Home Makala TUZO KICHOCHEO CHA KULINDA MTO RUAHA

TUZO KICHOCHEO CHA KULINDA MTO RUAHA

763
0
SHARE

NA FRANCIS GODWIN, IRINGA


MASHINDANO ya Tuzo ya Uhifadhi wa Mazingira yanayoratibiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa  (TANAPA) kwa  mikoa ya  Mbeya, Njombe na  Iringa, ni ukombozi  mpya  wa  uhai  wa  wanyama katika  Hifadhi ya Taifa ya  Ruaha. Pia kielelezo kwa Watanzania kuendelea  kupata  umeme  wa  uhakika kupitia Bwawa  la Mtera, mkoani  Iringa.

Ni vigumu kuamini jinsi wanyama  katika Hifadhi ya Taifa ya  Ruaha  mkoani  Iringa  wanavyopoteza maisha  kutokana na uharibifu wa mazingira   katika  vyanzo  vya  maji vinavyopeleka mto mkuu  wa Ruaha.

Zipo  harakati mbalimbali  za  kuhakikisha suala la  utalii  katika  mikoa ya kusini inaboreshwa, japo Watanzania wengi hawajui iwapo hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo kusini mwa Tanzania ndio hifadhi kubwa kuliko zote nchini.

Nasema hivyo kwa sababu Watanzania  leo hawajausahau ule wimbo maarufu uliokuwa ukiimbwa katika shule za msingi kwa miaka mingi, ‘mbuga za wanyama Tanzania’.

Mbali na hifadhi ya Ruaha, katika mikoa hiyo kuna hifadhi nyingine kama Udzungwa, Kitulo na Katavi ambazo umaarufu wake unakua siku hadi siku.

Wakati wimbo uliokuwa unasifia mbuga za Tanzania ukiwa haupotei vinywani mwa Watanzania, Hifadhi ya Ruaha ilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1,300 tu wakati  leo kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Dk. Christopher Timbuka, anasema hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 20,380.

Ukubwa huo unaifanya hifadhi hiyo iwe kubwa kuliko zote Tanzania na ya pili kwa ukubwa barani Afrika, baada ya Hifadhi ya Kruger iliyopo Afrika  Kusini; Hifadhi ya Serengeti inakuwa ya pili kwa ukubwa nchini ikiwa kilomita za mraba 14,763.

Dk. Timbuka anasema ukubwa wa eneo  la Hifadhi  ya Taifa  ya Ruaha  inatokana na  kuongezwa katika hifadhi hiyo, bonde la Ihefu linalopakana na Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.

Pamoja na  sifa  kubwa ya  hifadhi ya  Ruaha  Iringa,  changamoto  kubwa  inayoikabili  hifadhi  hii na kutishia  uhai wa  wanyama ni uharibifu  wa  vyanzo  vya maji  na hata kupelekea  wakuu  wa mikoa ya Mbeya, Njombe na  Iringa  pamoja na wadau wengine kuja na mkakati huu wa kuanzisha tuzo za uhifadhi za mazingira chini ya udhamini wa TANAPA.

Tuzo hizi  zimekuwa  sehemu ya  kufanya wananchi kujua hasara na faida ya utunzaji  wa mazingira na iwapo elimu  hii itaenea, hakuna mwananchi atakayeharibu mazingira wala kufanya ujangili.

Mapema  mwaka  huu,  Makamu wa Rais, Samia Suluhu, alizindua kikosi kazi cha kunusuru ikolojia ya Mto  Ruaha, kikosi ambacho kimefanya  tathmini  na kuanza kazi ya kunusuru mto huo japo mbali ya kikosi  hicho  pia jitihada  za TANAPA katika  kuelimisha jamii  zimekuwa  zikifanyia ili kuepusha uharibifu  wa  mazingira.

Kazi  hii  kwa wanasiasa wamekuwa wakiipuuza na kuona kama ni mwiba wa wao  kukosa kuchaguliwa ama kuchukiwa na wananchi waliowachagua, hata  kuamua kuwatetea wananchi wanaolima ndani ya  mita  60 kutoka  kwenye vyanzo  vya maji ama mapito ya maji

Mkuu wa Mkoa  wa  Iringa, Amina Masenza, anasema Serikali ya mkoa itahakikisha inatekeleza maagizo ya ofisi ya Makamu wa Rais kwa  kulinda Mto  Ruaha  mkuu na kuwa katika  suala  hilo  hakutakuwa na huruma kwa  wote  wanaovunja  sheria  za uhifadhi wa mazingira.

Mkuu  huyo  wa mkoa  anasema  kuwa lazima  shule  zote  za Mkoa  wa  Iringa  kuingia katika mashindano hayo ya  tuzo  za Tanapa  ili  kujenga  utamaduni wa  wanafunzi  kuendelea  kutunza mazingira.

Anasema  kuwa  kuazishwa  kwa mashindano hayo ya  tuzo  za TANAPA kwa  ajili ya uhifadhi wa mazingira  ni zaidi ya  uhifadhi  na kuwa lazima  wananchi wote  wanaozunguka  wilaya  za  mikoa ya  Mbeya, Njombe na Iringa  kujitokeza kushiriki mashindano hayo.

Mkuu wa wilayani Kilolo, Asia Abdalah, anasema wananchi  wa  wilaya hiyo lazima kuwa  mabalozi  wema  katika  utunzaji  wa mazingira  na  kuwa Serikali haitasita  kuwachukulia  hatua kali wote  wanaokwenda  kinyume na maagizo ya  uhifadhi mazingira.

Kwamba, Serikali ipo mbele kuokoa  ikolojia  iliyoharibika katika Mto Ruaha  Mkuu na tayari Samia Suluhu  ameunda  kikosi  kazi cha kunusuru  ikolojia  ya  Mto  Ruaha mkuu kwa  faida ya wanyama na  wananchi ambao  wanategemea  umeme  unaozalishwa na mto  huo.

Mkuu  huyo wa  wilaya akiwa katika  Kata ya Udekwa, Wilaya ya Kilolo,  wakati wa uzinduzi  wa shindano la tuzo  za   uhifadhi wa mazingira  lililoandaliwa na Shirika la  Hifadhi za Taifa (TANAPA).

“Lengo la  Serikali ni kuona  wananchi  wake  wanafanya  shughuli zao za  kilimo kwa  kuzingatia sheria za mazingira, hivyo ni lazima kila mmoja  kuchunga sheria za uhifadhi wa mazingira   hivyo kila mmoja ahakikishe hakuna anayeharibu mazingira.”

Anasema  iwapo  mazingira  yataharibiwa  kwa  sasa  ni  pigo  kubwa  kwa  vizazi  vijavyo,  hivyo  kuanzishwa tuzo hiyo ya uhifadhi wa mazingira  iwe  chachu  kwa  wananchi kujitokeza  kushiriki  kulinda mazingira  yanayowazunguka.

Meneja  wa ujirani  mwema Tanapa,  Ahmed  Mbugi,  anasema tuzo   hiyo  imeanzishwa  kwa  ajili ya  kuendeleza  uhifadhi na  utunzaji wa mazingira  itashirikisha  wilaya  za Chunya, Mbarali  mkoani  Mbeya, Wanging’ombe na Makete Mkoa wa Njombe kwa Mkoa wa Iringa ni Mufindi  na  Kilolo.