Home Makala Tuudumishe Muungano ulete tija zaidi kwa pande zote

Tuudumishe Muungano ulete tija zaidi kwa pande zote

1759
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA

NI MIAKA 55 sasa tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uasisiwe Aprili 26,1964. Watu waliozaliwa wakati huo kwa sasa wanaelekea uzeeni.

Hapana shaka yoyote, Muungano huu umekuwa kielelezo thabiti cha amani, maendeleo ya kisiasa na kiuchumi kwa Bara na visiwani.

Wananchi wa nchi hizi mbili ambazo sasa zinatambulika kama nchi moja, wamekuwa na ushirikiano wa hali ya juu kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuoleana.

Wa bara wamekuwa wakifanya shughuli zao Zanzibar, halikadhalika wale wa Zanzibar nao hufanya hivyo hivyo, kwetu hili ni jambo jema na la kupigiwa mfano.

Tunaamini siku zote muungano ni kitu kizuri, jamii inapoungana maana yake inakuwa na nguvu kubwa ya pamoja.

Tunatambua zipo changamoto kadhaa katika kuungana na hata Muungano huu mkongwe nao unazo changamoto zake.

Miaka 30 kulikuwa na nchi kadhaa zilizoungana, kama vile Muungano wa Kisoviet (Soviet Union) ulioasisiwa mwaka 1922 na kuziunganisha nchi 15, ulisambaratika kwa vile ulikuwa muungano wa mabavu.

Kusambaratika kulisukumwa na ujio wa siasa ya uwazi (glasnost) — siasa ambayo ilianzisha utaratibu wa serikali au taasisi za umma kuwajibika kwa wananchi, kuwapa uhuru zaidi wa kupata habari, kutoa maoni na kwenda wanakotaka.

Kutokana na tawala za Kisoviet zilizotangulia kubinya uhuru wa watu wake, nchi kadhaa zilizokuwa ni sehemu ya Jamhuri za Kisoviet, ziliamua kujiondoa kwenye Muungano na kujiunga na Muungano wa Ulaya (EU).

Muungano mwingine uliopo huko Ulaya ni Umoja wa Ulaya (EU) ambao ulianzishwa na nchi sita mwaka 1958 kwa Mkataba wa Roma na sasa una wanachama 28 ingawaje Uingereza iko katika mchakato wa kujitoa. Muungano huu ulilenga kuwafaidisha wanachi wote wa Ulaya kwa kuwa unafungua milango ya fursa nyingi.

Katika miaka yote ya Muungano wetu, kumekuwa na kitu kinachosemwa tangu uwasisiwe — kero za Muungano — hadi leo hii, miaka 55 tunawasikia wanasiasa wakizungumza kero hizo za Muungano. Tume ya Jaji Warioba ilikuja na mapendekezo murua ya kumaliza kero hizo, bahati mbaya mchakato wa Katiba Mpya haukumalizika na kero zinaendeelea kuwapo.

Lakini tuseme tu kwamba dunia inawashangaa Waingereza kwa kukubali kurubuniwa na kuchagua kujitoa kutoka EU bila kufikiria madhara yake yatakuwa ni nini. Nchi zikiungana zinakuwa na nguvu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Tanzania ni nchi changa na bado hatujapata maendeleo makubwa.

Ili tufanikiwe, ni lazima tutafute mbinu za kisiasa za kutuunganisha, ili tuwe na sauti moja katika masuala mbali mbali — hasa yanayohusu mambo ya nje. Ipo haja ya viongozi wetu wa Tanganyika na Zanzibar, kukaa upya na kukubaliana ni mambo gani yafanyike ili muungano wetu upate sura mpya na kuondoa kabisa mambo ambayo yanatukera na hatimaye tuzizike hizo kero za Muungano.

Viongozi wetu kila mara wanasema wametatua baadhi ya kero za Muungano, lakini bado kuna kutoridhika kwa wanasiasa wa pande zote kuhusu muundo wa Muungano. Waache kupigapiga maneno, wakilitatua hili, tunaamini mengine yote yatakuwa rahisi.

Muundo mpya wa Muungano ndiyo utakaoainisha nini kifanyike kwa upande wa Zanzibar na kwa Tanganyika. Mgawanyo wa mamlaka na madaraka kwa pande zote mbili na mahusiano yetu na nchi za nje na mashirika ya kimataifa.

Usajili wa vyombo vya moto, hisa za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, Tume ya Pamoja ya Fedha, utaratibu wa kuchangia gharama za Muungano, siyo mambo yanayowahusu wananchi moja kwa moja.

Sisi kama raia wa Tanzania, tunataka Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isiwabane wananchi, iwape uhuru zaidi wa kufanya biashara bila kujali nani anatoka upande gani. Isawazishe uwanja wa biashara, iondoe vikwazo vya ushuru, hasa kwa mazao ya wakulima.

Uwazi wa kibiashara utaondoa suala la njia za panya na magendo kupitia bandari bubu. Serikali zetu zikubaliane kwamba uhuru wa mawazo na uhuru wa wananchi kuhoji, kufanya siasa ni wajibu wao — pamoja na uhuru wa kupata na kutoa habari. Haya ndiyo mambo ambayo yatawafanya wananchi kuuenzi Muungano.