Home kitaifa UBABE, UTATA KIFO CHA FARU JOHN GUMZO 2016

UBABE, UTATA KIFO CHA FARU JOHN GUMZO 2016

2335
0
SHARE

Na ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

KWANZA ifahamike kuwa ninapoandika makala haya, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kasimu Majaliwa, ameunda Kamati maalumu inayochunguza sakata la kupotea au kufa katika mazingira yasiyoeleweka ya Faru aliyekuwa akiishi Ngorongoro Kreta.

Pia ieleweke kuwa sina lengo la kuingilia Kamati ya Waziri Mkuu, isipokuwa ninataka kueleza kwa kiasi ninachofahamu kuhusu mnyama huyo, ambaye amepata umaarufu wakati akiwa mzoga pengine kuliko alipokuwa hai.

Ngorongoro Kreta ndilo eneo pekee katika Afrika ambako wanyama aina ya faru wanatembea kwa uhuru, bila kuzuiwa na kuzingwa kwa uzio wa aina yoyote. Mazingira yao ya asili bado hayaja haribiwa na shughuli za kibinadamu.

Ni katika mazingira hayo ndimo aliishi faru  aliyeitwa John, ambaye kwa mujibu wa wanasayansi ya wanyama pori, yeye alikuwa dume la mbegu, yaani kwa lugha yao ya  kitaalamu anaitwa ‘Alpha Mailed’.

Faru John alikuwa na kazi tatu kubwa na maalumu—kula chakula cha kutosha (nyasi), pili akisha kushiba, kazi inayofuata ni  kujamiana na faru majike wanaoishi humo, halafu anafunga ratiba yake ya siku kwa kuwapiga faru wengine au kama kuna faru dume mwenye uwezo wa kupambana naye, basi hupimana ubavu.

Kutokana na ubabe wake, alilichukua eneo lote la Bonde la Ngorongoro kama himaya yake binafsi (territory) na hakutaka kabisa wanyama wengine na hasa faru, waonekane katika upeo wa macho yake—achilia mbali faru dume—kujamiiana na majike walio katika himaya yake.

Kwa mujibu wa taarifa za wataalamu wa sayansi ya wanyama (zoology), ni kwamba tangu alipokuwa ‘mtawala’ wa himaya hiyo, Faru John tayari alishaua faru wengine wawili waliojaribu kutikisa utawala wake, kuharibu miundombinu, kuharibu magari ya hifadhi, lakini pia katika vita hivyo dhidi ya maadui zake, yeye mwenyewe alipoteza jicho moja kiasi cha kuhatarisha maisha yake kutokana na kisasi kutoka kwa wanyama wengine wakali wanaoishi ndani ya bonde hilo.

Si hivyo tu, bali pia jambo ambalo ni baya zaidi na laana katika kizazi cha wanyama hao kama ilivyo kwa binadamu, Faru John alianza kujamiana na watoto wake mwenyewe, kitendo ambacho wanasayansi ya wanyama pori waliona kuwa ingehatarisha afya ya faru watoto ambao wangezaliwa.

Sasa kwa sababu yeye hakutaka faru wengine wajamiiane na majike, na kwa upande mwingine, na laana ya yeye kuzaa na wanawe, ikaonekana jambo hilo linatishia mwendelezo wa kizazi cha wanyama hao adimu. Hivyo huenda faru wangetoweka kabisa katika eneo hilo.

Mazingira hayo ndiyo yalikutanisha wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanayamapori Tanzania (Tawiri), Mamlaka ya Ngorongoro, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), na Chama cha Zoolojia cha Frankfurt (Frankfurt Zoological Society) cha Ujerumani, na kwa pamoja wakakubaliana kumtoa Faru John kutoka Ngorongoro Kreta na kumpeleka eneo salama kwa uhai wake. Kwa pamoja, watalaamu hao wakakubaliana kwamba apelekwe kwenye pori la Sasakwa Grumeti.

Faru huyo aliyekuwa na umri usiozidi miaka 38, baada ya kuishi katika mazingira hayo mageni kwake, na yenye upweke kwa namna fulani ikilinganishwa na kule kreta alikotoka, na pia kutokana na maradhi yaliyompata, alikuwa akidhoofika siku hadi siku na hatimaye alikufa.

Kifo cha Faru John kama nilivyosema awali, kilikuwa kifo cha kawaida kama wanavyokufa wanyama wengine, lakini liliibuka ghafla Desemba 6, mwaka huu, wakati Waziri Mkuu alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, sakata zima la Faru John, lilikuwa limejaa vitendo vya rushwa na wizi, hivyo asingeweza kuvumilia, kwani anasema aliuzwa kwa shilingi milioni 200 kwa wamiliki wa hoteli ya Grumeti, na waliofanya biashara hiyo tayari walipokea nusu ya fedha hizo.

Majaliwa alitoa siku mbili kwa wahusika wote, kumpatia taarifa za faru huyo akiwa hai, au akiwa amekufa basi pembe zake na nyaraka zingine zinazohusu kifo cha Faru John, ziwe zimemfikia ofisini kwake ikiwa ni pamoja na kutambua mabaki ya mzoga, na hata kaburi ikiwa alizikwa.

Suala hili la mabaki au kaburi la Faru John lilisababisha tafrani na mijadala isiyokuwa na kikomo katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kila chombo kikitafsiri kwa namna yake na kutoa tafsiri yake.

Mwanasayansi na mtafiti kutoka Tawiri, Dk. Ernest Mjingo, yeye anasema mara nyingi wanyama wanaozikwa, ni wale waliokufa kutokana na magonjwa ya mlipuko kama kimeta, lakini wanyama wanaokufa vifo vya kawaida (natural death), huwa hawazikwi kutokana na sababu za kiikolojia.

“Wanyama wanaokufa kawaida hatuwafukii, na sio kuwazika, bali wanabaki pale pale walipofia labda kama wataliwa na wanyama wengine na hii ni kutokana na sababu za kiikolojia. Isipokuwa wale wanaokufa kwa magonjwa ya mlipuko, tunawachoma moto na kupuliza dawa maeneo yote yenye mizoga.

Hili ndilo sakata la Faru John ambaye pengine suala lake limetumika kuficha jambo lingine kubwa zaidi ambalo wahusika wasingependa Waziri Mkuu alifahamu, ili wasitumbuliwe. Ni suala la muda tusubiri kusikia tume ya Majaliwa kuhusu Faru John itakuja na matokeo gani.