Home Habari Tutathimini mfumo wa vyama vingi vya siasa

Tutathimini mfumo wa vyama vingi vya siasa

916
0
SHARE

Na DK. HELLEN KIJO BISIMBA

HUU ni mwaka wa 27 tangu Tanzania irudie mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Wengi tunakumbuka mfumo huu ulivyorudishwa nchini baada ya kutokuwepo kwa karibu miaka 15 kama si zaidi. 

Ni kwanini nadhani tunahitaji tathimini? Ni kutokana na hali inayoonekana kuendelea nchini na kauli mbalimbali zinazojitokeza kwa viongozi na hata wasio viongozi.

Mwaka 1992, Katiba ilirekebishwa na kifungu cha 3 kifungu kidogo cha kwanza  kinasomeka ‘Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa’, kifungu cha pili kinaeleza kuwa; ‘Mambo yote yahusuyo uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini  yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo,’.

Bunge lilitunga sheria iliyo na tangazo la nchi yenye mfumo wa vyama vingi, sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992. Hii sheria najua imefanyiwa marekebisho mara kadhaa lakini haikufuta uwepo wa vyama hivi vingi vya siasa.

Tanzania imeandikisha vyama vya siasa kama 22 hivi baada ya kuukubali mfumo huu. Uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu umefanyika tangu mwaka 1995 na mwaka huu tunategemea uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka kesho 2020 uchaguzi mkuu yote ikifuata mfumo huu wa vyama vingi vya siasa.

Huu mfumo wa vyama vingi ni aina ya demokrasia ya ushindani wa kisiasa ili kuleta maendeleo katika nchi husika. Uwepo wa mfumo huu unasaidia na hata hapa kwetu umesaidia kukiangaliza chama kilichopo madarakani kwani vyama pinzani vimeweza kuibua mambo mbalimbaili ambayo yamekuwa hayaendi ipasavyo hivyo kurekebishwa kwa masilahi ya taifa kwa ujumla. Vyama hivi vingi katika siasa si ugomvi wala uadui bali ni ustaarabu wa kuendeleza nchi.

Hali inayofanya tujitathimini na kujitafakarisha ni kuwa kwa muda sasa vyama vya upinzani vinakosa kabisa haki ya kujumuika kuendeleza kazi zao.

Hivi karibuni nilimsikia msajili wa vyama hivyo akisema hakuna chama chochote kilichomtaarifu kuwa kimezuiwa kufanya mkutano. Huenda ni kweli hajataarifiwa rasmi kwa barua au kwa maandamano lakini huo ni ukweili unaoishi kwamba vyama hivyo haviwezi kukutana kwa uhuru kama inavyopaswa.

Kila wakati utaona kwenye mitandao ya kijamii au magazetini au vyombo vingine vya habari kuwa mkutano wa chama fulani umezuiwa pamoja na kutoa taarifa polisi.

Wakati mwingine utaona watu walio kwenye msiba wakiondolewa kinguvu ikisemekana kuwa ni wanachama wa chama fulani cha upinzani. Tumeshuhudia sasa hata mikutano inayofanyika ndani nayo ikiingiliwa na Jeshi la Polisi au kuzuiwa na watendaji wengine wa Serikali. 

Kuna wakati chama cha ACT-Wazalendo kilikuwa katika kufanya mkutano wake wa ndani kikaingiliwa na mkutano ukasitishwa, Chama cha Wananchi (CUF) nacho kiliwahi kukutwa na kadhia hiyo pamoja na vyama vinginevyo.

Wiki iliyopita nilishangazwa zaidi pale nilipoona mitandaoni taarifa ya  mkutano wa ndani wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) ulipopanguliwa kwa mabomu ya machozi huku mkutano wa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) ukizuiliwa.

Vilevile Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) naye kukamatwa na polisi huko mkoani Kagera akiwa kwenye mikutano ya aina hiyo.

Nikiangalia sana wanaokutana na madhila haya ni vyama vya upinzani tu maana sijaona mahali mikutano ya CCM ikizuiliwa au pengine ya kwao ikizuiliwa haitolewi taarifa.

Ukiacha kuzuiwa mikutano tumeona wabunge na wanachama wa vyama vya upinzani wakikamatwa na kuwekwa mahabusu huku wakifunguliwa kesi za kila aina.

Wengine wameshtakiwa hadi kufungwa jela kwa mwaka mzima au miezi kadhaa kabla ya kukata rufaa na kadhalika.  Tumeona Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alivyopigwa risasi karibu auawe , hatukujua aliyefanya vile na hadi leo hatujajua lakini alikataliwa kutibiwa na Bunge na wakati fulani mishahara yake ilizuiliwa na sasa amevuliwa ubunge kwa sababu zinazoogofya kuwa tumeshapoteza utu.

Huwa nafuatilia kuona iwapo makosa haya yanakuwaje yafanywe na viongozi wa vyama hivi vya upinzani tu na hasa vile vyenye sauti. Wale viongozi wa vyama ambao vyama vyao havina wafuasi wengi au  walio kwenye chama tawala wanaelekea kuwa malaika wasiokosea, maana hata malaika waliwahi kukosea wakaadhibiwa na muumba.

Kwa kukosa majibu ya haya yote nimeona nirudi kwetu wote nione uwezekekano wa kuutathimini huu mfumo. Nilimsikia Askofu mmoja akimwandikia Rais akihoji hii hali hasa kwa kile alichoona ni polisi kutumiwa kuuingilia utendaji halali wa vyama hivi upinzani.

Mimi naona sisi Watanzania kwa ujumla wetu tujitafakari kwanini huu mfumo upo, je unatufaa au hautufai na kama unatufaa tufanyeje ufanye kazi ipasavyo na kama hautufai tufanyeje kuondokana nao kisheria na kiutaratibu bila kuumiza mtu.

Nilimsikia mbunge mmoja wa chama cha upinzani akizungumza na Watanzania kwa uchungu kuwa wao wapinzani hawakuingia kwenye upinzani kwa faida zao binafsi na wanaweza wote wakaamua kuingia chama tawala wakatulia huko mambo yakaendelea lakini hilo sio lengo. Wale waliopambana hadi mfumo huu ukarudi walikuwa na sababu ambazo hazina maana tena?

Mimi kwa mtazamo wangu sioni kwanini watu wapitie mateso katika kufanya kazi iliyopo kisheria katika nchi huru kama hii ya kwetu. Pengine ni kwa vile mimi si mwanasiasa ingawa ni mfuatiliaji wa karibu wa masuala ya kisiasa.

Haya yanayowapata hawa walio katika baadhi ya hivi vyama vya upinzani, waliyapitia wapigania uhuru waliokuwa wakipambana na wakoloni, haipendezi kwa watu walio kwenye nchi huru iliyokubali mfumo huu kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Iwapo hata mmoja wao angekuwa ndugu yangu au ndugu yako, ni rahisi kumwambia ‘acha ukae katika chama ambacho hubughudhiwi’, maana wale wanaohamia chama tawala tunaona wanavyopewa vyeo .

Watanzania kwa asili ni watu wastaarabu  wenye upendo lakini ikifikia mahali watu wanaona sawa Mtanzania mwenzao aumie asishughulikiwe kwa sababu zisizo wazi au za kisiasa, iwe ni shida kumwona Mtanzania mwenzako aliyepatwa na shida kama kuwekwa rumande au kuwa mgonjwa.

Hapa tutakuwa tumekwenda mbali sana kiasi kwamba ni lazima tuhoji polisi wanapodiriki kuwapiga wanawake wasio na silaha, mabomu ya machozi kuwafurumua kutoka mkutano halali ili iweje na ni kwa faida ya nani?

Sisi watazamaji tunaangalia tu na tumenyamaza kimya au tunagugumia kwenye mitandao ya kijamii au vyumbani mwetu kwa nia gani hasa? Watu wengine wanasema wangetamani kusema lakini wanajiogopea.

Tukiwa tunaogopa kusema yanapomkuta mwenzetu nani atatusemea yakitukuta. Hatujaacha kuwa wananchi wa Tanzania na sidhani kama tuna mpango wa kuihama hii nchi nzuri kiasi hiki.

Kinachohitajika tujitathimini sisi wote kila mtu ana nafasi ya kutathimini. Iwapo unaona yanayoendelea ni sawa wasaidie wale wanaoona kuwa si sawa. Iwapo unaona si sawa tafuta jawabu la nini kifanyike. 

Mimi nimeanza kwa kushauri tufanye tathimini ya mfumo huu kama ilivyofanya Tume ya Hayati jaji Nyalali mwaka 1991. Tuunde tume tena iliyo huru tujitathimini na tupate njia inayofaa kuiendea.

Hao wanaopata misukosuko ni watanzania kama sisi na huenda ni jamaa zetu haipendezi.