Home Habari Tuwatakie heri watahiniwa kidato cha nne mwaka 2019

Tuwatakie heri watahiniwa kidato cha nne mwaka 2019

1220
0
SHARE

DK. HELLEN KIJO BISIMBA

JUMATATU wiki hii, wanafunzi wa kidato cha nne walianza mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari.

Kabla ya kuanza mitihani hiyo, walifanyiwa mahafali na kutunukiwa cheti cha kumaliza elimu yao ya kidato cha nne.

Wanafunzi wote waliofikia hatua hiyo wanastahili pongezi sana kwani wapo wenzao walioanza nao ambao waliishia njiani huku wengine wakiishia kidato cha kwanza kwa sababu mbalimbali.

Hawa waliofikia hatua hii tunawatakia heri katika mitihani yao ili waweze kufaulu vizuri na ikiwezekana waendelee hatua ya juu zaidi na hata watakaomalizia hapo wawe na upeo utakaowawezesha kuendesha maisha vizuri.

Ninapowatafakari hawa wanafunzi wanaofanya mitihani, ninasikia sauti nyingi za watu wanaozungumzia elimu ya sasa na utofauti wake na elimu ya wakati uliopita.

Wahitimu wengi wa wakati huu wanapata shida hata ya kuandika barua tu. Sasa hivi wanafuatilia sana ufaulu wa

shule na nafasi ya shule katika wilaya, mkoa hadi taifa. Hili ni jambo zuri isipokuwa wengine hupata hizo alama nzuri sana, lakini wanapofika kuitumia hiyo elimu inakuwa kama vile hawakuelimika kabisa.

Swali linakuja ni wapi wanapokosea waelimishaji na waelimishwaji? Kwa vile mkazo ni kufauu mitihani mara nyingi wanafunzi hukaririshwa badala ya kuelimishwa.

Hivi karibuni yupo mtu aliandika swali kwenye mtandao wa kijamii akiuliza hivi ni nani amewahi

kutumia Kigawe Kidogo cha Shirika [KDS] na Kigawo Kikubwa cha Shirika [KKS], muuliza swali alisema yeye aliona alipoteza tu muda kusoma hivyo vigawo na vigawe lakini haoni kabisa anavyovitumia. Ukweli ni kuwa hizo hesabu za vigawe vina matumizi katika maisha ya kila siku lakini wakati watu wanapofundishwa havihusiani kabisa na hali halisi ya vinavyoweza kuwa vinatumika katika maisha ya kila siku.

Mfano mzuri ni wakati wa uandikishwaji katika daftari la kudumu la wapiga kura. Ili kujua muda utakaohitajika ilibidi kujua idadi ya watu walio na sifa za kuandikishwa katika eneo husika na muda unaohitajika kuandikisha mtu mmoja ili kujua kwa idadi iliyopo kutahitajika siku ngapi kukamilisha zoezi. Ukiangalia hapo hakuna neno kigawe wala kigawo lakini katika kufikia jibu utakuwa umetumia vigawe au vigawo.

Swali hilo hapo juu, lilinikumbusha jinsi nilivyokuwa hodari wa kukariri masomo ya Fizikia na Kemia kidato cha kwanza na cha pili, lakini nikawa najiuliza hivi maana ya haya ninayokariri ni nini.

Nilikuwa naijua vizuri sana Ohm’s Law ambayo niliweza kuiimba kwa kichwa kwa lugha ya Kiingereza ‘The current flowing in a conductor is directly proportional to the potential difference across its ends provided the physical conditions and temperature of the conductor remains constant’.

Wakati nakariri sikuwa najua kabisa kuwa hii sheria inahusiana na masuala ya umeme na kwamba kama nikiielewa vizuri ninaweza kujielekeza kuwa mhandisi wa umeme.

Kutokana na hali hiyo, niliamua kuwa sitasoma Fizikia wala Kemia kidato cha tatu na kuendelea kwani sikuona vinanisaidiaje, nikaamua kusoma sayansikimu, kupika na kushona.

Nilibahatika baadaye nilipokuwa mtu mzima kuwa mgeni rasmi katika shule moja ya wasichana huko Lushoto Mazinde Juu. Wanafunzi walikuwa wanaonyesha stadi mbalimbali. Jambo

nililoliona tofauti ni jinsi mwanafunzi mmojawapo alipoeleza vizuri sana sheria ya kutanuka na kunywea katika Fizikia.

Alielezea inavyoweza kutumiwa na wajenzi wa barabara au wa majengo. Niliona hapa mtu akielewa hivyo ni rahisi sana kuwianisha na maisha halisi na kuamua kulifuatilia somo hilo kwa vile mtu anaona kabisa uhusiano wa anachojifunza na uhalisia katika kukitumia.

Nikaona kuwa hata mimi nilipojifunza Ohm’s law kama ningeelewa hasa maana yake huenda ningevutiwa na hilo somo.

Sasa tukirejea kwa hawa watahiniwa wetu ambao wengi wanakaririshwa karibu kila somo bila kuelewa lina uhusiano gani na kile atakachokuja kufanya ni vyema kabisa turejee mitaala yetu, turejee mbinu za ufundishaji, turejee maana ya elimu.

Kuna wakati walimu wanahangaika sana ili tu wanafunzi wafaulu kwa kiwango kikubwa na shule ipate sifa na hata mwalimu wa somo apate sifa na wakati mwingine walimu wapate bakshishi bila kujali iwapo wanafunzi hao wamefaulu kweli au wamefaulu ukariri.

Kuna wakati tunasikia baraza la mitihani limefuta matokeo ya shule au ya wanafunzi kutokana na udanganyifu. Udanganyifu huu wakati mwingine unafanywa si na wanafunzi peke yao bali wapo walimu wasio na maadili na wasiojiamini katika kufundisha kwao kiasi cha kudiriki kufundisha wanafunzi mitihani au hata kuwaandikia mitihani.

Ufaulu wa alama bila mtu kuwa na elimu ya kile anachosemekana kafaulu ni tatizo kubwa sana katika jamii yetu. Watu wanakuwa na alama ‘A’ katika somo la Kiingereza lakini mtu huyo huyo hawezi kusema sentensi moja ya Kiingereza iliyonyooka. Hii ‘A’ aliipata vipi? Wapo wabunge wetu ambao kwa muda mrefu wanapambana ili serikali yetu iangalie mfumo wetu wa elimu na mitaala tuliyonayo iboreshwe na iwasaidie wanafunzi kujifunza na kuelewa kwa kiasi cha kuweza kuitumia hiyo elimu katika maisha yao ya kila siku baada ya shule.

Tukiwa na mitaala inayoangalia hali halisi na tukifahamu kuwa uwezo wa Serikali ni kuelimisha wanafunzi hadi kidato cha nne, basi elimu hiyo ya kidato cha nne iwe itakayowawezesha wahitimu kufanya mambo ya kujiendesha wamalizapo shule kwa kiwango hicho.

Mwanafunzi asimalize kidato cha nne na asipoweza kuendelea kidato cha tano au kupata elimu ya vyuo basi

awe kama tu hajawahi kupata elimu. Kuna wakati wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi iliyokuwa mwisho darasa la nane, walikuwa na upeo na uwezo wa kufanya mambo mbalimbali katika kujiendeleza kimaisha.

Pia pangeweza kuwa na mgawanyo wa mitaala kwa sehemu watu wanapotoka na maisha wanayoyaishi. Eneo watu wanapojikimu kwa uvuvi pawe na masomo yanayoelekeza uvuvi bora, wanapolima kahawa au korosho kilimo bora cha aina hiyo ili anapohitimu aweze kutumia elimu hiyo kuendeleza maisha hapo alipo.

Wahitimu wengi wanaposubiria matokeo yao hawaangalii sana wanachokijua kwa uhitimu wao,

lakini matokeo yatakuwa na alama zipi. Zile alama ni nzuri sana ila zingekuwa nzuri zaidi iwapo zingelingana na elimu iliyopatikana kulingana na alama hizo. Wale wote wanaojaribu kuwaibia wanafunzi mitihani, kuwafanyia mitihani au kuwalazimisha wenye uwezo wawafanyie wasio na uwezo mitihani wote hao, hawawatakii heri wahusika kwani ukimpa mwanafunzi majibu ya mtihani hutamsaidia kujua yale anayopaswa kujua.

Hivyo basi tunatakiwa kuwa na mitaala

mizuri, walimu wajibidiishe kuwafundisha wanafunzi kuelewa wanachofundishwa na kisha

kujiamini katika kufanya mitihani ili hata kama wamepata alama zisizong’aa sana bado wawe wana utofauti katika elimu waliyoipokea miaka walipokaa shuleni.

Sifa zisiwe za ufaulu wa alama tu bali wenye alama walivyofanikisha maisha kutokana na alama hizo na si vinginevyo.

Wanafunzi wote wanaofanya mitihani nao wanapaswa kujiandaa vya kutosha ili wasishawishike kuambiwa majibu, waonyeshe walivyojiandaa na wafanikiwe katika mitihani yao na hata wanapoendelea mbele katika maisha yao ya kila siku. Kila la heri watahiniwa wote wa kidato cha nne 2019.