Home Maoni Tusitafute mambo yanayotugawa

Tusitafute mambo yanayotugawa

970
0
SHARE

WAKATI wa kampeni za uchaguzi mkuu, na baada ya uchaguzi uliomalizika Oktoba 25, 2015, RAI tulisistiza umuhimu mkubwa wa kuwa na Rais thabiti, jeuri na mwenye kusimamia maamuzi yenye manufaa kwa taifa letu. watanzania waliamua kumchagua John Pombne Magufuli kuwa Rais wa awamu ya tano. Nasi tuliungana na watanzania kuhakikisha tunasimamia haki ya kila mmoja na kulinda taifa letu.

Tuliamini kuwa baada ya Oktoba 25 kuna maisha mazuri na yenye furaha katika taifa letu, licha ya changamoto za hapa na pale. Vyama vyote viliwakilishwa vyema na katika nafasi ya urais na wa wagombea wakiahidi mambo mengi.  Tulikuwa na wagombea wengine kama  Dk. Godfrey Malisa (CCK), Janken Kasambala(NRA), Edward Lowassa (CHADEMA), Christopher Mtikila(DP), Chifu Lutayosa Chemba (ADC), na Macmilian Limo(TLP).

Wengine ni Hashim Rungwe(CHAUMA), Fahami Dovutwa(UPDP), wkaati kwa upande wa Zanzibar kutakuwa na Dk.Ali Mohammed Shein(CCM), Maalim Seif Sharrif Hamad (CUF).

Hatua hii ilionyesha namna wanasiasa walivyokusudia kuwawakilisha wananchi katika vyombo vya uamuzi. Lakini tulipoendeela katika mchakamchaka huo Taifa letu lilihitaji viongozi wenye uthubutu zaidi kuliko mipango mingi isiyotekelezeka.

Wagombea wote walitegemea ilani za vyama vyao, hivyo suala la vipaumbele walivyojinadi navyo havikuwa na nafasi yoyote. Rai yetu ni kwamba nchi inahitaji viongozi wenye uthubutu zaidi kuliko maneno. kiongozi ambaye atasimamia kwa haki bila kumwonea soni yeyote kwa kutuunganisha zaidi na kutupilia mbali yale yote yanayotugawa au kuleta mgawanyiko.

Tulihitaji viongozi wenye angalau nusu ya misimamo ya Mwalimu Julius Nyerere alivyoweza kuongoza idadi kubwa ya vijana waliokuwa wakipikwa kuwa viongozi na namna alivyoweza kutatua matatizo ya nchi.

Katika miaka ya uongozi wa Mwalimu Nyerere alionyesha umahiri wa juu katika uongozi. Ni jambo la fedheha kushuhudia viongozi wetu wakiachilia mgawnayiko mkubwa uliowahi kujitokeza wakati wa uchaguzi kuwa msingi wa kuenenda katika taifa letu.

Mgawanyiko uliojitokeza ulichangiwa na changamoto za kujitosheleza kwa wananchi binafsi na taifa kwa ujumla wake. kwamba taifa letu halikuwa na kiwango kizuri cha kujitosheleza kiasi kwamba wananchi waliona njia pekee ni kuhamishia hasira hizo kwenye uchaguzi uliopita.

RAI tunaamini kuwa taifa hili lingali na viongozi wenye kuthamini na kuyaona mambo mema kwa maslahi ya wananchi. Tunaamini kuwa wapo viongozi ambao wataweza kusimamia mambo yanayotuunganisha zaidi kuliko yale yanayotugawa.

Tunakumbuka kuwa wakati waMwalimu  Nyerere tulishuhudia mapambano ya maneno na uthubutu dhidi ya Nduli Idd Amini. Si hilo tu, tulishuhudia mambo kadha wa kadha kuhusu mustakabali wa viongozi wetu na taifa kwa ujumla.

Kwa namna nyingine utawala wa Nyerere ulikuwa imara sana kulinda misingi ya uongozi, maadili , kuunganisha wananchi na uchapakazi. Bahati mbaya tumeshuhudia wimbi kubwa la baadhi ya watanzania kushabikia migawanyiko ndani ya taifa letu. Tumeshuhudia baadhi yao wakiona fahari mgawanyiko badala ya mambo yanayotuunganisha.

Taifa letu limeshuhudia kasi ya ukuaji wa demokrasia pamoja na elimu ya uraia. Ukuaji wa demokrasia lazima uendane na ufahamu wa kutosha kwa wananchi ili kutambua viongozi wenye uthubutu na kulinda maslahi ya taifa, jamii na kuepuka migawanyiko.

Uthubutu wa kiongozi katika mambo hayo unakuwa na manufaa kwa taifa ambalo linajenga afya ya matumaini na kujiamini pawe na ukuaji wa uchumi. Uthubutu wa viongozi unasaidia kuboresha utendaji ambapo mtawala hasiti kuwachukulia hatua waokiuka miiko ya uongozi.

Kiongozi mwenye uthubutu huonekana tangu mwanzoni mwa kutafuta ridhaa ya wanachama na wananchi pia. Kwa mantiki hiyo ili kutambua nafasi ya uthubutu ni kuhakikisha wanachama wa vyama husika wanathubutu kutambua uthubutu wa muombaji wa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.

Ni wakati ambao wananchi, wafuasi wa vyama na wapenzi wanatakiwa kuungana na kuhakikisha wanatengeneza dira moja ya kutambua viongozi wenye uthubutu katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Nchi yetu si changa. Nchi yetu haikulaaniwa na Mungu kwamba iwe masikini. Bali uhaba wa kupata uthubutu kitendaji ndio kikwazo cha mafanikio yetu.

Ni rai yetu kwa wanachama wote, wapenzi wa vyama na viongozi wa dini na siasa pamoja na matabaka mbalimbali wanajenga utamaduni wa kuwahimiza wananchi kuyalinda mambo yote yanayotuunganisha. kuyajali mambo yote yanayotufanya tuwe kama taifa lenye amani na utulivu. Hilo litasaidia kuondokana na migawanyiko isiyo na ulazima ndani ya taifa letu.