Home Maoni TUWALAZIMISHE WANASIASA WABADILIKE

TUWALAZIMISHE WANASIASA WABADILIKE

2169
0
SHARE

Mwananchi akipiga kura

 

MIONGONI mwa mambo yanayonitatiza, ni uwasilishaji wa hotuba, au michango ya baadhi ya wanasiasa nchini. Pengine si hotuba tu, bali namna ambavyo mfumo mzima wa kisiasa tulionao nchini.

Aghalabu imezoeleka kwa wanasiasa kutumia maneno ambayo hayana tija kwa wapigakura wao. Wanapigania maeneo ambayo hayagusi maisha ya wananchi. Wanaimba kila aina ya santuri, ilimradi waweze kusikika.

Mathalani, unatazama televisheni au unasikilzia redio, au unapokutana nao ana kwa ana, halafu unamsikia mwanasiasa anakosoa jambo kwa kusema “huyu kiongozi, au mwanasiasa ni mpuuzi tu, anakiuka taratibu za uendeshaji wa taasisi fulani”.

Wengine kutoka chama tawala wanatuambia wananchi kuwa wale wanasiasa wa chama cha upinzani ni ‘malofa na wapumbavu’ kwa hiyo msiwachague, badala yake tuwachague wao na chama chao.

Au mwanasiasa kutoka chama cha upinzani anaweza kumkosoa mwenzake wa chama tawala, “Aaah huyu mwanasiasa ni fala sana.”

Maneno ya aina hiyo yamekuwa mengi. Staili ya uwasilishaji wa wanasiasa wetu nchini licha ya mipasho au vijembe (Jibe kwa Kiingereza), bado tunakabiliwa na tatizo kubwa la uwasilishaji wa mawazo mbadala.

Hata tunapowasikiliza kwenye mikutano ya kuomba kura ni rahisi kubaini kuwa hawana ajenda au mambo yaliyopaswa kuzungumzwa miaka 20 iliyopita yanaendelezwa leo.

Ni rahisi kuona ahadi ambazo za dhahiri unabaini ni uongo mtupu. Kuna desturi za kuwaambia wananchi masimulizi ambayo yamekuwa mazoea na yamejenga utamaduni bandia (kwa sababu yanapaswa kubadilishwa).

Sasa basi, kwenye suala la mabadiliko ndani ya nchi hii yanapaswa kuanza na wanasiasa wenyewe kwenye mwenendo wao wa kila siku kuendesha siasa kwa ujumla wake, au walazimishwe kubadilika kwa kukataa mashuhudu yao.

Fiona Kamikazi, raia wa Rwanda, amewahi kuniambia maneno haya: “Mimi sihitaji mgombea ambaye atakuja kuniambia habari za mauaji ya Kimbari ya 1994, au habari za huzuni kuhusu hali iliyotokea dhidi ya Watutsi. Nataka mgombea ambaye ataniambia habari za uchumi na maendeleo. Mgombea ambaye ataniambia stori za kuboresha huduma na ufanisi wa kiuchumi wa nchi hii. Mgombea atakayeweza kuuambia ulimwengu stori za mafanikio ya uchumi yaliyopo na tuendako.”

Hapo ndipa hoja yangu inapojikita. Kwa mfano, mwanasiasa kusema kundi la wenzake ni ‘wapumbavu na malofa’ linaihusuje jamii? Kauli kama hizo kwenye kampeni za urais, ubunge, na udiwani zinapanga kuboresha vipi maisha ya wananchi?

Kwamba ukishashusha kijembe hicho basi unahitimisha hotuba na watu washangailie kana kwamba inawasaidia chochote katika maisha yao?

Aidha, mwanasiasa mwingine anamwambia mwenzake, kuwa anashindwa kuendesha taasisi fulani sababu yeye ni fala. Je, kauli kama hiyo inatusaidiaje sisi wananchi? Je, huyo fala anakosea nini? Je, hoja ya mtoa maneno kama hayo ni ipi?

Katika ulimwengu wetu huu lazima tufahamu kuwa hata wale ambao wanatusikiliza kwenye mikutano yetu, wanao uwezo wa kuelewa mantiki zinazowasilishwa. Wananchi waliopaswa kuambiwa maneno ya fala au wapumbavu na malofa, ni wale wa karne ya 18 huko.

Lakini kwa kizazi hiki cha Kitanzania, ni lazima tuwaambie, kwa nini tunawapa madaraka. Ni lazima tukubaliane na rafiki yangu Fiona kuwa zama hizi hatupaswi kuwambia watu juu ya habari za vijembe ambavyo vinachukua 99 ya hotuba za wanasiasa.

Ulimwengu wetu unakabiliwa na changamoto nyingi. Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo, na inatakiwa kuwambia wananchi kuwa hakuna jambo zuri kama kuongelea masuala.

Kwamba mwanasiasa anapanda jukwaani anawaambia wananchi kuwa, “Tanzania ni nchi mojawapo barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara yenye matumizi ya chini sana ya mbolea katika ngazi ya wakulima wadogo (smallholder farmers). Kwa sasa Tanzania imefikia kiwango cha kilo 19 tu za virutubisho kwa hekta, yakiwa ni matumizi madogo mno kwa viwango vya dunia, mfano nchi ya China ina wastani wa matumizi ya kilo 210 kwa hekta moja (Utafiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Julai 2017).

Huu ni mfano wa dhahiri ambao mwansiasa anatakiwa kuzungumzia kokote anendako. Awaambie wananchi (ambao kwa kiasi kikubwa sasa kiwango cha uelewa wa wapigakura kimekua zaidi, hususani wapigakura waliozaliwa miaka 1990 kuelekea karne ya 21).

Wapigakura wa namna hii sio wa kuwaletea vijembe pekee, bali wanachambua maudhui ya hotuba zenu na kuweka mizani.

Haiwezekani katika karne ya 21 mwanasiasa anatumia dakika nyingi kushusha vijembe na kuondoka kisha akaita huo ni mkutano wa hadhara. Badala yake sitakosea nikisema hakuna tofauti na vijiwe vya kahawa kwenye mikutano mingi ya wanasiasa nchini.

Mwasiasa anakwenda kuzungumza na wananchi wa Lindi, anatakiwa kujua changamoto zilizopo hapo. Anakwenda kuzungumza na wananchi wa Songea anatakiwa kujua hatima ya kilimo na kiwanda cha tumbaku. Anatakiwa kujua suala la masoko ya mahindi na kahawa pia.

Mwanasiasa akienda Mtwara, anatakiwa kujua kinachoendelea katika suala la zao la korosho. Mwanasiasa akifanya ziara mjini Tukuyu, mkoani Mbeya, anatakiwa kuzungumzia maendeleo ya biashara ya ndizi na mpunga kwa wakulima.

Anatakiwa kujua changamoto za biashara kati ya Tanzania na Malawi. Anatakiwa kujua hali ya utalii katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, na jirani zao Malawi.

Mwananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, anataka kutatuliwa changamoto za zao la Pamba, hahitaji ngonjera zisizoingiza chochote kwenye akaunti yake benki.

Mwananchi anahitaji kujua madini yanachangia vipi huduma za jamii na kumfikia alipo, si kuambiwa ‘lofa, pumbavu, fala au anaongoza bila kufuata taratibu halafu huelezi doasari hizo ni zipi’. Halafu unataka ushangiliwe?

Mwanasiasa wa kizazi kipya anatakiwa kuzungumzia habari za uchumi na maendeleo. Habari za ufanisi wa miradi na utekelezaji wa mikakati.

Mwanasiasa wa kizazi kipya anatakiwa kujua kuwa habari nazo huamua hatima ya upigaji kura. Ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii limechochea ukubwa wa upatikanaji wa habari.

Maeneo ambayo hayakuwahi kufikiwa na wanasiasa wayazungumza wananchi wenyewe kupitia soko la habari. Wananchi wakija kukusikiliza mwanasiasa hakikikisha huleti habari za “tunapigana kila njia kuhakikisha kesi ya mwanasiasa fulani aliyeguswa mkono kwani ameingiliwa,”.

Habari za namna hii sitasita kuziita upuuzi usio na manufaa yoyote kwa wapigakura.

Mpigakura wa kizazi hiki kinachozidi kubobea kwenye uelewa, hawezi kuendelea kunufaishwa na vijembe au mikwara bubu ambayo haina msaada wowote katika maisha yake.

Haiwezekani mwanasiasa akipiga porojo za kuguswa mtu fulani mwilini mwake, halafu katika jimbo, kata, kijiji au taifa, hakuna utekelezaji wa miradi, shughuli za maana hazipewi kipaumbele.

Wananchi wanataka maji safi sio vijembe. Wananchi wanataka kujua mambo ya uchumi, deni la taifa linapaa, hali ya maisha ikoje na mwelekeo wa uchumi wa nchi unakwenda wapi.

Mpigakura makini wa kizazi hiki, anatakiwa kujua sera ya nchi, chama, mwanasiasa au asasi yoyote kuelekea ujenzi wa Tanzania yenye nguvu ya mlo, siyo ‘sifa zisizo na maana. Ndiyo maana nasema tuwalazimishe wanasiasa kubadilika. Tuwalazimishe, na matunda yake yanakaribia. Tuendako 2020 tutaongelea uchumi na maendeleo tu.

Mungu ibariki Tanzania.

Baruapepe; mawazoni15@gmail.com