Home Makala UADILIFU WA POLISI, TAKUKURU NA MAHAKAMA UTAPUNGUZA RUSHWA

UADILIFU WA POLISI, TAKUKURU NA MAHAKAMA UTAPUNGUZA RUSHWA

626
0
SHARE

NA GORDON KALULUNGA

NIANZE kwa kutoa pole kwa watu wote ambao wamepatwa na mikasa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufiwa au kudhulumiwa haki zao na wenye maamuzi ndani ya Serikali na katika sekta binafsi.

Najua bomoabomoa inaendelea katika mikoa mbalimbali hapa nchini na baadhi ya waliokumbwa naambiwa hawatalipwa fidia kwa sababu Sheria ya Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) ya mwaka 1932 inakataza kujengwa makazi ndani ya mita 120 kutoka katikati ya barabara kuu.

Kwa kawaida tunaambiwa kuwa kutokujua sheria si kinga ya kukupatia haki na hapo ndipo wengi machozi yao yanaishia katika mikono ya neno Mungu atatulipia.

Wiki iliyopita, Rais John Magufuli alimwapisha Brigedia Jenerali John Julius Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Katika hafla hiyo ambayo ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, rais aliipongeza Takukuru na kutoa rai ya kuendeleza mazuri waliyoyaanza, huku akikiri kuwa yanayoshughulikiwa sasa yanatokana na uwepo wa rushwa katika nchi yetu.

Kwa mantiki hiyo hiyo, baadhi ya wengi wanaohusishwa na rushwa walikuwa ni viongozi wa umma.

“Ukiangalia mambo makubwa tunayopambana nayo yanasababishwa na rushwa iliyosambaa kila mahali, watumishi hewa chanzo ni rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa, pembejeo za ruzuku ndani kuna rushwa na huko mahakamani nako ni rushwa tu,” ilinukuliwa taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Rais Magufuli aliongeza kwa kusema: “Na mimi kiongozi wenu nimeamua kupambana na rushwa na niwaombe nyote mshirikiane kuondoa rushwa katika maeneo yenu ya kazi”.

Ninaamini kabisa kuwa Rais Magufuli kuna mahali huwa anatumia sentesi za kifasihi kueleza hali waliyonayo baadhi ya watumishi katika ofisi za umma ambazo kwa sasa baadhi si kimbilio la wanyonge.

Serikali yoyote duniani hasa inayoendeshwa katika misingi ya utawala bora, huwa inasimama vema na kuheshimika pale watumishi wake wanaposimamia haki na wanatoa huduma kwa wakati bila kuwepo chembe za upendeleo au dalili za rushwa.

Wananchi wa Tanzania wanazo sehemu mbalimbali za kupata huduma na hapa nazungumzia ofisi za umma.

Kumekuwa na kilio ambacho machozi ya baadhi ya wananchi yamekuwa yakikaukia kwenye mashavu yao, baada ya vilio vyao kama si kupuuzwa basi kutosikika na watunga sera au watumishi wenye mamlaka ya kuchukua hatua.

Hivi sasa katika nchi yetu kumezuka mtindo kuanzia ngazi ya kitongoji kukiwa na malalamiko na wananchi wakipata nafasi ya kutoa maoni yao, utawasikia wakimuomba Rais Dk. John Magufuli asikie kilio chao.

Katika akili ya kawaida kabisa yaani akili ya mwanafunzi wa chekechea, inaonyesha ni jinsi gani baadhi ya wananchi wanavyomwamini rais wa nchi yao pekee kuwa ndiye anayeweza kuwa mkombozi na mfuta machozi yao.

Swali la kwanza la kujiuliza kuwa kwanini wananchi hawa wanataka sauti zao zisikilizwe na mkuu wa nchi badala hata ya wawakilishi wake huko waliko wananchi?

Je, wanawasingizia wawakilishi wa rais kuwa kuna mahali nao hawawezi kutenda haki kama wanavyofikiri na kwamba labda wamemezwa na wanaodhani kuwa wanawatesa kwa muda mrefu?

Ikumbukwe kuwa maumivu ya kutoa sauti inayoashiria kilio hasa kwa mwanamume ni hatua ya mwisho sana.

Je sauti hizi za wananchi zinaamua kutoka ili kufurahisha genge au wanazitoa kutokana na maumivu waliyonayo kwa muda mrefu na kuhisi kuwa rais wa nchi ndiye anayeweza sasa kuwasikiliza na kutoa haki kwa usawa?

Tunaweza kuendelea kujiuliza kuwa je, vyombo vinavyohusika kuchukua hatua na kutoa haki kwa wakati bila upendeleo vipo? Na kama jibu ni ndiyo, swali linakuja kuwa kwanini havijawa kimbilio la wanyonge?

Kwanini wananchi wanashawishika au kujishawishi kununua haki? Je kuna waporaji wa haki ndani ya vyombo husika au watoa huduma wa Serikali?

Anayejua haya nitampa nafasi atusaidie kama Taifa maana tumeambiwa kuwa ukilalamika bila kuwataja wahusika kukiona.

Baadhi wanavitaja vyombo kama mabaraza ya kata, polisi, Takukuru, mahakama na sehemu nyingine serikalini ambako ndiko zinapatikana huduma za umma kuwa kuna baadhi ya watendaji wasio waaminifu.

Sentensi kama hizi zinashtua sana lakini tukiamua kujisahihisha basi tuumeze ukweli mchungu ambao ama unalenga kutuimarisha kiutendaji au unalenga kufufua matumaini mapya ya raia ili hata tukiuawa au kufanyiwa jambo baya raia wawe wa kwanza kutulilia.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa mkoani Mbeya, alisikika akiwaambia Takukuru kuwa wawashikilie watuhumiwa wa sakata la Soko la Mwanjelwa, lakini wasiandae mashtaka wao bali angetuma kikosi maalumu kutoka ofisi yake.

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu aliitolea katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkapa uliopo jijini Mbeya, ambayo kwa wachambuzi wa mambo ya kijamii na waumini wa Azimio la Arusha ambalo lilikuwa na misingi imara zaidi kuhusu uadilifu na uongozi wa umma, zikatujia tafakuri nyingi ambazo zinaambatana na hisia za baadhi ya wananchi kuhusu uadilifu wa baadhi ya watumishi wa umma.

Binafsi sina shaka kabisa na misingi na uimara wa vyombo vyetu vilivyopo kisheria, ila kelele zilizoko nyikani ni nyingi sana na bahati mbaya sana hata ambao hawajawahi kutendewa wao, lakini nao wameambukizwa kuimba wimbo ambao haina kiashiria chema na kwa sasa sauti zao wanazielekeza kwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu.

Watendaji wa mabaraza ya kata, polisi, Takukuru na mahakama ni waadilifu sana na sina shaka nao na ninaamini kuwa kwa sasa wakijitahidi kuulinda na kuuimarisha uadilifu wao kwa umma, baadhi ya kelele zitapungua kama si kutoweka kabisa na hakika vyombo hivi vitakuwa kimbilio zaidi la wanyonge.