Home Makala Tutokomeze ujinga kuelekea Tanzania ya viwanda

Tutokomeze ujinga kuelekea Tanzania ya viwanda

1593
0
SHARE

Na CHRISTINA GAULUHANGA

DAR ES SALAAM

WAKATI dunia ikiendelea kukua katika matumizi ya teknolojia, bado kuna kundi kubwa la watu ambalo limeachwa nyuma na kusahaulika katika nyanja mbalimbali kama vile elimu na uchumi.

Kundi hilo ndilo lililosababisha Serikali kuamua kuanzisha sera ya utoaji elimu bure huku ikiwekeza katika ujenzi wa madarasa na kuongeza idadi ya shule za kata ambazo zimesaidia kwa kiasi kikubwa vijana wengi kupata elimu ya sekondari na hata vyuo kutokana na familia nyingi kutomudu kuwaendeleza watoto wao kielimu.

Hapo awali jamii kubwa ya watoto, hasa wale wenye kipato cha chini walikuwa wakiishia darasa la saba kutokana na kushindwa kumudu gharama za ada na michango mingine, lakini kwa sasa wengi wao angalau wameweza kunufaika na elimu ya sekondari na wengine hadi kufikia vyuo.

Zipo taasisi na mashirika ya kiserikali na binafsi ambayo yaliona athari za ukosefu wa elimu hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inapambana kuelekea kufanikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Taasisi ya Sos Children’s Village ni miongoni mwa wadau ambao wamefanya jitihada kuhakikisha kila mtoto au kijana anapata nafasi ya kwenda shule kama njia mojawapo ya kumkomboa kutoka katika umasikini.

Mratibu wa Programu ya Kucheza na Kujifunza wa taasisi hiyo binafsi, Sarafina Lelo, anasema ni bora kuwaendeleza kielimu watoto waliokosa elimu ili kuwaepusha na mazingira hatarishi.

Anaiasa jamii kutumia fursa ya Mpango wa Elimu kwa Watoto Waliokosa (MEMKWA), ili waweze kunufaika nao.

Taasisi hiyo iliyoanzishwa rasmi  mwaka 2017, imekuwa ikiendesha mafunzo mbalimbali ikiwamo mradi wa kucheza na kujifunza.

Sarafina anasema mfumo huo umesaidia kubadili maisha hasa kwa wananchi waishio vijijini ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji ambao watoto wao hapo awali walikosa fursa nyingi za elimu.

“Wapo watoto wengi mitaani ambao wamekosa elimu hivyo ni vyema walimu, wazazi na viongozi wakawafichua na kuwapa haki zao za msingi,” anasema Sarafina.

Ili kuhakikisha watoto wengine wanapata fursa ya kwenda shule wamekuwa wakishirikiana na maofisa maendeleo pamoja na walimu kuwatafuta wanafunzi waliokosa elimu kisha kuwaendeleza kupitia madarasa ya MEMKWA.

Kwa Dar es Salaam, mradi huo unaendeshwa katika maeneo ya Zingiziwa na Chanika, Wilaya ya Ilala, ambapo pamoja na mambo mengine wamekuwa wakitoa elimu kwa wakufunzi wa madarasa ya MEMKWA ili kuwajengea uwezo wa kukabaliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

“Tangu kuanzishwa kwa madarasa ya hayo tumetoa kwa mara ya kwanza mwaka huu mafunzo ndani ya Manispaa na yameleta motisha kwa walimu kwani wanafunzi wengi wao, ni wale ambao wamepita kwenye changamoto mbalimbali hivyo walimu wanaowafundisha ni lazima nao wawe na dhamira ya dhati,” anasema Sarafina.

Anasema pia wamekuwa wakijenga miundombinu ya vyoo na madarasa ambapo ili uimarisha mahusiano mazuri ya kielimu wamefungua  klabu 10, ambazo huwasaidia watoto kufahamu haki zao hasa za kielimu ambapo tangu waanze wameona mabadiliko makubwa ya kielimu.

 Sarafina anasema pia wamekuwa wakiendesha mradi wa malezi mbadala kwa ajili ya kuwaimarisha familia.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi huo,  Elamu Kayange, anasema mafunzo hayo shirikishi yatasaidia kuwa kivutio kwa watoto kujifunza na kuelewa haraka, na kwamba malengo ya mradi ni kuwafikia walengwa 1,000 katika hizo mbili.

Anasema takwimu za manispaa hiyo zinaonesha kuwa wapo watoto 471 wa darasa la nne na 145 wa darasa la saba ambao wanafanya mtihani mwaka huu.

Mkurugenzi wa SOS, David Mulongo, anasema nchi 138 zinatekeleza mradi huo.

Naye,  Ofisa Elimu Vielelezo Manispaa ya Ilala,  Amina Maulid, anasema ipo haja kwa walimu wa MEMKWA kupata mafunzo ya mara kwa mara kwa kundi la walimu wa madarasa hayo limesahaulika na halipewi kipaumbele kama walimu wengine jambo ambalo linaweza kurejesha nyuma jitihada za wadau.

Naye, Meneja Mradi huo, Kayange, anasema mwamko mdogo wa wazazi kukubali kuwapeleka watoto wao katika madarasa ya MEMKWA ni miongozi mwa changamoto zinazowakabili.

Kayange anasema wamekuwa wakiwatumia maofisa ustawi wa jamii kuwakusanya watoto hao lakini hata hivyo wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi ikiwamo baadhi ya wananchi kukosa uelewa wa umuhimu wa elimu.

“Naiomba jamii itusaidie kuibua kundi la watoto waliokosa elimu ili tuweze kuwawezesha kielimu kwani itasaidia kuwaondoa katika lindi la umaskini,” anasema Kayange.

Katika utafiti usio rasmi walioufanya, wamebaini watoto wa kundi hilo wengi wao wamepita kwenye mazingira hatarishi hivyo kuna kila sababu ya kutumia nguvu kubwa kuwashawishi kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ili na wao waone umuhimu wa elimu.

“Watoto hawa wengi wao wamelelewa kwenye mazingira hatarishi na baadhi yao wanatamani kurudia darasani lakini changamoto waliyonayo ya kimazingira inawakwamisha wengi hivyo jitihada zinahitajika,” anasema.

Pia anawaomba wadau kujitokeza kushirikiana na serikali katika jitihada za kuondoa ujinga ili kufikia malengo ya uchumi wa viwanda ambapo elimu  na ubunifu zaidi vinahitajika katika kuendeleza viwanda hivyo.