zilizokuwa na mfumo wa Rais mmoja kuongoza kwa muda mrefu. Tanzania ilisimama katika mfumo wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

Hii iliigwa kutoka mfumo wa utawala wa Marekani, ingawa wao ni vipindi viwili vya miaka nane vikigawanywa katika minne minne. Katika siku za karibuni mazuri yote haya yanaonekana kuelekea kutupwa kutokana na tama za baadhi ya viongozi wan chi za Afrika na duniani kwa ujumla.

Yapo mataifa tayari yameshaondoa ukomo wa utawala na mengine yanafikiria kufanya hivyo kwa sababu zile zile za kutaka kutawala kwa muda mrefu.

Tayari China imeshajiingiza kwenye tama hizo, hali ambayo imewashtua wengi ndani na nje ya nchi hiyo ingawa si kwa uwazi hasa kutokana na Taifa hilo kuwadhibiti wananchi wake kwenye mitandao ya jamii.

Utamaduni huu wa kuondoa ukomo wa vipindi vya urais uliowekwa kikatiba umekuwa ukishika kasi kama tulivyotangulia kueleza hapo juu tayari baadhi ya nchi za Afrika kama vile Uganda, Rwanda na Cameroon zimefanikiwa kufanya hivyo.

Zipo baadhi ya nchi zinakwama kutokana na kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi, nchi hizo ni Zambia chini ya Frederick Chiluba mwaka 2000/2001,  Namibia (Sam Nujoma) mwaka 2004, na Malawi (Bakil Muluzi) mwaka 2003 zilitamani kufanya hivyo.

Aidha ndugu zetu Zanzibar katika miaka ya mwishoni ya 1990 chini ya Rais Dk. Salmin Amour alitaka kufanya hivyo ingawa alikwama.

Hapa Tanzania tama za kufanya hivyo zimeanza kuwafikia baadhi ya wanasisa, mwaka janahoja kama hiyo iliibuka na Mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo mapendekezo hayo hayakuwa ya moja kwa moja ya kuondoa ukomo wa vipindi vya urais, bali ni kuongeza urefu wake kutoka miaka mitano ya sasa hadi saba.

Ingawa baadaye Mbunge huyo alitangaza kuiondoa hoja yake hiyo na hata Rais John Magufuli kutangaza kutokubaliana nayo, mjadala huo umekuwa ukiendelea, huku wengi wakiwa na hofu huenda ukaibuka tena.

Sababu ya kuendelea na wasiwasi ni kwamba hoja hiyo tayari inaonekana kupewa nafasi Zanzibar baada ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd kusema kuwa wazo hilo si baya na linajadilika.

Majaribio yote hayo yanaonekana kuwa mwanzo wa kufanikisha hoja hiyo ambayo inapingwa na baadhi ya wanasiasa. Mapema wiki hii mmoja wa wabunge wa CCM aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba hatua ya baadhi ya viongozi wa Afrika kuongeza muda madarakani lazima upingwe kwa nguvu zote, hasa na vijana, kabla haujaota mizizi na kusambaa.

Tunaunga mkono jitihada za kuipinga hoja hii dhalimu, ambayo kamwe haitakuwa na maslahi yoyote kwa Taifa letu bali itaturudisha tulikotoka.

Tunaamini watu walioweka ukomo wa uongozi walitazama zaidi maslahi ya nchi na si maslahi binafsi, hatuamini katika kuongoza kwa muda mrefu hata kidogo.

Kama mtawala ameshindwa kuleta mabadiliko ndani ya miaka mitano mpaka 10 anawezaje kuleta mabadiliko ndani ya miaka miwili au mitatu atakayoiongeza kutoka kwenye muda wa sasa wa kikatiba.

Ni vema wananchi na wabunge wenye nia njema na Taifa hili kusimama  kwa pamoja na kulipinga jambo hili vikali.