Home Latest News TWAWEZA NI RAFIKI WA CCM, ISINYONGWE

TWAWEZA NI RAFIKI WA CCM, ISINYONGWE

4678
0
SHARE

NA BOLLEN NGETTI                       |               


WIKI iliyopita tulichambua namna Serikali ya awamu ya tano imeingiwa kiwewe, imevimba kwa hasira inayowaka moto kutokana na ripoti ya utafiti wa kitaalamu iliyotolewa hivi karibuni na taasisi ya TWAWEZA ikionesha kuporomoka kwa umaarufu wa Rais John Magufuli kutoka 96% (2016) hadi 55% (2018). Endelea.

CCM inatakiwa ikutane na kuketi kitako kutafakari kwa kina ripoti hii ya Twaweza. Tafakuri yao ijikite katika mambo haya: Kwanza Rais Magufuli aliingia madarakani kwa kupata kura 52.8% sawa na watu zaidi ya 8 milioni akifuatiwa na Edward Lowassa aliyepata 38% sawa na watu 6 milioni. Magufuli alijipambanua kama jemedari wa kupambana na rushwa na ufisadi na kila mmoja anaona kwa macho vita hiyo ambapo wezi wengi wako magerezani na wengine mahabusu.

Rais amekuwa mstari wa mbele kupiga vita dawa za kulevya, amehuisha utaendaji wa watumishi wa umma kuondoa urasimu na maonevu, ameanzisha miradi mikubwa “iliyowashinda” watangulizi wake kama ujenzi wa reli ya kisasa ya kati, ujenzi wa kituo cha kufua umeme cha Stigler Gorge, ujenzi wa hospitali kila wilaya, mahakama ya mafisadi, kafufua shirika letu la ndege nakadhalika. Katika mambo haya ilitegemewa umaarufu wa Rais Magufuli kupanda kutoka asilimi 96 ya 2016 hadi 100% lakini umeporomoka hadi asilimia 55 ni kwa nini?

Miradi ya maendeleo inafanyika majimboni lakini bado umaarufu wa Wabunge umeanguka kutoka 68% (2016) hadi 44% mwaka huu. Akitahadharisha wabunge wake kuhusu kupiga kura ya kupitisha bajeti ya mwaka 2018/19 Spika Job Ndugai alisema; “naomba tutambue kuwa endapo tutapiga kura nyingi za hapana ili bajeti isipite Rais atalivunja Bunge ili turudi kwenye uchaguzi na ninajua ikitokea hivyo wengi wenu hapa hamtorudi.” Kwa nini Spika Ndugai anajua wabunge wengi hawatorudi bungeni? Je, ni kutokana na utafiti huu wa Twaweza kuwa umaarufu wa wabunge umeporomoka kutoka 68% hadi 44%? Kwa nini tumkubalie Ndugai lakini tutilie shaka Twaweza?

CCM itambue kuwa uzoefu mara nyingi unaonesha kuwa viongozi ngazi ya Urais waingiapo madaraka mara ya kwanza umaarufu wao huwa juu maana utendaji wao haujajulikana na hushuka wanapogombea mara ya pili maana tayari kila mmoja ameonja ladha ya uongozi wake hivyo idadi iliyokupenda mara zote hugawanyika walau kidogo ukichukulia mfano Jakaya 2005 alishinda Urais kwa asilimia 81 lakini 2010 akapata asilimia 68 tena kwa kazi ya ziada. Swali kwa waandamizi wa CCM kama Rais Magufuli alishinda kwa asilimia 52.8 na uzoefu huu ukawa na ukweli ndani yake 2020 (endapo atagombea) atashuka hadi kufikia asilimia ngapi?

Msemaji Mkuu wa CCM, Hamphrey Polepole akionesha kukubaliana na ripoti ya Twaweza amekaririwa na gazeti dada na hili, Mtanzania Toleo Namba 8963 akisema; “matokeo haya ni ya kipindi cha awali cha uongozi ninaamini kutokana na miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa matokeo haya yatabadilika mwakani kwa maana kwamba yatapanda.” Polepole anataja miradi mikubwa ya umeme, ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, madaraja, reli, gesi, huduma ya maji mijini na vijijini nakadhalika. Polepole anatakiwa kujiuliza kwani miradi hiyo inatekelezwa gizani Watanzania 1,241 hawaioni?

Polepole pia anapaswa kujiuliza mwakani sehemu kubwa ya miradi hii kama tegemeo la kupanda umaarufu wa utawala awamu ya 5 itakuwa haijakamilika. Lakini ni mwaka huo huo kutafanyika uchaguzi mkuu wa Serikali za Mitaa nchi nzima. Tafakuri imsukume kujiuliza kama 2016 Rais alikuwa 96%, 2017 akaporomoka hadi 71% na 2018 akashuka hadi 55% je, 2019 ataporomoka kutoka 55 hadi kufikia ngapi? Na je, kama yeye hapandi bali ni kuporomoka tu, basi 2020 ataporomoka hadi kufikia ngapi na ni katika Uchaguzi Mkuu kama atagombea?

Ripoti hiyo pia imeonesha wananchi 64% wanaona uhuru wa watu kujieleza kama inavyoelekezwa na Katiba Ibara ya 18 umetoweka huku asilimia 62 wakiona udhibiti wa vyombo vya habari kukosoa matendo maovu ya Serikali ukiimarika siku hadi siku ambapo wanasiasa na wana habari kadhaa wamekamatwa, wameteswa, wamefunguliwa mashitaka mapya al-maarufu uchochezi.

Utafiti huu wa Twaweza unaakisi kabisa kilichotokea huko nchini Libya. Kwamba chini ya utawala wa Kanali Muamar Gaddafi wananchi walikuwa na huduma zote muhimu kwa maisha yao kama maji safi na salama, umeme wa kutosha, usafiri wa anga na jangwani, elimu bure, huduma za matibabu. Gaddafi alienda mbali zaidi kwa “upendo” wake kwa wananchi wanyonge kiasi cha kuwekwa utaratibu wa kuozesha vijana wake kwa gharama za Serikali na hapo ungepewa nyumba ya kuishi kuanzisha maisha na mkeo. Lakini unajiuliza ni kwa nini Walibya bado walimgeuka Gaddafi na wema wake huu na hatimaye kumuua kwa aibu? Ni rahisi kujificha nyuma ya hoja mufilisi kuwa walichonganishwa na nchi za magharibi waliokuwa na wivu kwa utajiri wa Libya lakini ukweli ni kwamba wananchi wa Libya walinyimwa haki ya msingi ya kuzaliwa nayo binadamu, haki ya kusikilizwa, haki ya kutoa maoni kama tulivyoiweka ndani ya Katiba yetu, haki ya kukosoa na kukosolewa.

CCM ikubali kwamba hata nyumbani baba akileta mkate na siagi kila siku mezani ni haki ya mke na watoto kuhoji wapi anakopata fedha za kununua mikate na siagi hiyo kila siku ilhali baba wa jirani hafanyi hivyo!

Katika safu hii nimewahi kuandika, “kuna faida nyingi kuliko hasara kuwapa wananchi wako uhuru wa kuhoji, kukosoa na kusikilizwa maana kuwanyima uhuru huo kunaweza kuwafanya wakawa kimya nawe ukawaona ni wapumbavu lakini kwa kuwa ni binadamu wenye utashi tofauti na wanyama wa mwituni watatafuta tu namna ya kuongea na utalazimika kuwasikiliza kama ilivyotokea kwa Mfalme Luis wa Ufaransa karne ya 16 ambaye mkewe alishangaa wananchi wakiandamana kupinga maisha magumu naye akawauliza kwani hawana mikate ya kupaka siagi majumbani mwao wakala?”

Utafiti wa Twaweza ni ushahidi kuwa wananchi wanaongea na mioyo yao. Wanajililia na nafsi zao. Ni kengele ya hatari kukiamsha chama-tawala, CCM na Serikali kuwa huko tuendako kuna haja ya kujitathmini zaidi na kujipanga kimkakati badala ya kupambana na Twaweza.

Wasaidizi wa Rais wanapaswa kumwambia ukweli kiongozi wetu kama nia yao ni kumsaidia na si wanafiki. Wamueleze kuwa matukio kama ya watu kutekwa, kuteswa, kupotea katika mazingira yasiyoeleweka, watu kupigwa risasi hadharani na watu wasiojulikana na upelelezi usifike mwisho, watu kunyimwa kutumia haki yao kujieleza kwa njia ya maandamano, watu kuzuiwa kufanya siasa za uenezi, kupuuza hitaji la Katiba Mpya, viongozi wa dini kutishwa, vyombo vya habari kufungiwa na waandishi kukamatwa na kutiwa misukosuko, kuendesha bunge la wananchi na mahakama gizani, Serikali kujiona iko juu ya chama-tawala, Ubunge kuwa mali ya chama na si wananchi na mengine mengi ni mambo ambayo hata kama tungebadili barabara zote nchini kuwa treni za umeme na elimu bure kutoka Awali hadi ngazi ya Uprofesa bado umaarufu wa Rais usingebaki kileleni maadamu ni maendeleo ya vitu si ya watu.

Kuondoa dhana ya uongozi shirikishi na badala yake DC kuhisi wilaya ni mali yake, RC kuhisi mkoa ni mali yake hali kadhalika. Haya ni mambo ambayo hayawezi kumwacha salama Rais katika utafiti wowote utakaohusu umaarufu wake. Kwani hatujasikia viongozi wakisema, “katika mkoa wangu, katika wilaya yangu, katika Serikali yangu!” (rejea ushauri wa Waziri Mkuu mstaafu David Msuya kwa Rais Ikulu).

Ushauri pekee kwa CCM na Serikali kutoka safu hii ni kuacha kupambana na mawazo ya wananchi kupitia taasisi kama Twaweza na viongozi wa dini badala yake ijitafakari na kujitathmini. Ifanye utafiti kujiridhisha ukweli wa madai ili ijipange, ijisahihishe, ishindane kwa hoja si vioja vya kukata mauno ofisini mbele ya kamera kushangilia bajeti ya Serikali. Muda upo, tujisahihishe. Kidumu Chama Cha Mapinduzi.