Home Makala Tutampataje kiongozi wa aina ya JPM 2025?

Tutampataje kiongozi wa aina ya JPM 2025?

588
0
SHARE

NA GEORGE MICHAEL

KATIKA dunia hii iliyojaa kila aina ya dhuluma, chuki, ubeberu na mbinu chafu za kiuchumi (Accumulation of wealth by Nations), kila nchi huhitaji uongozi makini wenye mawazo mapana, misimamo na uzalendo wa hali ya juu.

Mataifa makubwa yamekuwa yakitumia vyombo vya ‘kimataifa’ kama Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kubeba agenda za siri za kiuchumi, kiusalama na kisiasa kwa malengo ya kuendelea kutawala dunia au maeneo fulani fulani yenye utajiri mkubwa.

Rejea sakata la Rais wa Marekani, Donald Trump kugoma kutoa fedha kwa IMF na China kuamua kuchukua mzigo huo wa kutoa fedha kwa shirika hilo ili kuweza kupambana na ugonjwa wa virusi vya Corona.

Mchezo huu wa Marekani na China wa kutafuta mamlaka ya kisiasa na kiuchumi hauna masilahi yoyote kwa Afrika zaidi ya kutafuta masilahi yao ya kiuchumi. China inatoa fedha hizo kwa malengo maalumu yapi?

Dunia haina umoja tena, Kenya anamfungia mpaka Tanzania, Zambia hivyo hivyo hata ambao hawajafunga mipaka si kwamba wanatupenda sana, hapana bali wanatutegemea  na wakifunga mipaka watakufa njaa.

Wamarekani wana msemo wao,”there is no a permanent friend and permanent enemy to America”, yaani hakuna rafiki wa milele wala adui wa milele. Rafiki yao Wamarekani ni masilahi yao ya pamoja kama Taifa.

Na sisi kama Tanzania tunahitaji tuishi katika falsafa hii, zile zama za kusema Kenya ni ndugu zetu sana zimepitwa na wakati. Mkenya ametuonyesha yeye ni nani kwetu na wengine wote waliotufungia mipaka.

Bahati mbaya sana, mipaka ya Afrika inachekesha sana, mpaka una vichochoro zaidi ya mia halafu unasema unafunga mpaka (lockdown).

Mfano mpaka wa Kasumulu Kyela (Malawi- Tanzania), una njia za panya zaidi ya 40 na watu wanapita kwa mitumbwi kupitia mto Songwe halafu unasema nafunga mpaka, Afrika bwana!

Labda nirejee katika hoja yangu ya msingi, wakati huu dunia itashuhudia mataifa yakitengana kuliko wakati wowote kutokana na sababu tofauti tofauti ikiwemo Corona na sababu za kiuchumi. Wakati huu uongozi wa Taifa lazima uwe wa aina ya kipekee kuweza kukabili changamoto za ndani na za nje.

Rais  John Magufuli amekuja katika wakati muafaka, ameonyesha kila aina ya uongozi katika kipindi hiki kigumu labda ndiye Rais pekee Afrika aliyefanya “visivyofanywa” na wengine.

Lazima akina mzee Benjamin Mkapa, Philip Mangula na wengine wajuzi wa mambo ya Taifa wafikirie aina ya uongozi utakaofaa kwa awamu ya sita, lazima tuanze kufikiria sasa.

Rais Magufuli katusaidia sana kutupa “model” mpya ya uongozi ndani ya Taifa letu. Rais Magufuli katufundisha kuwa ili taifa liwe imara linahitaji mtu/uongozi wa kariba yake.

Kwamba lazima iwe na “a leader of character (identify). Taifa linahitaji liwe na kiongozi mwenye ‘principles, standards na qualities’ ambazo ni hekima iliyotukuka, unyenyekevu wa hali ya juu, uaminifu, uthubutu (courage) na kumcha Mungu katika kiwango cha juu.

Pia kiongozi wa Taifa ili kwa wakati huu, lazima awe “a leader with presence” yaani katika hali yoyote lazima kiongozi aonyeshe yupo na kusiwepo na ombwe la uongozi. Ili kiongozi aonekane yupo lazima awe na mamlaka ya kuamuru na anapoamuru jambo lazima kifanyike kwa usahihi na wakati (commanding presence). 

Rais Magufuli ameonyesha uwezo mkubwa sana katika hili, watu wametumbuliwa kwa sababu ya kutofuata maelekezo ya uongozi kwa usahihi na kwa wakati.

Sifa nyingine ya kiongozi ajaye lazima awe anajua principle ya “quick recovery from feedback”. Kiongozi unapopata tatizo au kushambuliwa na adui, adui anaweza akawa njaa, Corona au tatizo lolote la Taifa ni lazima ufanye tathimini ya haraka haraka ili uweze kuchukua hatua sahihi na kwa uharaka (quick appreciation).

Kwa kufanya hivyo utapunguza ukubwa wa tatizo na utaondoa hofu katika taifa au jumuiya yako.

Sifa nyingine ni uwezo binafsi wa kiongozi husika kuyaona mambo katika uwanja mkubwa (intellectual capacity). Angalia JPM alivyoitazama Corona na hatua alizochukua, hakuangalia wengine wanafanya nini, bali aliangalia yeye ni nani kama kiongozi wa nchi na anapaswa kufanya nini.

Sifa nyingine ni utimilifu/utimamu wa akili ya kiongozi husika. Taifa lenye changamoto kama Tanzania haihitaji kiongozi mwenye “kichwa cha panzi” (mental ability) humfanya kiongozi aweze kufanya maamuzi sahihi hata kukiwa na kelele nyingi katika nchi kama Tanzania ambapo wapiga kelele wamejaa, unahitaji kiongozi ambaye ana utimilifu wa akili kuweza kufanya maamuzi na maelekezo sahihi.

Ni wakati huu ambapo Rais atajua kama viongozi wenzake chini yake kama wana sifa hiyo (mental ability) kwa sababu watu wakati wa matatizo kunakuwa na kelele nyingi na ni lazima, nasisitiza ni lazima wasaidizi wa Rais wacheze ngoma moja na Rais.

Sifa nyingine ya kiongozi wa nchi ni lazima awe na “sound judgement”. Maamuzi ya kiongozi wa juu lazima yawe sahihi na yachukuliwe katika wakati sahihi. Jeshini wana msemo wao “appreciation of the situation” yaani kufanya tathimini ya hali halisi kabla ya kufanya maamuzi.

Rais Magufuli hii anayo rejea maamuzi ya miradi ya kimkakati, rejea maamuzi ya sekta ya madini ya barrick, rejea maamuzi ya vyeti feki, rejea maamuzi ya wafanyakazi hewa. Kati ya yote aliyoanzisha hakuna hata moja aliloshindwa.

Sifa nyingine ambayo ni muhimu kwa kiongozi wa Taifa ni “domain knowledge” JPM kaonyesha ujuzi mkubwa wa eneo lake la kiutawala na kielimu. Magufuli anazungumza lugha zote za taifa hili. 

Hii ni sifa kubwa sana kwa kiongozi, hii inakupa uhalali wa eneo na watu unaowaongoza lakini pia JPM kaonyesha pia ujuzi katika eneo lake la kemia, hakuna unachoweza kumdanganya.

Sifa hii pia ni muhimu sana,”innovation”. Nani alijua kuwa leo hii machinga wangeweza kulipa kodi ya serikali? Nani leo hii hajui vitambulisho vya wajasiliamali? TRA wajuzi wa mambo ya kodi hawawezi wakafikiria nje ya kiongozi wan chi wenyewe wanafuata kilicho kwenye vitabu tu.

Tanzania tunahitaji mwendelezo wa watu kama Magufuli, kuna hofu kubwa hata kwangu pia kwamba Rais Magufuli akiondoka leo, tunaweza kuwapata watu wa kariba yake? 

Mwandishi ni mwalimu mstaafu na mkulima kutoka Tabora pia ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).